Mwarobaini ni mojawapo ya mimea maarufu yenye kinga dhidi ya wadudu waharibifu. Ndani yake kuna dawa inayoweza kutolewa kwa urahisi na kutayarishwa na kutumika kama dawa ya mimea ya kuulia wadudu.

Hata hivyo, dawa hii haiathiri wadudu wote kwa wakati mmoja. Kuna aina ya wadudu wanaoathirika mapema kuliko wengine, na athari yake kwa wadudu wengine huchelewa.

Jinsi mwarobaini unavyofanya kazi

Wadudu mbalimbali, hasa nzige, hawapendi harufu ya mwarobaini. Dalili huanza kuonekana baada ya kunyunyizia maji yenye mwarobaini, wadudu huacha kula kwa sababu harufu na ladha ya mimea iliyonyunyiziwa dawa si nzuri.

Utafiti wa kitaalamu umebaini kuwa aina nyingine ya wadudu wanaokufa muda mfupi baada ya kula majani au sehemu nyinginezo za mmea zilizonyunyiziwa dawa ya mwarobaini, ni pamoja na viwavijeshi ambao hufa siku moja au tatu baada ya kula mimea iliyonyunyiziwa dawa hiyo.

Pia kuna wadudu wengine ambao huathirika kwa kubadili mwenendo au tabia zao na kupoteza uwezo wa kutaga mayai. Vilevile kuna aina za wadudu wanaoathirika kidogo, au hawapati madhara yoyote kutokana na dawa ya mwarobaini.

Dawa hii ya mwarobaini ina uwezo mkubwa wa kutibu ugongwa wa mnyauko ambao unaathiri migomba. Mikoa ya Kagera, Mara na Morogoro imekuwa ikikumbwa na ugonjwa huo.

Namna ya kutayarisha dawa ya mwarobaini

Utafiti umebaini kuwa kwa kawaida matunda ya mwarobaini hudondoshwa chini na ndege, popo na wengineo, hivyo mbegu zilizokwishamenywa zinaweza kuokotwa chini ya mti huu.

Ili kuweza kutengeneza dawa hii ya mwarobaini, lazima uzingatie yafuatayo: Loweka matunda kwenye maji kisha sugua kwa viganja viwili au juu ya chekeche kubwa kwa sababu kuvuna mbegu kwa kutingisha ni kazi kubwa kuliko kuokota zilizodondoshwa na ndege.

Baada ya kuzitoa maganda, mbegu hazina budi kusafishwa kikamilifu. Utoaji wa maganda husababisha ukuaji mzuri wa mbegu. Mbegu zisipooshwa na zisipokaushwa vizuri zitaota ukungu ambao hupunguza nguvu ya dawa hii ya kuulia wadudu.

Ili kuepuka kuota ukungu, mbegu hazina budi kukaushwa vyema bila kulaliana, na kuanikwa kwenye kivuli sehemu ya uwazi kwa siku kadhaa hadi zikauke.

Kadhalika, ili kuepusha ukungu kwenye mbegu baada ya kukauka, itatakiwa mbegu hizi zihifadhiwa kwenye vyombo vyenye hewa ya kutosha kama vile magunia matupu.

Lazima mbegu za mwarobaini zikaangwe au kusagwa na kuwa unga. Unga huu uhifadhiwe kwenye chombo safi. Mbegu hutwangwa kuvunja ganda gumu la mbegu ili kutoa dawa ya kuua wadudu waharibifu wa mazao.

Unga wa mbegu za mwarobaini huchanganywa na maji na kukorogwa vizuri. Mchanganyiko huu uachwe kwa muda wa saa 5-6 au usiku mzima ili uwe mkali zaidi. Robo kipande cha sabuni kilainishwe na kiongezwe kwenye mchanganyiko huu kabla ya kunyunyizia. Hii husaidia dawa ishike vizuri kwenye majani. Ni muhimu kuhakikisha unakoroga vyema wakati unapoweka unga wa mbegu za mwarobaini ndani ya maji.

Changanya kilo moja ya mwarobaini kwa debe moja la maji au gramu 50 za mbegu zinahitajika kuchanganywa na lita moja ya maji. Kama hakuna mizani inawezekana kutumia vifaa vya kupimia ujazo kama makopo, madebe ilimradi ujazo unaohusika ujulikane.

Endapo hakuna mbengu, majani ya mwarobaini yanaweza pia kutumika. Kiasi cha gramu 40 za majani zinahitajika kuchanganya na lita moja ya maji. Kiasi hiki kinalingana kwa kukadiria na kiganja kimoja kilichojaa cha majani. Changanya kiasi sahihi cha maji na uache mchanganyiko huu kwa muda wa saa 12.

Kabla ya kunyunyiza dawa hii kwenye mmea, chuja mchanganyiko huu na ongeza sabuni kiasi. Matumizi ya mchanganyiko huu wa majani ni sawa na ule wa mbegu za mwarobaini.

Kunyunyiza dawa ya mwarobaini

Kuna namna mbili za kunyunyiza dawa ya mwarobaini. Kwanza ni kwa kutumia bomba la kunyunyizia dawa shambani: Chuja dawa kuondoa chembechembe kwenye mchanganyiko ili zisizibe mrija wa bomba.

Chuja mchanganyiko kwa kutumia chombo kisafi au chekeche lenye tundu dogo, au kwa kutumia mifagio ya majani au mabaki ya miti au kitu kingine kinachofanana. Tumbukiza ufagio ndani ya mchanganyiko wa dawa, halafu kung’uta chini ya mmea mara kadhaa mpaka majani yalowe.

Muda unaohitajika kunyunyiza dawa hii

Sumu iliyopo ndani ya dawa ya mwarobaini inafanya kazi kwa siku 3 hadi 6, halafu taratibu hupungua nguvu. Muda wa kurudia kunyunyizia dawa unategemea aina ya mmea unaonyunyiziwa na wadudu wanaohusika.

 

Mimea inahitaji kufuatiliwa kwa uangalifu baada ya kunyunyiziwa dawa ili kuthibitisha ufanyaji kazi ya dawa. Ikiwa wadudu ni wengi dawa ya kuulia wadudu inyunyizwe kila baada ya siku tano hadi saba.

Kama hakuna wadudu wengi nyunyizia mimea iliyoshambuliwa na wadudu tu. Ukiongeza kijiko cha chai cha mafuta yatokanayo na mboga mboga, utaongeza ubora wa dawa.

Matumizi mengine ya mwarobaini

Majaribio ya kuhakiki dawa hii kuwa inafanya kazi ipasavyo yamefanywa na mwandishi wa makala hii kwa takriban miaka minne, yaani kuanzia mwaka 2010 mpaka sasa. Utafiti huo umefanyiwa majaribio katika Kijiji cha Kikono, Kata ya Buyango mkoani Kagera.

Imegundulika kuwa unga wa mbegu za mwarobaini unafaa kuwa dawa ya kuulia wadudu wanaoshambulia mazao mashambani. Dawa hii ya mwarobaini huzuia bunguo katika mashina machanga ya mahindi au mtama kabla hayajachanua. Unaweza kuchanganya sehemu moja ya unga wa mbegu za mwarobaini na sehemu moja ya unga wa mbao au udongo mkavu.

Weka mchanganyiko huu katika shingo ya shina la mmea unaohusika. Kilo moja ya unga wa mwarobaini inatosha kwa mimea 1,500 hadi 2,000. Maji ya mvua huyeyusha dawa ya mwarobaini inayojikusanya ndani ya shimo la mmea na hutiririka kwenye sehemu nyingine za mmea.

Mwarobaini ulio tayari kunyunyizwa

Kwa kutegemea mvua, dawa ya mwarobaini inaweza kunyunyizwa ndani ya shingo la mmea. Rudia kuweka dawa hii baada ya siku 8 hadi 10 katika kipindi chote ambacho bunguo ni tishio. Inatakiwa kurudiwa mara tatu ili kukinga zao na bunguo. Inashauriwa kutumia dawa hii ya mwarobaini kwa mimea michanga kabla ya kuchanua maua na si mimea mikubwa.

Mmea huu ni moja ya tiba nafuu na salama ambazo wakulima wadogowadogo vijijini wanaweza kumudu, ukizingatia kwamba bei ya dawa za viwandani kwa sasa ziko juu na nyingine zimeonekana kuwa na athari kubwa kwa afya ya binidamu na mazingira yake.

Hivyo kwa mtazamo wetu, tunaomba utafiti wa kina ufanyike kuona namna gani mmea huu unaweza kutumika kwa njia bora zaidi katika kuboresha kilimo chetu kwa manufaa ya jamii yetu.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu: 0783 040 581

By Jamhuri