Mwanachama mkongwe wa klabu ya Yanga, Ibrahim Akilimali, amesema kuwa ataendelea kupinga suala la ukodishwaji wa klabu hiyo hadi atakapoingia kaburini.

Mzee Akilimali amedai kuwa amekuwa na bahati mbaya kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa Klabu ya Yanga kutokana na kupinga suala la Yanga kumilikiwa na mtu mmoja .

Nimekuwa na bahati mbaya kwa baadhi ya wanachama na viongozi, ni kutokana na kukataa katu suala la Yanga kumilikishwa mtu mmoja hilo haliwezekani na nitapinga hadi naingia kaburini. Nipo tayari uanzishwe mfumo wa kampuni kama inaavyotajwa katika katiba ya Yanga ibara ya 56 ambayo inasema Yanga itaanzisha kampuni ya umma ambapo wanachama wanamiliki hisa asilimia 51 na wanahisa asilimia 41. Lakini kwa kuwa nilikataa ndiyo naambiwa napinga mabadiliko, Yanga haikodishwi kama masufuria na kwa bahati nzuri serikali ikatusikiliza sisi watu wachache tuliopinga ukodishwaji ndipo wanaposema kuwa mimi napinga maendeleo.“amesema Mzee Akilimali jana kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.

Hata hivyo, Mzee Akilimali amesema kuwa anaunga mkono juhudi za maendeleo ndani ya Yanga lakini sio kwa kuikodisha kwa mtu mmoja.

Mimi nahitaji maendeleo ya Yanga hadi kiama lakini utaratibu ufuatwe sio kumpa mtu mmoja, kwa kuwa viongozi wangu walitaka kukodisha na mimi pamoja na serikali kupinga, ndiyo wameniambia mimi napinga maendeleo, jambo hilo si sawa,” amesema Mzee Akilimali.

Hivi karibuni Klabu ya Yanga ilitangaza kuanza mchakato wa mabadiliko kama ilivyo kwa watani wao Simba ambao wamemkabidhi timu Mohamed Dewji ‘Mo’ kwa ajili ya kuingia katika mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu kwa njia ya hisa.

Mzee Akilimali amekuwa akitajwa mara kwa mara kuwa miongoni mwa wanachama ambao wanapinga mabadiliko ndani ya klabu hiyo jambo ambalo limekuwa likiwachukiza baadhi ya wanachama.

1510 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!