Nafsi ya binadamu inapenda mambo mazuri na matamu inapojionyesha na kujipambanua mbele ya nafsi nyingine za wanadamu, lakini ina mtihani mkubwa wa kutawaliwa na ushetani katika kufanya mambo mabaya na machungu, hivyo kuondoa heshima na thamani ya nafsi.

Nafsi hupata furaha inapotenda mambo mema, na hupata aibu inapotenda mabaya kinyume cha  imani ya Muumba. Nafsi hupata karaha inapotendewa maovu na nafsi ya binadamu mwingine.

Nafsi zinazotawaliwa na ushetani hazikumbuki imani ya Muumba wao, kwani zinapagawa na mzuka uliolaaniwa na Muumba. Ukienda Asia, Ulaya hata Marekani utazikuta zikirandaranda kwa nia ya kutenda mabaya na machungu, huku zikijifukiza moshi wa manukato kughiribu na kuvuta nafsi fulani fulani.

Hivi leo Bara la Afrika linapata shaka na misukosuko ya vita ya hapa na pale katika nchi zake kutokana na nafsi za baadhi ya Waafrika kutaka mambo mazuri na matamu bila ya kuzingatia na kufuata masharti ya imani iliyoko ya imani ya Muumba. Nafsi za Waafrika hawa zimetawaliwa na ushetani.

Aidha, dunia imeingia katika shaka, mivutano, misukosuko na mapambano ya vita ya maneno au ya silaha kutokana na nafsi kutaka mazuri na matamu kupitia uvunjifu wa imani na kubariki ushetani. Nafsi inapofikia alama hii, ukweli haisikii onyo wala haikubali hadhari. Matokeo ni wanadamu kuyumba na mwishoni kutoweka duniani.

Lakini zipo nafsi zinazopenda mambo mazuri na matamu kwa kuzingatia na kufuata imani ya Muumba katika kufanikisha mema mbele ya nafsi nyingine. Nafsi hizi zinapatikana Afrika, Asia, Ulaya hata Marekani. Zenyewe hazifukizi moshi wa manukato, bali zinajionyesha na kuonwa hadharani.

Nafsi za wanadamu zinazopenda mambo mazuri na matamu, zinazotawaliwa na ushetani kutenda mambo mabaya na machungu, huku yakisema uongo, yakificha mengi mazuri na kupigia la mgambo machache mabaya. Macho hujaa matongotongo na masikio huzibwa na nta.

Zile za wanadamu zinazopenda mambo mazuri na matamu kupitia imani, zinakemea maovu, zinakosoa na zinarekebisha mambo, zinatoa maarifa mbalimbali, zinasifu na kupongeza juhudi ili kupata maendeleo katika jamii ya wanadamu.

Nafsi ya mwanadamu aitwaye Abasi Mzee ( marehemu), yenye imani ya Muumba, enzi ya uhai wake akiwa na Egyptian Musical Club alitunga na kuimba wimbo wenye maneno yafuatayo:

Akufanyiaye ubaya,

bora umnyamazie,

Usichukue hatua,

nafasi yake umwachie,

Kama hujamkosea,

fahamu atajidhuru mwenyewe,

Atakalo kusudia,

Mola si pamoja naye.

Usimfanye lolote,

ingawa una uchungu,

Mikono juu uiweke,

bora umwachie Mungu,

Mwache ende pande zote,

hata juu ya mawingu,

Ubaya una mwisho wake,

mwache ajigawe mafungu,

Atapata ada yake,

zawadi ya ulimwengu.

  

Alopewa amepewa,

huwezi kumnyang’anya,

Yeye ametunukiwa,

kwa usiku na mchana,

Hata ukimchukia,

katu hatarudi nyuma,

Kama yupo wa kuzuia, jua anajidanganya,

Jua utaangamia,

wenda yeye kwako mwema,

Wenda yeye kwako mwema,

bure wapata lawama.

Nguvu usitumie,

ndugu yangu nakwambia,

Utajidhuru mwenyewe,

ukaifuata dunia,

Haki ya mtu ujue,

wala haitopotea,

Wala usijisumbue,

Mungu hajakuridhia,

Mungu ndiye mwenyewe,

omba utafanikiwa,

Omba nawe utapewa,

haifai kumvamia.

Nafsi za watoto wa Afrika lini zitajitambua kutenda yaliyo mema na kuacha yaliyo mabaya? Tutafakari ukweli unadumu na uongo haudumu.

By Jamhuri