Ndoto ya Tanzania ya viwanda inaonekana kuanza kuyeyuka kutokana na mwekezaji kusota kwa miaka kumi akihangaika kupata vibali ili awekeze katika ujenzi wa kiwanda cha sukari, Bagamoyo, mkoani Pwani.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kampuni ya EcoEnergy ni kutoka nchini Sweden. Mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 550, ambao ni mkopo toka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Kwa muda mrefu kumekuwa na majadiliano ya kina kati ya Serikali na EcoEnergy tangu mwaka 2006 ambapo mwaka 2013 Serikali iliikabidhi kampuni hiyo hatimiliki ya eneo la mradi kwa miaka 99, hati za mazingira pamoja na kibali cha kuvuna maji kutoka mto Wami ili kuwezesha mradi kuanza.

Baada ya yote hayo kufanyika, Serikali imeshindwa kutoa kibali kwa EcoEnergy, hali inayoifanya kampuni hiyo kushindwa kuanza mradi huo mkubwa wa uzalishaji sukari.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI imeziona  endapo mradi huo ungeanza, Serikali ingekabidhiwa asilimia 10 ya hisa ambazo, hata hivyo, zingepanda hadi kufikia asilimia 25 ndani ya kipindi cha miaka 18 ya uzalishaji.

Kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi wa hesabu uliofanywa na kampuni ya Ernst and Young, hadi kufikia Juni, mwaka jana, EcoEnergy walishatumia takribani shilingi bilioni 100 katika kugharamia upembuzi yakinifu, kuendesha shamba la mfano la kilimo cha mbegu za miwa, shughuli za jamii inayozunguka mradi pamoja na kulipa fidia na kuandaa ramani ya kiwanda.

Mwenyekiti Mtendaji wa EcoEnergy, Per Carsdedit, anasema kampuni hiyo inataraji kuzalisha tani 150,000 za sukari kwa mwaka, lita za ujazo milioni 14 ethanol, ambayo itatumika kuzalisha umeme Megawatt 32.

Anasema mradi huo utatengeneza ajira za moja kwa moja zipatazo 2,300 kuajiri wakulima wa nje kwa kaya zipatazo 2,000 na kwamba watu zaidi ya 100,000 wangenufaika na mradi huo.

“Kutokana na mazingira mazuri ya Tanzania, tulijipanga kufanya uwekezaji mkubwa wa kisasa, wenye kutumia teknolojia ya pekee katika ukanda huu wa Afrika. Imekuwa bahati mbaya tunashindwa kufahamu Serikali imekwama wapi kutoa uamuzii ili tuanze kazi,” anasema Carsdedit.

Carsdedit anasema kampuni yake ina uwezo wa kupunguza kiwango cha sukari na mafuta ghafi vinayoagizwa kutoka nje ya nchi, ili kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazopotea.

“Nchi kama Uganda, Zambia, Malawi, Afrika Kusini zinazalisha sukari ya kutosha na kuuza ziada nje. Inasikitisha kuona Tanzania inaagiza nusu ya mahitaji yake ya sukari toka nje. 

“Kuna haja ya kutafakari juu ya jambo hili kwa kina kwa sababu kadri idadi ya watu inavyoongezeka, mahitaji ya sukari yanapanda, hivyo kusababisha uagizaji wa sukari kutoka nje…suluhisho ni kuwa na uwekezaji mkubwa wa sekta ya sukari ndani ya nchi,” anasema Carsdedit.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI limeziona, Serikali ilitiliana saini makubaliano ya kuanza mradi na EcoEnergy mwaka 2006, kampuni hiyo ilipewa hati ya umiliki ardhi mwaka 2013 yenye namba 123097.

Mwezi Agosti, 2012 wawekezaji hao walipata cheti cha msamaha wa kodi kutoka Kituo cha Uwekezaji (TIC) chenye namba 010429, huku mwaka 2011 Bodi ya Sukari iliwapatia EcoEnergy cheti cha uzalishaji sukari chenye namba BE/SMR/A.05 pamoja na leseni ya kuzalisha sukari namba BE/SML/A.05.001.

Ripoti ya utunzaji wa mazingira yenye nambari EC/EIS/089 ilitolewa mwaka 2009; Mamlaka ya Maji Wami walitoa kibali cha kuvuna maji chenye namba WA 0169 mwaka 2013.

August 2013, Mamlaka ya Bonde la Mto Wami na Ruvu zilitoa kibali cha matumizi ya maji ya mto Wami, pamoja na kuelekeza kiwango cha maji yanayoweza kuvunwa na mradi bila kuathiri mahitaji ya watumiaji wengine ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Akizungumza na JAMHURI, Mbunge wa Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa, anasema mradi huo ni mzuri kwa maendeleo ya Bagamoyo na Taifa kwa ujumla. 

Dk. Kawambwa anasema amemwalika Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na kwamba atatembelea mradi huo pamoja na kuzungumza na wananachi Jumanne (leo).

“Tunatarajia ugeni wa Mheshimiwa Waziri Mkuu kutembelea maeneo ya mradi ambapo atazungumza na wanachi,” Dk. Kawambwa anasema.

3613 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!