Baada ya maandamano ya kumshinikiza Rais Nicolas Maduro kung’atuka madarakani kukumbwa na vurugu, kiongozi mashuhuri wa upinzani, Juan Guaido, amejitangaza kuwa rais wa mpito.

Guaido amepata uungwaji mkono kutoka mataifa ya Marekani, Canada na majirani wa taifa hilo walio na ushawishi mkubwa katika Kanda ya Amerika Kusini kama vile Brazil, Colombia na Argentina.

Muungano wa Ulaya umetoa wito wa kufanywa upya uchaguzi na kuunga mkono bunge la kitaifa litakaloongozwa na Guaido.

Lakini kuna baadhi ya mataifa yanayomuunga mkono Rais Maduro ikiwemo Urusi na China. Maduro ameilaumu Marekani kwa kujaribu kupindua utawala wake.

Moscow imeonya kuwa hatua ya Guaido moja kwa moja huenda ikasababisha “uvunjaji wa sheria na umwagikaji mkubwa wa damu.” Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imesema: “Tunaonya kuwa hatua hiyo itakuwa na athari mbaya.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Hua Chunying, amesema kuwa China inapinga “kuingilia” mambo ya ndani katika mzozo wa Venezuela. “China inaunga mkono mikakati ya kulinda uhuru wa Venezuela wa kujitawala.

“China itaendelea kushikilia msimamo wake wa kutoingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine,” alisema.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Mamlaka ya Urais wa Uturuki, Ibrahim Kalin, Rais Recep Tayyip Erdogan, amempigia mwenzake, Nicolas Maduro na kumhakikishia kuwa Uturuki itasimama naye: “Ndugu Maduro, simama imara, tuko nawe kwa hilo,” alisema.

By Jamhuri