Sehemu iliyopita, mwandishi alieleza namna watu wa koo za Boroko la Loita kutoka Kenya walivyoingia Loliondo na kuonekana ndiyo wakazi halali wa eneo hilo. Anaeleza pia chanzo cha mgogoro Loliondo akisema ni vita ya uchumi ambayo sasa imepata kasi kutokana na raia wa kigeni na NGOs zinazofadhiliwa na mataifa ya Ulaya na Marekani. Endelea.

Dunia ya leo inazungumza lugha moja, “Uhifadhi wa mazingira, kutunza vyanzo vya maji na mabadiliko ya tabianchi”. Lakini sisi wana-Loliondo tumekuwa mabingwa wa kuharibu mazingira, vyanzo vya maji na mazalia ya wanyamapori huku tukijinasibu kuwa ni wahifadhi na watunzaji wazuri wa mazingira.

 

Kama sisi ni watunzaji wazuri wa mazingira kwanini vijito na mito iliyokuwa ikitiririsha maji miaka ya 1970 katika maeneo yetu sasa imekauka na kuongezeka kwa vipindi virefu vya ukame kuliko huko nyuma? Katika maeneo yetu tuna vitalu vingapi vya miche ya miti? Tumepanda miti mingapi angalau kwenye maboma au vyanzo vya maji kurudishia vinavyokauka? Maboma yetu yote tunayoishi tunajenga kwa miti, huko ndio kuhifadhi au ni kuharibu mazingira?

 

Katika maeneo yetu ni maboma mangapi yenye vyoo vya kisasa zaidi ya vyoo vya asili? Silaha zetu zote za jadi hutokana na miti, nishati yetu yote hutokana na miti, mapambo yetu mengi ya utamaduni wa asili hutokana na wanyamapori. Ujangili umeongezeka katika maeneo yetu kutokana na jamii kushirikiana na Wasomali kuliko awali; huko ndiko kutunza na kuhifadhi mazingira?

 

Sisi ni wafugaji, lakini mapato yatokanayo na mazao ya mifugo yanainufaisha nini Tanzania zaidi ya nchi jirani? Kama ilivyo adha kwa wanyamapori waliopo Pori Tengefu Loliondo ni sawa na ilivyo gesi ya Mtwara, tanzanite ya Merereni, almasi ya Mwadui, dhahabu ya Buzwagi n.k. Lazima tuwatunze nao watutunze.

 

Sikubaliani na jinsi OBC Limited ilivyopewa mkataba wa uwindaji Loliondo kutoka Ikulu mwaka 1993. Imekiuka kwa maksudi kanuni za uwindaji na inachokifanya sasa kwa kujenga majengo ya kudumu karibu na chanzo cha maji kwani ma-ecologist nguli wanasema Loliondo ni ukanda wa Somali-Maasai Regional Centre of Endemism [phytochorion] wenye sifa ya kuwa na zaidi ya asilimia 50 ya viumbe na mimea adimu duniani [flora and fauna].

 

Tunao viongozi wa kuhoji na ku-review mkataba wao kuanzia ngazi ya madiwani hadi bungeni, tena mbunge wetu amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira. Mkataba wao unaoisha mwaka 2018. Ni vizuri mikataba  ya kampuni nyingine za uwindaji Loliondo nayo iwekwe  wazi kwa wananchi badala ya kulalamika tu kwamba nia ya Serikali ni kuiongezea kampuni ya OBC Limited eneo bila ushahidi usio acha shaka.

 

Kimsingi hoja zinazotolewa na madiwani wetu zimekosa msingi, kwani ni hoja za nguvu badala ya nguvu ya hoja; hivyo kujaa hadaa na kushindwa kupiku hoja makini za Balozi Kagasheki kimizania. Nawashauri wanasiasa na NGOs Loliondo kasi na nguvu walizotumia kusambaza mgogoro huu wazitumie kutuletea maendeleo kuliko kulumbana.

 

Wanaharakati na wanasiasa watuambie kabla ya kuja wawekezaji kwenye pori tengefu wanyamapori walikuwapo, walikuwa wanatunufaisha nini? OBC, kampuni za Wazungu, vijiji na pori tengefu kila moja anamiliki ardhi yenye ukubwa gani? Wawekezaji wote wakiondoka na Serikali kuturudishia pori tengefu litatunufaishaje zaidi ya kuchungia mifugo na kuzikaribisha koo za Boroko na Loita?

 

Kuliko madiwani wetu kuendelea kusambaza sumu ya migogoro, wasidhani wananchi bado tupo gizani, bali washughulikie matatizo yetu kwani mwaka 2015 si mbali. Tena kero zetu zote wameshindwa kuzitatua hadi sasa, mfano aibu ya njaa za kila mwaka, mitandao mibovu  ya barabara, matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa binadamu na mifugo, mifumo dume katika jamii zetu [ukatili wa kijinsi], ukeketaji, haki za watoto wa kike kumiliki mali [ardhi], huduma duni za afya [afya ya mama na mtoto], kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika, wilaya nzima kutokuwa na kidato cha tano n.k.

 

Niwatahadharishe wana-Loliondo wenzangu, wanasiasa na NGOs tusijisahau. Loliondo ndiyo mama na baba yetu. Ndiyo mahali pekee panapotufaa sisi kuishi. Uzuri na utajiri tuliopewa bure na Mungu tuutumie kwa manufaa yetu. Tusilishwe maneno wala kugombanishwa ili kuzalisha migogoro. Tuchunguze kwa makini maneno tunayoambiwa na wanasiasa wetu maana shetani hujificha kwenye maelezo.

 

Kampuni za uwekezaji zilizojazana Loliondo zinaiona ardhi yetu ni lulu kwa sababu ya wanyamapori tulionao; siku wakitoweka nao wataondoka na kutuachia ardhi na shida zetu kama walivyo wawekezaji kwenye madini.

 

Hivyo, yeyote anayepinga mpango wa Balozi Kagasheki haitakii mema Loliondo wala hifadhi nyingine za taifa na pengine ni mhujumu maendeleo yetu na endapo madiwani wetu wataendelea na mgogoro huu, ni heri Pori Tengefu Loliondo liunganishwe na SENAPA kwa manufaa ya umma kuliko ilivyo sasa maana hatunufaiki.

 

Kampuni za uwindaji na Azaki Loliondo

Loliondo kuna kampuni nyingi za uwindaji na upigaji picha za utalii. Baadhi ya kampuni hizo ni OBC Ltd [Waarabu], And Beyond, Thomson Safaris, Dorobo Tours and Safaris, Sokwe Asilia, Nomad Safaris [Ulaya na Marekani] n.k.

 

Miongoni mwa asasi za kiraia [NGOs] zilizopo Loliondo ni NGONET, PINGOS Forum, Ujamaa Community Resource [U-CRT], Pastoral Women Council [PWC] n.k. Miongoni mwa asasi hizi hufadhiliwa na kampuni za Wazungu zilizowekeza Loliondo.

 

Baadhi ya maswali ya kujiuliza, ni kwanini baadhi ya NGO hizi ofisi zao zipo ndani ya ardhi inayomilikiwa na kampuni za wawekezaji wa Kizungu? Kwanini baadhi ya viongozi wake ni wakurugenzi wa NGO hizo? NGOs zinazofadhiliwa na kampuni za Wazungu kuna siku zitatetea kampuni ya Kiarabu?

 

Kuna taarifa kuwa OBC Limited inalipa tozo zote kwa mujibu wa mkataba wake na Serikali, huchangia kwa asilimia kubwa maendeleo ya wananchi katika eneo husika, huchangia mapato ya wilaya na pato la Taifa. Je, hizi kampuni nyingine za Wazungu zinachangia nini kwa wananchi, Halmashauri ya Wilaya na Serikali Kuu? Kwanini hizi NGOs na baadhi ya madiwani wanaichukia OBC Limited na kusingizia kuwa inachukiwa na wananchi bila kueleza sababu za kuichukia?

 

Kimsingi, sababu za mnyukano huu ni utajiri wa maliasili na rasilimali zilizopo Loliondo, wivu wa mapato mengi yatokanayo na uwindaji, utalii na upigaji picha, woga wa kimaslahi na ushindani wa kibiashara kutoka kwa kampuni ya OBC Ltd. Mbinu nyingi halali na chafu hutumika ili kuwadhoofisha washindani wengine kibiashara. Baadhi ya mbinu zinazotumiwa na kampuni hizo ni wawekezaji kuanzishia wanaharakati NGOs kwa ajili ya kuwatetea na nguvu za kisiasa na siasa.

 

Ikumbukwe kuwa huko nyuma NGOs hizi  ziliwahi kutumia taasisi za kimataifa kutoa matamko ya kuipinga Serikali katika mradi wa kujenga barabara ya lami kutoka Kigongoni-Selela-Ngarasero-Loliondo-Natta-Mugumu-Makutano kwa kisingizio cha kulinda mazingira na ikolojia ya mbuga ya Serengeti.

 

Hao hao ndiyo waliopinga ujenzi wa kiwanda cha chumvi na magadi ukanda wa EPZ Ziwa Natron kwa kisingizio cha kuharibu mazingira na ikolojia ya asili ya mazalia ya ndege aina ya flamingo. Lakini hao hao leo ndiyo wanaopigia chepuo kilimo cha kujikimu ndani ya Mamlaka ya Ngorongoro.

 

Lakini hawakupinga ujenzi wa barabara ya lami mbuga ya Maasai Mara, hawakupinga ujenzi  uwanja bubu wa ndege Loliondo mpakani mwa Tanzania na Kenya, hawakupinga ujenzi wa kiwanda cha chumvi na magadi soda Ziwa Magadi wala ujenzi wa reli. Lakini kwa upande wa Tanzania tukiyafanya hayo ni haramu na hatupaswi kutumia rasilimali zetu kwa maendeleo yetu hadi tukawaombe kibali! Jamani hapa tunajifunza nini?

 

Aghalabu, Serikali imeshayajua hayo yote kupitia kwa jamii, Usalama wa Taifa, usalama wa raia au intelijensia ya Polisi; sasa ianzishe chombo mahsusi cha kusajili, kusimamia na kuratibu kazi za NGOs zote nchini na pengine kujua vyanzo vya mapato na matumizi yake, maana haiingii akilini eneo dogo kama la Loliondo kuwe na NGOs 37 huku walengwa wa misaada hiyo wakiendelea kuwa maskini wa kutupwa kweli kweli.

 

Nani anayefadhili migogoro ya ardhi Loliondo?

Wafadhili wakuu wa migogoro ya ardhi Loliondo ni kampuni za kigeni za uwekezaji kupitia NGOs zilizotapakaa eneo dogo la Loliondo, kwa kuwalisha sumu ya migogoro baadhi ya viongozi wa kisiasa wilayani Ngorongoro kwa maslahi binafsi. Nao huisambaza kwa wananchi ili waichukie OBC Limited na Serikali yao kwani kiongozi wa mila akisema jambo hata kama ni la ovyo ni amri inayopaswa kutekelezwa na yeyote bila kuhoji.

 

Kamati ya Nchemba

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, baada ya kuombwa na Mbunge wa Ngorongoro, Kaika ole Telele, aliunda kamati ya kukusanya maoni ili baadaye yatumike kuishauri Serikali namna bora ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

 

Kamati hiyo iliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba. Wajumbe wengine walikuwa ni Lekule Laizer [Longido-CCM], Christopher ole Sendeka [Simanjiro-CCM) na Mary Chatanda ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha.

 

CCM ilifikia uamuzi huo baada ya mgogoro huo kushika kasi na viongozi wote wa kuchaguliwa wa CCM kuanzia wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa vijiji, madiwani na wengine kutishia kujiuzulu nyadhifa zao iwapo Serikali itatekeleza uamuzi wake wa kuhifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500 kati ya 4,000 katika eneo la pori tengefu. Uamuzi huo uliazimiwa na baadhi ya madiwani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Olpiril.

 

Itaendelea

 

Please follow and like us:
Pin Share