Washington, Marekani

Jopo la washauri wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) limekumbana na mvutano mkali wakati wa kupitisha mapendekezo ya kuanza kutolewa kwa nyongeza ya chanjo ya corona (Covid-19) kwa waliochanjwa chanjo ya aina ya Pfizer nchini Marekani.

Chanjo hiyo ya nyongeza imezinduliwa kwa ajili ya wazee na watu waliomo katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

Kupitishwa kwa chanjo hiyo kunafungua ukurasa mpya kwa taifa hilo kuhakikisha linaondoa maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa CDC, Dk. Rochelle Walensky, ametia saini mapendekezo hayo katika mkutano uliokutanisha wataalamu huku mlolongo wa mapendekezo yaliyotolewa yakipingwa na wajumbe wa jopo hilo.

Jopo la wataalamu hao linashauri chanjo hiyo ya nyongeza wanapaswa kupewa watu wenye umri kuanzia miaka 65, wazee, wauguzi na watu wenye umri kuanzia miaka 50 hadi 64 wenye matatizo ya kiafya lakini linapingana na baadhi ya mapendekezo.

CDC inashauri kuwa itakapopita miezi sita, waliochanjwa Pfizer watatakiwa kuchanjwa dozi nyingine ya nyongeza ndipo utaratibu wa kuchanjw chanjo ya corona utakuwa umekamilika.

Pendekezo la Dk. Walensky la kuwataka wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 64 wanaofanya kazi katika vituo vya afya na katika mazingira hatarishi kupata chanjo kwa umuhimu wa afya zao limepingwa na jopo hilo.

Pamoja na pendekezo hilo kupingwa na jopo hilo, bado Dk. Walensky amelirudisha katika mapendekezo ya awali huku hatua hiyo ikikusudia kulenga kile ambacho Mamlaka ya Chakula na Dawa (FDA) katika taifa hilo ilikizingatia wakati wa kupitisha mapendekezo yake wakati wa uidhinishwaji wa chanjo hiyo ya nyongeza.

Kipengele kilichoongezwa katika mapendekezo ya watu wanaotakiwa kupata chanjo ya nyongeza ni pamoja na watu walioko gerezani, watu wasio na makazi maalumu na wafanyakazi wa sekta za afya.

Pia jopo hilo limekosoa mapendekezo hayo likiamua kuongeza kipengele cha uhiari kwa watu wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 49 wenye matatizo sugu ya afya na wale wenye uhitaji bila kuwa na matatizo yoyote ya kiafya.

Washauri katika jopo hilo wamekataa kwenda mbali zaidi kuhusu kipengele hicho na badala yake wameweka wazi kuwa wafanyakazi katika vituo vya afya wanaweza kukubali kupokea chanjo hiyo ili kujikinga kuugua mno na maambukizi mapya.

Katika mkutano wa kupitisha mapendekezo hayo, jopo limepiga kura kuyapitisha huku kura tisa za wahudhuriaji zilikubaliana na mapendekezo hayo huku sita zikiyapinga na kuna mengine Dk. Walensky akikataa kukubaliana nayo.

Pamoja na majadiliano kuchukua muda mrefu, Dk. Walensky, ametoa msimamo wake akionyesha kukubaliana na mapendekezo yote.

“Kama Mkurugenzi wa CDC, ni kazi yangu kutambua ni wapi tunatakiwa kuchukua hatua ili tupate matokeo makubwa,” anasema Dk. Walensky na kuongeza:

“Hapa CDC tumepewa kazi ya kuchambua takwimu, nyingine haziko sawa ili tuzifanyie mapendekezo kwa mustakabali wa afya.

“Katika janga kubwa, ambapo hali haieleweki, tunatakiwa kuchukua hatua ambayo tunaamini itafanya vizuri kabisa.”

Wataalamu wanadai kuwapatia chanjo watu wasiochanja hata ile ya kwanza ndiyo njia sahihi kuliko ambavyo jopo la CDC limeanza kuvutana kuhusu ile ya nyongeza huku wakidai ni kutoka kwenye lengo.

Wanadai chanjo zote tatu zinazotolewa nchini Marekani bado zinao uwezo mkubwa wa kudhibiti maambukizi kwa kuzuia mtu asiugue kwa kiwango kikubwa, kulazwa na muda mwingine kuzuia kifo katika kipindi hiki cha kusambaa kwa aina ya kirusi kipya cha Delta.

Takriban watu milioni 182 nchini Marekani wameshapata chanjo na idadi hiyo ikionyesha kuwa ni asilimia 55 ya watu wote walioko katika taifa hilo.

Mkufunzi wa Chuo cha Vanderbilt, Dk. Helen Talbot, anasema kutoa chanjo ya nyongeza si suluhisho kwa janga la corona.

“Hospitali zimejaa wagonjwa ambao hawajachanjwa, tunakosa kuwa makini kwa watu wanaohitaji uangalizi wetu kwa sababu tuna watu wengi ambao hawajachanjwa,” anasema Dk. Helen.

Mpango wa CDC unakuja siku chache baada ya Ikulu ya Marekani kuutangazia umma wa taifa hilo kujiandaa na chanjo ya nyongeza kama lengo la kupambana na ugonjwa corona.

Hata hivyo, jopo la wataalamu wa FDA na CDC wameupokea kwa mwitikio mdogo kinyume cha matarajio ya Ikulu ya Marekani.

Mpango wa chanjo ya nyongeza unaweka mabadiliko muhimu katika taifa hilo huku mataifa kama Uingereza na Israel yenyewe yakiwa yamefika hatua ya kutoa chanjo tatu za nyongeza kwa watu wake.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapingana na hatua ambayo mataifa hayo yamefikia katika utoaji wa chanjo ya nyongeza yakidai kuwa mataifa maskini hayajafanikiwa hata katika chanjo ya kwanza.

Katika mkutano wa kuzinduliwa kwa chanjo ya nyongeza, Dk. Walensky, anasema kuwachanja wasiochanjwa kunabaki kuwa mkakati unaopewa kipaumbele kikubwa Marekani na duniani kote.

Kwa upande wa watu waliochanjwa chanjo ya Moderna na Johnson & Johnson, CDC wanasema bado serikali haijakusanya takwimu za kutosha kuiwezesha kutambua kama waliochanjwa chanjo hizo wanatakiwa kupata chanjo ya nyongeza.

CHANZO: CBS 

By Jamhuri