Mwekezaji ahusishwa kifo Katibu wa Chadema

Watu watatu akiwamo Polisi Jamii wa Kijiji cha Ming’enyi, Kata ya Gehandu, Hanang mkoani Manyara, wanadaiwa kumuua Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tawi la Kijiji, Andu Kero.

Wanatuhumiwa kumuua kwa kumpiga wakati wakitekeleza agizo la Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho la kumkamata, kutokana na kudaiwa kuchochea mgogoro wa ardhi.

Kero alikuwa akituhumiwa kuchochea mgogoro huo kati ya kikundi cha wakulima wanaodaiwa kuvamia na kulima katika eneo la ardhi ya mwekezaji wa Kampuni ya Ngano Limited kutoka nchini Kenya.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ming’enyi, Gedasho Nesi, anadai kwamba Kero ni miongoni mwa wakulima wanaodaiwa kulipiga kwa mawe trekta na kuvunja vioo wakati likiwa linang’oa mahindi ya wakulima hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Christopher Fuime, amethibitisha kuuawa kwa Kero, na kwamba aliuawa kwa kupigwa na watuhumiwa hao katika eneo la Kibaoni saa 3:06 usiku.

Polisi Jamii anayetuhumiwa kushiriki mauaji hayo ametajwa kwa jina moja la Simon, anayedaiwa kutumwa kumkamata Kero.

“Yametokea mauaji huko Kibaoni ya mkulima  mmoja wa Kijiji cha Ming’enyi na tunamshikilia askari mgambo mmoja, huku tukiendelea kuwatafuta watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo. Wametoroka na tunaendelea kuwatafuta huku upelelezi ukiendelea,” amethibitisha Fuime.

Awali, katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Christina Solomon Mndeme, alikiri kutokea kwa mauaji hayo na kukiri kuwa chanzo cha mgogoro huo pia kimegubikwa na mazingira ya kuwapo kwa siasa na ukabila.

Amesema Kamati inaendelea na uchunguzi zadi wa matukio hayo yaliyoanza kuhatarisha usalama.

“Najua upo mgogoro, lakini kwa sasa tusubiri uchunguzi ufanyike, siwezi kulizungumzia hilo, na hao viongozi wanaotajwatajwa tulishawaita na kuwahoji, majibu yatatolewa na Mkuu wa Wilaya anayekuja, kwa sasa mimi naondoka kuelekea katika kituo kingine cha kazi cha Wilaya ya Ulanga,” amesema.

Uchunguzi wa tukio hilo umeelezwa na baadhi ya wananchi waliokataa kutaja majina yao kuwa siku ya tukio, Kero alifikwa mauti wakati akimrejesha Mwandishi wa Habari wa ITV/Radio One mkoani Manyara, Charles Masayanyika, kutoka eneo lenye mgogoro kwenda mjini Katesh ili aweze kufika Babati baada ya pikipiki waliyokuwa wakiitumia kupata pancha.

“Ndugu yetu ameuawa na watu hao waliokuwa wakitekeleza agizo la Ofisa Mtendaji wa Kijiji, inauma sana lakini tunamwachia Mungu na mkono wa sheria. Suala hapa ni mgogoro ambao chanzo chake kinatokana na wakulima hao kujiunga na Chadema na hofu ya kushindwa Uchaguzi Mkuu,” amesema mkulima mmoja na kuongeza:

“Tunashangaa Ofisi ya Serikali ya Kijiji kuendesha ukamataji wa usiku kinyume cha sheria. Huyu mtu hakuua, lakini ni jinsi gani ofisi ya kijiji na kata zilivyokuwa zimeandaa mtego huo wakati wa usiku.”

Masayanyika ambaye alinusurika huku kukiwapo taarifa kwamba walipanga wamkamate kutokana na baadhi ya viongozi wa kata na kijiji hicho kuchukia hatua ya ufuatiliaji wa mgogoro huo.

Mwandishi huyo amezungumza na JAMHURI na kukiri kutokea kwa mauaji ya mkulima huyo aliyekuwa akimsafirisha kwa usafiri wa pikipiki kabla ya kufika mjini Katesh.

“Ni kweli hayo yanayosemwa, lakini sipendi kulizungumzia hilo sana kwani baada ya polisi kunitaka kutoa maelezo, nashangaa nimetumiwa ujumbe kupitia simu wa kunitisha kwa kile kinachodaiwa nimesababisha madhara na nimekosa maadili ya kazi yangu huku wakidai wakinikamata watanichinja,” anasema.

Ameongeza: “Kinachonisaidia kwa sasa nimepata tumaini na nguvu baada ya ndugu wa marehemu kunielewa na kuridhika, lakini pia wakieleza kuwa uongozi wa kijiji hicho na kata ndiyo chanzo cha kifo cha ndugu yao.”

Baadhi ya wakulima hao Desemba 16, mwaka jana walichomewa maboma yao na kupata hasara ya mazao katika eneo hilo wanalodai kuwa wamekuwa wakilima kwa miaka 17.

Wanasema kijiji hicho kimekuwa kikitambua michango yao ya maendeleo na kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kupitia kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura.

Wanadai kwamba wafugaji zaidi ya 400 walivamia maeneo ya makazi yao na kuyachoma. Februari 16 mwaka huu mwekezaji wa kampuni ya Ngano Limited anadaiwa alinyunyiza sumu ya kuua magugu na baada ya mazao hayo kunyauka aliingiza trekta na kuharibu mahindi ya wakulima kwenye eneo hilo linalodaiwa kuvamiwa.

Wanasema wanashangazwa na mwekezaji kuleta mgogoro huo hasa katika Kitongoji cha Gichela ambacho wananchi wake walihamia Chadema baada ya unyanyasaji wa viongozi wa kisiasa, lakini wananchi wa vitongoji wanapoishi viongozi hao na kulima hawasumbuliwi.

Wanasema kitendo hicho kinaonesha kuwa ameshindwa kulima shamba hilo lenye ukubwa wa hekta zaidi ya 6,300 na badala yake anadaiwa kutumiwa na viongozi hao wa kata ambao wanalima maeneo makubwa bila kunyanyaswa.

Naye Diwani wa Kata ya Basutu, Sarah Haanly, amesema mauaji hayo yana mkono wa viongozi wa Serikali ambao wananufaika na uporaji wa maeneo hayo ya wananchi kupitia mgongo wa mwekezaji huyo.

Amewataja wahusika wakubwa wa mgogoro huo na mauaji ya Katibu wa Chadema katika kijiji hicho ni Mbunge wa Jimbo la Hanang, Dk Mary Nagu, na Mwenyekiti wa Halmashauri, Anjo Mang’ola.

Kuhusika kwa viongozi hao kunatokana na kujikita kumsaidia mwekezaji kupora eneo hilo la kijiji ambacho kimekaliwa na wananchi hao kwa miaka 17 sasa na mwekezaji kawakuta katika eneo lao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ndiye aliyetoa amri ya kumkamata katibu wa Chadema aliyeuliwa chini ya usimamizi wa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Gedasho Nesi, na kwamba amemegewa hekari 60 za mashamba na mwekezaji huyo mashariki mwa kijiji hicho.

Diwani huyo anasema kuhusika kwa Dk. Nagu katika mgogoro huo ni kushindwa kwake kuupatia ufumbuzi na kuwageuka wananchi anaoelewa kwamba tangu mwaka 1998 wanaishi katika maeneo hayo aliyopewa mwekezaji ambaye anawanyanyasa wananchi.

“Miezi miwili iliyopita, mwekezaji amechoma nyumba 18 na mazao ya wananchi, lakini jambo la kushangaza, Dk. Nagu anawaeleza wananchi wake kuwa hatatoa msaada wowote ule kwao, kwani ni wavamizi,” amesema.

Amesema kitendo cha mwekezaji kuteketeza mali za wananchi na viongozi hao kutetea upuuzi huo kimewadhalilisha sana wananchi wa Tanzania ambao wamekuwa wakinyanyaswa na wageni ndani ya nchi yao kwa kivuli cha uwekezaji.

Meneja wa Shamba la Gidagamoud kupitia Kampuni ya Ngano Limited iliyo chini ya kampuni mama ya Raul Group iliyopo nchini India aliyefahamika kwa jina moja la Karai, amesema amenyunyiza sumu hiyo na kuyalima mahindi hayo baada ya kunyauka kwa kuwa eneo hilo ni mali yake.

Anasema ameshindwa kuyalima mazao yote baada ya wakulima hao kuvamia shamba hilo na kuvunja vioo vya trekta lake; tuhuma ambazo baadhi ya wafugaji waliokuwa eneo hilo wanazipinga.

Mwekezaji huyo pia ameingia kwenye mgogoro kati yake na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo baada ya kuamua kuweka mipaka ya shamba inayoingia kwenye makazi ya wananchi katika Tarafa ya Basout.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ming’enyi, Mbisha Mchaloga, alipohojiwa na JAMHURI kuhusu mauaji hayo, amesema kwamba yeye ameyasikia tu akiwa katika Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani akichunga mifugo yake.

“Tangu mauaji hayo yalipotokea Februari 16, mwaka huu, nimesikia wahusika wamekamatwa lakini kinachoendelea hadi sasa mimi sielewi,” amesema Mchaloga.