Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), imewataka wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuachana na fao la kujitoa na badala yake iwe fao la kukosa ajira.

Mkurugenzi wa Sheria wa SSRA, Onorius Njole, amewaeleza waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kuwa fao la kujitoa kwa mwanachama ni sawa na kujifukuza mwenyewe na kupoteza kiasi kikubwa cha fedha anazostahili kulipwa kwa siku moja.

Njole anasema kwa siku ya kwanza mtu anapojitoa ikiwa anapokea Sh 500,000 hupoteza Sh milioni 1, vile vile anayepokea Sh milioni 1 anapoteza milioni 2 kwa siku moja tu. Hivyo, fao la kujitoa halimpi faida mwanachama wa mfuko wa wowote wa hifadhi ya jamii.

Pamoja na hayo anasema ‘Fao la Kujitoa’ likiondolewa na kuwekwa la ‘upotevu ama ukosefu wa ajira’ linaweza kumsaidia mtu kwa maisha yake ya baadaye pia mwajiri kuendelea kuchangia na kuondoa migogoro ya kazi isiyokuwa na ulazima.

Anasema wengi waliokuwa wanahitaji fao la kujitoa walikuwa watumishi wa umma na awali lilikuwa halina athari kubwa kwao lakini kwa sasa wanaomba kurudishwa katika mfuko wa pensheni kwa kulipwa kila mwezi.

‘‘Hawa hawachangii chochote, hulipwa kutokana na kodi za wananchi wote. Watu wanaumia badala ya kupata fao la kujitoa ambalo halipo.

‘‘Anasema sifa kwa fao la kukosa ajira ni mwanachama wa mfuko kuchangia kwa kipindi cha miezi 18, asiwe ameacha kazi kwa hiari yake na kwamba atapata asilimia 33 ya mshahara wake wa mwisho kwa miezi 18 ambao hakatwi makato yoyote,’’ anasema Njole.

Hata hivyo, anasema asilimia kubwa ya watu wanaojitoa ni wale walioelimika na wanaotazamia ajira nyingine, pia wako baadhi yao walioacha kazi kabla ya kupata ajira mpya ambao watahamishiwa katika uchangiaji wa hiari bila kuathiri mafao yao.

Anasema Serikali imetajwa kuwa ndiyo mkopaji mkubwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii, huku ikifikia ukomo wa kukopa kutokana na madeni yake ya nyuma na sasa kazi yake ni kulipa deni lake kwa mifuko.

Deni la Serikali linahusiana moja kwa moja na uwekezaji na kabla ya mwaka 1999 kulikuwa na mifuko iliyokuwa inawekeza na watumishi waliolipwa kwa makato kama kodi na hilo ndiyo linalodaiwa na wengi wanaolipwa kupitia PSPF kwa watumishi wa Serikali Kuu.

Kwa upande mwingine, anaeleza kuwa mwajiri kumlazimisha mwajiriwa kujiunga na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii anaoutaka yeye ni ukiukaji wa sheria, kila mwanachama anapaswa kuchagua mfuko anaoutaka kwa hiari yake mwenyewe. 

Njole anasema kitendo kinachofanywa na baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii kuwafuata waajiri na kuwataka wawalazimishe watumishi kujiunga na mfuko husika ni kosa la jinai. 

Mkuu wa Mahusiano na Uhamasishaji wa SSRA, Sarah Msika, amewaomba wananchi kujiunga kwa wingi na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kukidhi mahitaji yao pale wanapopata majanga.

Msika anasema idadi ya wananchi waliojiunga na mifuko ya  yote saba ya hifadhi ya jamii nchini ni zaidi ya milioni 2 tu ambayo ni idadi ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya Watanzania wote wanaofikia zaidi ya milioni 47.

Mifuko saba ya hifadhi ya jamii iliyopo nchini kwa sasa ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF), Mfuko wa Pensheni (PPF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Msika anasema SSRA ilianza kazi rasmi mwaka 2010 chini ya Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, sura namba 135 na kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Majukumu 13 ya SSRA ni pamoja na kulinda maslahi ya wananchama wa mfuko, kuhakikisha mifuko inakuwa endelevu, inaendeshwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Majukumu mengine ya Mamlaka hiyo ni kufanya ukaguzi wa mifuko, kusajili mifuko, watunzaji na meneja wa uwekezaji katika sekta ya hifadhi ya jamii, kudhibiti na kusimamia utendaji wa mifuko, kumteua msimamizi wa mfuko pale inapotakiwa kufanya hivyo.

Kuhusu wanachama ambao wanahama kutoka mfuko mmoja hadi mwingine, anasema wanakosa kukidhi masharti yanayotakiwa katika kulipwa pensheni ikiwa ni sharti la kutimiza umri wa miaka 55 na kuchangia kwa kipindi kisichopungua miaka 15.

‘‘Mifuko ya hifadhi ya jamii imeundiwa mwongozo unaofanana hivyo mwanachama hapaswi kuhama kutoka mfuko aliokuwa amejiunga awali na kujiunga na mfuko mwingine baada ya kubadilisha ajira yake isipokuwa kutoa taarifa ya mwajiri wake mpya na mshahara wake,’’ anasema.

Kwa mujibu wa kifungu cha 30 cha sheria namba 8 ya mwaka 2008, mfanyakazi haruhusiwi kujiunga na zaidi ya mfuko mmoja wa lazima (Mandatory Scheme). Hata hivyo anaruhusiwa kujiunga na mifuko ya hiari kwa idadi yoyote kadri apendavyo.

Anasema mifuko ya hiari ni ile iliyoundwa na bodi ya wadhamini kwa kutengeneza kanuni na kusajiliwa na SSRA na mifuko hiyo ni VSRA ya GEPF, DAS ya NSSF, DAS ya PPF, PSS ya PSPF na LAPF. 

Anasema kabla ya miaka mitano ya kustaafu ni lazima mwanachama ahakiki mafao yake kwanza, ikizingatiwa kwamba mifuko hii ni ya watu na inapaswa kufanya kazi katika mazingira ya watu.

Akieleza kuhusu uwekezaji wa mifuko, anasema SSRA imeweka mwongozo wa kusimamia usalama wa fedha za wanachama na kwamba kila shilingi inayowekezwa inazalishwa na ukwasi wa mfuko.

Pia mwongozo wa kusimamia mafao ya wanachama na gharama za uendeshaji wa mfuko ambazo ukomo wake wa juu ni asilimia 10 ya michango. Kwa kipindi cha miaka miwili tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo, mifuko iliyo na gharama ndogo na kubwa ilitakiwa kufikia kiasi hicho, lakini suala hilo linapaswa kwenda taratibu.

Mkurugenzi wa Utafiti, Takwimu na Uendelezaji wa Sera wa SSRA, Ansgar Mushi, anasema mifuko ya hifadhi ya jamii inasimamiwa na Bodi za Mifuko na iwapo taratibu zitakiukwa au kujitokeza kwa wizi wa fedha za wanachama, Mamlaka inawashtaki na kuwafilisi wajumbe wa bodi husika.

Pamoja na kusimamia bodi hizo, anasema Mamlaka inasimamia mikutano ya mwaka ya mifuko hiyo ambayo inatakiwa kuwashirikisha wanachama wote ambao watapewa fursa ya kuuliza maswali na kupewa majibu sahihi kwa lengo la kufahamu hali ya mfuko wao.

‘‘Wafanyakazi waliopo katika sekta ya habari, sheria na uhandisi wengi ndiyo wanaoongoza kwa kutojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Ukomo wa kazi ni kwa mwanadamu ni kifo iwe kwa umri wa ujana, uzee na ulemavu. Na utajiri ni kazi ngumu, kwani unamfanya mtu kuhifadhi akiba bila kuangalia tatizo linalomkabili kwa wakati huo,’’ anasema Mushi.

Ibara ya 11 kifungu cha (1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahusisha huduma za jumla za jamii ambazo ni afya, elimu, chakula na nyinginezo huku Serikali ikiwa na jukumu la kuhakikisha wananchi wake ambao ndiyo walipa kodi wakipata huduma hizo.

Anasema asilimia 20 ya makato huhifadhiwa kama akiba ya baadaye kwa mtu katika mfuko hivyo mifuko inatakiwa kuweka wazi viwango vya mafao kwa wanachama na wajibu wa kulinda thamani ni wanachama wenyewe.

Kikokotoo kipya kilichoboresha mafao kilianza kutumika rasmi Julai 2014, na kanuni zimeanza kutumika kwa wanachama waliostaafu wa mifuko ya NSSF na PPF ambazo haziwagusi wanachama waliokuwapo GEPF, PSPF na LAPF kabla ya Julai 1, 2014.

Anasema kuna mafao ya aina mbili yanayotolewa na mifuko hiyo ya hifadhi ya jamii ambayo ni muda mfupi yakihusisha matibabu, kuumia kazini, elimu na mafao ya uzazi. Fao la pili ni muda mrefu ambalo ni pensheni ya uzeeni na pensheni kwa wategemezi.

Mifuko ya hifadhi ya jamii haipaswi kutoa gawio kwa wanachama wake kama zinavyofanya kampuni za kibiashara kutokana na kufuata mfumo wa kibima.

By Jamhuri