Mwasisi wa TANU: Rais ni Dk. Slaa

IMG_9630

Mwasisi wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), Lameck Bogohe (93), amesema mtu pekee anayestahili kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa.
Bogohe, ambaye ni mmoja kati ya waasisi wawili walio hai kati ya waasisi 17 wa TANU, ni mwanachama wa United Democratic Party (UDP) inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo. Mwasisi mwingine wa TANU aliye hai ni Constantine Milinga.
Bogohe anasema haoni kama kuna mwanasiasa zaidi ya Dk. Slaa anayestahili kwa sifa kushika wadhifa wa urais na kuzimudu changamoto nyingi zinazolikabili Taifa kwa sasa.
Katika mahojiano maalum na JAMHURI yaliyofanyika nyumbani kwa mmoja wa watoto wake, eneo la Kisesa, Mwanza, Bogohe anasema: “Dk. Slaa anafaaa sana. Mimi ni UDP, lakini naamini huyu anafaa kabisa kuwa rais wetu. Ukiniuliza kuhusu Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), nitakuambia huyo hapana.”
Anaongeza: “Kwa upinzani ninaye huyo mmoja tu, kwa CCM ninao watano. Lakini hao watano mmoja wao wakimpitisha, aisaidie tu CCM kupata maksi ya kuweko kwamba chama kiko hai; lakini watashindwa. CCM ni Dk. John Magufuli, Samuel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe, Profesa Mark Mwandosya; nilimwongeza Waziri Mkuu (Mizengo Pinda), yeye anaweza sana, lakini nimekwisha kumgundua ana msalaba moyoni mwake mbaya sana. Anashindwa kuelewa hili ni la Serikali, na hili ni la dini. Amelichanganya Bunge kufikia sasa mpaka wakamlaumu na yeye. Huyo nimemwondoa. Wamebaki wanne. Hili la dini, Waziri Mkuu ni mpole sana, ana huruma kama anawahubiria Wakristo.
“Sasa hao wanne mmojawapo wakimchagua atawaletea sifa CCM ya kubaki kwenye ubao unaosomeka hivi: ‘Kilishindwa lakini msindikizaji wake ni mzuri, amekiletea maksi haya’.
Anamzungumzia Edward Lowassa kwa kusema ana nafasi ndogo ya kuiwakilisha CCM kutokana na hatua yake ya kujiuzulu uwaziri mkuu.
Msimamo wake kwa upinzani ni huu: “Kwa upinzani ni Slaa. Dk. Slaa anafaa sana. Kama tungekuwa tunaelewa, tungempa kura zetu. Samahani nimekampeni kabla ya kampeni, lakini mimi nadokeza tu maana mimi tena siyo wa CCM, mimi ni wa chama changu cha UDP, na ninapendekeza hayo maana wakiweka Dk. Slaa, CCM wataichimbia shimo la miaka 100 bila kushinda.”
Kuhusu wagombea wengine, anasema: “Mbowe hapana. Ni Dk. Slaa tu. Wapo wengi, watakapochukua fomu tutawaelewa. Kama wakichukua nitakuambia. Stephen Wasira hana sifa ya urais, yeye anatanguliza mbele mno mambo ya kujiona, kujigamba. Huo siyo utaratibu wa utawala.
“Bernard Membe sijamjua tofauti na jina maana wale ni wageni katika siasa. Kuna wengine wakiwa wabunge nao wanataka urais. Unataka urais, umefanya nini hapa wewe. Januari Makamba ni mtoto mdogo hana pointi yoyote ya urais na ubunge amepita tu kwa bahati ya huko kwao. Nyalandu, wote hao futa kwangu. Hana sifa ya urais. Haya ni maoni yangu, nisichanganywe kuwa nawasemea wengine.”
Mwasisi huyo kwenye orodha yake hana pendekezo la rais mwanamke.
“Kuwa na rais mwanamke hapana. Mwanamke wakati huu tunaye hapa Spika (Anne Makinda), lakini ameyumbishwa. Kwa urais sasa ndio kabisaa! Ebu (wanawake) wasubiri kidogo, wasiwe na matangazo kuwa mwanamke naye apate hili. Tujue utawala ni kitu kingine cha hekima. Siwakatalii, lakini wakienda kwenye platform (jukwaani) tutawapata. Hao wanaosemewa wakiwa rais watafanya nini?”
Mzee Bogohe anaunga mkono Jaji Augustino Ramadhani, kuwania urais, lakini anataoa angalizo. “ Huyo atafaa, lakini kisheria. Kiutawala hafai. Kisheria anafaa. Lakini urais anaweza kufaa Zanzibar, yeye kuitawala Bara ionekane kama ina rais ni shida.”
Miongoni mwa mambo anayopendekeza yashughulikiwe na rais ajaye ni migogoro ya  ardhi hasa mivutano ya wakulima na wafugaji.
“Nchi hii imepungukiwa mambo mengi sana. Kwanza kilimo, tangu Ujamaa (siasa ya Ujamaa na Kujitegemea) hatuna mabwana wala mabibi shamba; lakini ofisini wanakwenda kupata mishahara.
“Mkulima hajaonana na bwana shamba tangu Ujamaa hadi leo. Mashamba mengi yako vijijini, lakini mabwana shamba wengi wako mijini. Wanapiga kiwi (rangi) viatu. Bwana shamba alikuwa na buti na kofia, ananyeshewa mvua kule mashambani, anakwenda mashambani moja kwa moja kuonana na wakulima anawashauri zao hili linataka hivi. Ndio walikuwa mabwana shamba.
“Leo tuna mabwana shamba wa bajeti ya Wizara ya Kilimo. Wanalipwa mishahara mingapi hawa, wale wa ufugaji wanalipwa kiasi gani. Tangu Ujamaa unaona kuna raia wafugaji wana ng’ombe walionawiri? Ng’ombe ni wa zamani, mifupa nje tu. Dawa zipo, sindano zipo lakini nani anawashughulikia wakulima na wafugaji maskini? Dawa zinatolewa, lakini wafugaji hawapati. Serikali imekuwa yao.”
Kutokana na changamoto nyingi zinazolikabili Taifa, Mzee Bogohe anashauri rais na waziri mkuu ajaye wafanye haya: “Hawa wawili tunaowaweka ngazi za juu kutuongoza waache upuuzi. Mwaka huu ukitaka urais, ufikirie hata siku saba…hujaigusa fomu…nataka urais, niwe rais nitafanya nini?
Wewe mwenyewe ujishauri halafu ndio ukachukue fomu.
“Na sisi watawaliwa tuache ujinga wa kunyamazia haki zetu, tukikosewa tupige kelele. Ninyi waandishi wa habari ndio mtakaotusaidia sana. Siku hizi watu wanaogopa kufanya mabaya wasionwe na waandishi wa habari. Sasa tumejifunza dhambi zote zimekuwa za Tanzania. Nchi nyingine hazina tatizo kama Tanzania, tuyaache basi, tupige hatua.”
Mzee Bogohe anawashauri Watanzania anaowaita wenye ‘mapenzi mema’, kujiengua katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili washiriki kuleta mageuzi ya kweli.
“Hao wanaong’ang’ania CCM wanafanya hivyo kwa sababu ya fedha tu. Wanadhani wakitoka CCM hawatapata fedha. Si kweli, mimi nilikuwa TANU. Nimeshiriki kuiasisi nchi hii lakini nilipoona siwezi kuendelea kuwa kwenye chama hicho nilitoka. Sijawahi kuwa mwana CCM, lakini uzalendo wangu kwa nchi yangu si wa kutiliwa shaka.”
Anaushauri Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuendelea kuwa wamoja ili wasaidie kuiondoa CCM madarakani.
“Ukawa wakitengana watakuwa wametenda dhambi kubwa sana. Wasithubutu kufanya kosa hilo,” anasema.
Ingawa chama chake cha UDP si miongoni mwa vinavyounda umoja wa Ukawa, Mzee Bogohe, anasema maudhui ya umoja huo hayana tofauti na yake ya UDP.
Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
Bogohe anasema alijiengua TANU baada ya kuwekwa kizuizini mara mbili. Tukio la kwanza ni la yeye kuhusishwa na hujuma dhidi ya chama hicho na viongozi wake wakuu, na pili ni uamuzi wake wa kupinga siasa ya Ujamaa ambayo anasema alimweleza Mwalimu Julius Nyerere kwamba ilikuwa haifai.
Pamoja na tofauti zote, Bogohe anasema Tanzania haijapata kiongozi makini na mwenye maono kama Mwalimu Nyerere, na kwamba ndio maana Mwalimu alipofariki dunia mwaka 1999 alilia kwa uchungu kwa kumkosa rafiki na mshika wake mkuu katika siasa.
Bogohe alizaliwa Mei 4, mwaka 1922; ilhali Mwalimu Nyerere akiwa amezaliwa Aprili 13, 1922.
Mfululizo wa makala zinazotokana na MAHOJIANO MAALUM na Mzee Bogohe zitachapisha katika matoleo yajayo ya Gazeti la JAMHURI.