Mzimu wa Escrow waigawa Serikali

Mzimu wa malipo ya zaidi ya Sh bilioni 300 kutoka kwenye akaunti ya Escrow, zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) umeendelea kuigawa Serikali, baada ya baadhi ya maafisa wazito kutaka wamshauri Rais John Pombe Magufuli awaagize waliozichukua fedha hizo wazilipe, huku wengine wakisema ni zigo la Serikali.

Fedha hizo zilizotolewa mwaka 2013, zimeendelea kuwa mzimu kwani kwa sasa baada ya hukumu ya Mahakama inayoshughulika na migogoro ya uwezekaji – ICSID – yenye makao yake Washington DC, Marekani, inaonekana kuwa kaa la moto kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

ICSID imeitaka Tanesco kuilipa kampuni ya Standard Chartered ya Hong Kong kiasi cha dola milioni 148 (karibu Sh bilioni 320). Katika shauri hilo, Tanesco walikuwa wanawakilishwa na kampuni za mawakili za R.K. Rweyongeza & Co. Advocates na Crax Law Partners ya Tanzania, na ile ya Zurich, Kellerhals Carrard.

Afisa Mwandamizi wa Serikali ameiambia JAMHURI; “Kwa sasa tumewapa hoja wadeni wote dhidi ya Tanesco. Mara zote tulikuwa tunasema ndani ya akaunti ya Escrow kuna fedha zetu, sasa tumewapa PAP zote hoja kwamba kuna hela zetu imekufa kabisaaaa… wanatuhoji kuwa sasa tulikuwa tunakataa nini?

“Standard Chartered wanasema wao ni legal assignee wa IPTL. Sasa wamefungua kesi huko London wanapinga PAP kulipwa fedha hizo wakati kuna kesi ya msingi inayoendelea pale London wanadai zaidi ya dola bilioni 1 (karibu Sh trilioni 2.3). Kesi ni nyingi mno. Kuna kesi Standard Chartered wanapinga uamuzi wa Jaji (John) Utamwa katika Mahakama yetu Kuu …

“Polisi wanachunguza suala hili, PCCB wanachunguza, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inachunguza, hawa wanayo madai katika mikataba kadhaa ikiwamo Contract Guarantee, Implementation Contract na Power Purchasing Contract wanadai Serikali imetaifisha mitambo yao kwa kumpatia PAP zile fedha. Kimsingi ni shida tupu kwa sasa serikalini kuna vikao visivyoisha,” kilisema chanzo chetu.

Afisa mwingine aliiambia JAMHURI kuwa wapo wanaoona ikiwa Rais Magufuli atashikilia msimamo kuwa aliyechukua fedha hizo alipe, basi inaweza kujikuta anaingia katika ugomvi na Serikali iliyotangulia ya Rais Jakaya Kikwete kwani mishale mingi inaonekana kuelekea kwake.

Hadi sasa Serikali haijafikia uamuzi, ila JAMHURI inaweza kuthibitisha kuwa PAP waliingia mkataba na Serikali kuwa watalipa madai yoyote yatakayojitokeza baada ya kuwa wamechukua fedha hizo, basi mwisho wa siku msimamo wa Serikali utaendelea kubaki kuwa aliyelipwa fedha hizo ndiye aliyetakiwa kurudisha.

JAMHURI ilipowasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema kwa sasa hana la kusema kwani suala hilo linafanyiwa kazi katika ngazi mbalimbali.

Wiki iliyopita, Kaimu Mwenyekiti ambaye pia ni Mwanasheria wa Kampuni  wa IPTL, Joseph Makandege, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kampuni hiyo, haiyatambui madai ya Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) kama mdai na wala hawana haki kwa mujibu wa sheria.

Makandege alinukuliwa akisema, IPTL inaungana na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kukata rufaa katika Mahakama ya ICSID kwani hukumu iliyotolewa ina upungufu mwingi wa kisheria.

Licha ya uamuzi huo, Makandege anasema IPTL haikulipwa kwa kutumia viwango vya zamani bali walilipwa kutokana na umeme waliouuza kwa Tanesco na si vinginevyo.

“Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong hawastahili kulipwa fedha na Watanzania kwani hawastahili kwa mujibu wa sheria nasi kama IPTL/PAP hatuwatambui na hawana haki ya kutuzungumzia. Na ndiyo maana wameamua kukimbia Mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje, hawa wana msukumo wa mabeberu wenye nia ovu.

“Kwa uamuzi huu wenye utata uliotolewa na ICSID, ni wazi Standard Chartered walikuwa na nia ovu, ninasema hivyo kwa sababu tangu Septemba 5, 2013 suala hili liliamuriwa vizuri chini ya Jaji Utamwa (John) na IPTL ikashinda kesi na kutwaa uongozi.

“Lakini pia dai letu jingine tuliomba Mahakama Kuu itupe nafuu ya Standard kutulipa gharama kama fidia ya dola za Marekani bilioni 3.240, ambapo hata tuzo waliyopewa na ICSID eti wanataka walipwe dola za Marekani milioni 148 na kama wakitulipa fedha zetu, hata madai yao yaingia humo na bado kuna fedha nyingine inabidi watupatie sisi,” alinukuliwa Makandege.

Anasema licha ya Mahakama kutoa uamuzi, wataendelea kusimamia uamuzi huo wa kutomtambua mtu anayeitwa Martha Renju wala, Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong.

“Sisi msimamo wetu kama IPTL/PAP tunasema hadharani kwamba hatuitambua Benki ya Standard Chartered ambao hawa kila wakati wamekuwa wakikimbia Mahakama zetu za ndani na kukimbilia nje na hata hukumu hii ya tuzo ina viashiria vya mabeberu.

“Tuzo husika waliyopewa ni dhahiri Standard Chartered ni batili kwa mujibu wa sheria. Wao ni kina nani hadi wakafungue kesi kwa niaba yetu. Hii ni kesi ya ngedere imepelekwa kwa nyani,” anasema Makandege.

Uamuzi wa ICSID

Hukumu iliyotolewa na ICSID inasema Mahakama hiyo inayo mamlaka ya kupitia upya uamuzi uliotolewa mwezi Februari 2014, kwamba Tanesco inaweza isilipe deni inalodaiwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong. Mahakama hiyo inasema deni inalodaiwa Tanesco, inaweza kutoa amri ya namna malipo yanavyoweza kufanyika.

Hukumu hiyo ambayo JAMHURI imepata nakala yake, inasema Mahakama imeamua kwamba kukokotolewa kwa bei kutatokana na kiwango cha faida (IRR) ya asilimia 22.31 kutokana na mkopo wa mbia.

“Kwa hiyo, pesa anayodaiwa Tanesco chini ya mkataba wa ununzi wa umeme, mpaka kufikia Septemba mwaka jana, ni dola za Marekani milioni 148.4… Mahakama imeamua kwamba kiwango cha riba kwenye kiwango kinachodaiwa chini ya mkataba wa ununuzi wa umeme lazima usizidi asilimia 4,” inasomeka sehemu ya hukumu hiyo.

Akizungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam, Mwezi Desemba, 2014, Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, alisema; “Tangu Desemba, 2014 nilipoanza kazi baada ya mapumziko ya ugonjwa nilikabidhiwa taarifa mbalimbali kuhusu sakata hili. Tangu wakati huo nimekuwa nazisoma pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali na kuagiza nipatiwe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kutoka kwa wahusika.

“Mwaka 1998 Tanesco walifikisha kwenye Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji, London, malalamiko kwamba gharama za uwekezaji za IPTL ni kubwa mno kuliko kiasi halisi walichowekeza.

“Mwaka 2001, Kituo cha Usuluhisi kilifanya uamuzi wa shauri hilo. Madai ya Tanesco yalikubaliwa kuwa uwekezaji halisi uliofanyika ni dola za Marekani milioni 127 na siyo dola milioni 163.17 walizodai IPTL. Kutokana na kupungua huko kwa gharama za uwekezaji, tozo ya uwekezaji (capacity charges) nayo ilipunguzwa kutoka dola za Marekani milioni 3.6 kwa mwezi mpaka dola za Marekani milioni 2.6 kwa mwezi. Kituo pia kilitoa mwongozo kuhusu ukokotoaji wa tozo hiyo.”

Rais Kikwete aliwaambia wazee wa Dar es Salaam kwamba kwa jumla uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu akaunti ya Escrow na ushauri wa Mwanasheria Mkuu kwa Serikali wa kutekeleza uamuzi huo vimetiliwa shaka.

Akazidi kuwaambia wazee kwamba umeonekana kuwa haukuwa uamuzi sahihi na kwamba umeitia hasara nchi. Isitoshe uamuzi huo umeibua hisia za kuwapo harufu na vitendo vya rushwa. Wapo waliosema si bure iko namna! Wapo waliotaja majina na watu wanaodai wamepata mgawo wa Escrow, tena wengine wamechukua fedha kwa viroba, sandarusi na lumbesa.

“Bahati mbaya sana katika mjadala ilijengeka dhana isiyokuwa sahihi kwamba jambo hili lilianzishwa na maafisa hao wa Serikali kwa nia ya kujinufaisha wao binafsi. Ukweli ni kwamba uamuzi ulifanywa na Mahakama Kuu na kwenye Serikali ilikuwa utekelezaji wa amri hiyo.