2 Rais Kikwete akiongea na Viongozi wa CCM Mkoa Dsm Leo jijiniHistoria inaonesha kuwa vipindi fulani katika mustakabali wa nchi unalazimisha kupima nini ni janga zaidi ya jingine.
Marehemu Samora Machel na Frelimo walikubali kutia saini Mkataba wa Nkomati wa ushirikiano na makaburu kama mkakati wa kujinusuru, na kutoa nafasi kukabili janga kubwa kuliko yote wakati huo, la kuondolewa Serikali ya Frelimo na Renamo ikisaidiwa na makaburu.
Wakomunisti wa Afrika Kusini waliingia ubia na ANC ya mabwanyenye weusi ili kutokomeza kwanza ukaburu na mapambano na ubepari yaje baadaye.


Katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wakomunisti walishirikiana na mabwanyenye wa mlengo wa kulia na kati kutokomeza janga kubwa zaidi wakati huo la ufashisti, yaani ubepari wa mlengo wa kulia kupitiliza.
Hivyo hivyo, mapambano ya kuleta Uhuru wa Tanganyika yalivyounganisha nguvu za mabwanyenye Wazungu na Waasia pamoja na zile za wakulima na wafanyakazi wa rangi zote kwa azimio lile la Mkutano Mkuu wa TANU wa 1958 pale Tabora.
Hivyo hivyo, Mandela na ANC waliingia “urafiki wa mashaka” na De Clark, kiongozi wa makaburu ili kuondolewa kwa ukaburu kuwe kwa amani ya “kula matapishi” ya kuwalaani huko nyuma kuwa ni wabaya wa Mwafrika!


Mabadiliko ya haraka haraka yanayoendelea hapa Tanzania yenye lengo la kuiondoa CCM madarakani kama chama dola kinachodumaza na kudhoofisha ushindani wa kisiasa miongoni mwa mabwanyenye wa tabaka tawala Tanzania, ni mabadiliko yatayoleta neema kwa Watanzania wote.
Ile tu CCM kudhoofishwa na kujiunga Ukawa kwa Edward Lowassa ni kuvuja kwa pakacha ambayo ni nafuu ya mchukuzi. Ni kuondoa kizingiti kikuu cha kushamiri kwa demokrasia pana na maendeleo endelevu Tanzania ambacho ni kuhodhiwa na ukiritimba wa chama dola cha CCM kinachojinadi kama chama cha mlengo wa kushoto wakati ni chama cha mlengo wa kulia kama vyama vyote vya siasa Tanzania kwa sasa.


Kumeguka kwa CCM-Mamboleo kama taasisi ya kakundi ka wanamtandao ulioingiza Serikali ya sasa ya Tanzania madarakani mwaka 2005, ni faraja kwa wote wenye kuitakia mema nchi hii na ni kiashiria cha kukomaa kwa vuguvugu la ukombozi wa pili wa Tanzania, utakaochukua sura ya demokrasia zaidi ili kuwa na maendeleo endelevu zaidi yapatikane kupitia kupatikana nafasi chanya zaidi ya kupitishwa kwa Katiba Mpya kama ilivyopendekezwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
 Kwa mara ya kwanza vyama vya siasa vya upinzani kiuhalisia (tofauti na vile ambavyo vimebebwa na watawala wa sasa kwa lengo la kuua upinzani wa kisiasa kijanja kijanja kama ACT-Wazalendo), sasa vimeunganishwa na kupigania Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba (Ukawa) badala ya kuunganishwa na kutaka kuiondoa CCM madarakani pekee.


Ghafla mwanasiasa mwenye nguvu nyingi ndani ya chama cha kifisadi cha CCM, mwanasiasa ambaye umaarufu wake umetokana na kuongoza mtandao uliouweka utawala wa sasa wa CCM madarakani, Edward Lowassa, amekasirishwa na kukatwa jina lake na aliodhani ni rafiki zake ndani ya CCM na kuamua kusema basi na lolote liwe kwa kujiunga na vuguvugu la kupigania Katiba Mpya!
Naye sasa kang’amua kuwa Katiba ya sasa na ile Pendekezwa ni za ovyo maana haziruhusu kuwapo mgombea huru bila mizengwe. Hasira za Lowassa zimezaa tunda zuri la kung’amua kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko kupitia Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba.


Hasira hizi za mkizi ni furaha ya mvuvi na ni busara kwa viongozi wa Chadema na Ukawa kwa ujumla kutoongopa “kula matapishi yao” kwa kumkaribisha Lowassa …huyu huyu waliyemwita fisadi… kujiunga na Ukawa na kugombea urais. Nafasi ya kihistoria imejitokeza ya kuiondoa CCM madarakani kwa amani!
Sishangai wasaliti wa vuguvugu la kuiondoa CCM madarakani wanatushauri sisi Watanzania wenye shauku ya kuutumia upenyo huu wa mpasuko ndani ya CCM kuiondoa madaraka.
Eti tuombe radhi kwa “kula matapishi yetu” wote tuliowahi kumwita Lowassa fisadi! Wao wanataka tuendelee kuvumilia kutawaliwa na CCM labda kwa miaka mitano au zaidi hivi mpaka chama kipya cha watakatifu kiitwacho ACT-Wazalendo kitakapokuwa tayari kututawala badala ya CCM!
Sishangai kusikia ushauri huu kutoka kwa wasaliti hawa ambao kazi yao hata huko nyuma imekuwa ni kuudhoofisha upinzani dhidi ya CCM na kuisaidia CCM iendelee kuwa madarakani! Hawa jamaa ni wasomi sana na ni wajanja sana, hilo lazima kulikiri.


Sitashanga kama haya ninayoyasema yatapigwa madongo na wasaliti hawa! Historia itakapoandikwa baada ya Ukawa kupata viti vingi zaidi Bunge lijalo, au hata kuuchukua urais na kupata Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba, itawapa hukumu yao stahiki.
Wajanja na werevu hawa! Bila shaka wanaoomba Ukawa ishindwe kupata viti vingi Bunge lijalo na iukose urais na hivyo tuendelee kutawaliwa na CCM na wao wapate viti vya kutosha kuwa viongozi wakuu wa eti upinzani murua wenye maadili ya Azimio la Arusha Tanzania!
Ni haki yao ya binadamu kuendelea na matumaini haya kama na sisi tulivyo na haki ya kuendelea na matumani yetu ya uwezekano wa ushindi mnono chini ya Ukawa dhidi ya ukiritimba wa chama kimoja – chama dola cha CCM.

 

By Jamhuri