Kwanza nianze kwa kuwasalimu na kuwapa hongera kwa kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu. Najua mashabiki na wafuasi wa wagombea, presha zinapanda na kushuka kila siku. Nawatakia heri kwa kuwa maisha yataendelea hata baada ya Oktoba 25, sisi wa mraba huu ngoja tuendelee na kazi yetu.

  Leo nitachambua kwa kina yahusuyo biashara ya daladala. Kwa wale wanaofuatilia makala zangu tangu miaka mitatu nyuma, watakuwa wanakumbuka kuwa nimewahi kueleza kidogo kuhusu biashara ya daladala.

  Nimeanza kupanua mjadala wa daladala lakini lengo langu ni kupitia pia biashara za bodaboda, guta, bajaji na vikirikuu. Kwa nini? Ni kwa sababu hizi ni biashara ambazo watu wengi wakishapata fedha za pamoja wanakimbilia kuzianza pasipo kupata ABC zake. Nitakuletea ABC kwa kina.

  Baada ya kununua basi dogo la kwanza (Hiace) na kulisajili kwa biashara ya kusafirisha abiria mjini (daladala); nilikutana na ulimwengu mpya wa changamoto za biashara za magari. Changamoto ziliponizidia niliaazimu kukutana na walionitangulia kwenye biashara hiyo ili nipate hazina ya ushauri. 

  Nikamfuata mzee wangu mmoja hapa mjini Iringa ambaye ameanza biashara ya kusafirisha mizigo na abiria tangu mwaka 1978. Mzee wangu huyu baada ya kunisikiliza aliniambia sentensi moja tu na akasema huo ndiyo ushauri anaonipa na ambao utanisaidia. 

 Alisema hivi, “Kijana wangu! Ili umudu biashara ya magari hasa hizi daladala unatakiwa uwe mjeuri-jeuri kwa madereva, makondakta na wakati mwingine kwa matrafiki”. 

  Nikataka anipe ufafanuzi kuhusu hili ndipo akaongeza ufafanuzi huu, “Hawa watu ninaokwambia usicheke nao ndiyo ambao wanaweza kukuliza ama kukufanya ufurahi. Ukizubaa katika hili usishangae kujikuta muda umepita, gari limechakaa na fedha za kununulia gari jingine huna.” Ushauri wa mzee wangu huyu niliufanyia kazi na ulizaa matunda (kwangu).

  Uzoefu wangu katika biashara hii ya daladala unachagizwa pia na nafasi ya uongozi niliyopata kushika kuanzia mwaka 2009 hadi januari 2012. Nilikuwa makamu mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa mabasi ya abiria mkoani Iringa kinachojumuisha magari yote ya abiria ukiacha mabasi ya mikoani. Nafasi hii ilinipa kufahamiana na kushirikiana na wafanyabiashara wengi wa magari ya abiria Iringa. 

 Hivyo, nafahamu chungu na tamu za biashara ya daladala na machozi yao nayajua. Ukiacha changamoto ya faida (ambayo nitaichambua kwa kina kwenye makala hii), biashara ya daladala ina “timbwili-timbwili” si mchezo.

  Madereva wanasumbua sana, faini za barabarani zisizoisha na uharibifu wa magari ni kama chachandu chungu kwenye biashara hii. Kati ya biashara nilizowahi kuzifanya,s biashara ya daladala inaongoza kwa kupasua kichwa. 

 Wakati fulani huko nyuma wamiliki wa daladala Dar es Salaam waliwasilisha kusudio la kupandisha nauli za daladala kwa asilimia mia tatu (300%) mbele ya baraza la watumiaji wa huduma za usafiri. Baraza hilo pamoja na Sumatra waliwagomea wamiliki wa daladala kwa sababu mbalimbali.

  Moja ya sababu hizo ni pamoja na mosi; wamiliki wa daladala walishindwa kuwasilisha taarifa za kifedha za biashara zao (approved financial statements),

pili sababu walizozitoa kuhusu kupanda gharama walidai (exaggerated) zilikuzwa mno na kukosa ushahidi wa bei katika soko. Baada ya kufuatilia mnyukano ule niliwahurumia sana wamiliki wa daladala kwa sababu wenye rungu la kuwasaidia hawajui viatu vya umiliki wa daladala vinavyobana na kuumiza.

  Nimetafiti biashara hii katika mikoa ya Mbeya, Morogoro na Dodoma huku Iringa nikiwa nimeifanya kwa vitendo. Sehemu karibu zote changamoto zinafafanana ingawa kuna tofauti ndogondogo kutegemea na tamaduni za kimaeneo.

  Sehemu hizi zote viwango vya fedha inayolazwa ni kati ya Sh. 30,000 na 40,000 kwa siku kwa mabasi madogo (Hiace Super Roof). Kwa mabasi ya kati (Coaster) kiwango kwa siku ni kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 80,000 kwa siku.

  Sasa twende kimizania ya uhasibu hapa. Bei ya kununua basi dogo (Toyota Hiace Super Roof) pamoja na kusajili leseni, njia, na taratibu zote ili ianze biashara ni kati ya Sh. milioni 20 hadi milioni 25. Bei ya kununua basi la kati (Coaster) ni kati ya milioni 35 hadi milioni 45. Magari hayo yote ni yale yaliyotumika kule Japan (Used Cars).

  Tukokotoe mahesabu ya basi dogo. Kwa upande wa mapato kama gari inalaza Sh. 30,000 kwa siku ina maana kwa mwezi unakusanya Sh. 840,000 (laki nane na arobaini elfu). Hesabu hizi ni kwa siku 28. Siku mbili kikawaida hutengwa kwa ajili ya kufanya ‘service’ ya gari ambayo ina fanyika kwa mwezi mara mbili kila baada ya siku 14.

  Tushuke kwenye matumizi. Galoni moja la kilainishi kizuri (oil) ni Sh. 45,000 gharama ya kubadilisha sahani za breki ni Sh. 25,000 vifaa ambatanishi vya ‘service’ ni karibu Sh. 20,000. Ukichanganya na ufundi na ikiwa unafanya service ya uhakika katika gari lako kila service moja unatumia Sh. 100,000 kwa kadirio la chini. Katika kipengele cha ‘service’ kwa mwezi unatumia kama laki mbili.

  Mshahara wa dereva kwa mujibu wa sheria za Sumatra zinazoambatana na masharti ya kupewa leseni yanakutaka mmiliki wa gari ulipe kuanzia kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi Sh. 80,000. Kodi za Serikali ikiwamo leseni ya barabara, leseni ya njia, zima moto, mapato na ushuru wa manispaa/jiji ni wastani wa Sh. 60,000 kadirio la chini.

  Nyingi ya kodi hizi zinalipwa kwa mwaka lakini hapa nimezigawanya katika mafungu ya miezi 12. Mwisho tujumlishe mshahara wa wewe mjasiriamali unayemiliki gari. Najua wajasiriamali wengi hawana utaratibu wa kutenga mishahara yao kwa biashara zao, lakini hata kama hutengi mshahara tukadirie kuwa unajilipa Sh. 80,000 tu kwa mwezi.

  Sasa ukichukua mishahara ukajumlisha na kodi ukajumlisha na gharama za matengenezo (service) unapata matumizi ya Sh 420,000. Kwa haraka haraka unaweza ukadhani faida inayobaki ni Sh. 420,000. Hapa ndipo wafanyabiashara wengi wa magari hufilisikia kwa kusahau jambo la muhimu kuliko yote.

  Jambo hili la muhimu ni gharama ya uchakavu wa gari (depreciation cost). Gharama hii kitaalamu hutakiwa kujumuishwa kwenye kipengele cha matumizi. Tunaposema gharama ya uchakavu ni pale unapoelewa kuwa ikiwa gari inatembea basi tairi zinazidi kuisha, vyuma vinasagika na bodi linachakaa.   Kinachoamua kiwango cha gharama ya uchakavu ni makadirio ya muda ambao gari lako litakaa kabla ya kuchakaa kabisa. 

  Kuna njia kadhaa za kitaalamu, lakini hapa nataka nitumie njia rahisi ya  ‘kijasiriamali’ ili tuelewe vema. Mathalani, gari yako inapita kwenye barabara nzuri unaweza kukadiria kuwa uhai wa gari lako utakuwa ni miaka mitano. Unachofanya unachukua thamani ya kununulia hadi kusajili gari ianze biashara kisha unagawanya kwa miaka mitano. 

  Twende pole pole hapa. Tumesema wastani wa chini wa basi dogo ni Sh. milioni 20 hadi ianze biashara. Ukichukua Sh. milioni 20 ukagawanya kwa miaka mitano unapata Sh milioni nne ambayo ndiyo gharama ya uchakavu kwa mwaka.

  Sasa chukua milioni hii nne kisha gawanya kwa miezi 12 unapata wastani wa Sh. 333,000 (laki tatu na thelathini na tatu elfu). 

  Hii fedha tunaiingiza kwenye sehemu ya matumizi. Kwa maana hiyo jumla kuu ya matumizi yetu kwa mwezi inakuwa ni Sh. 753,000 (laki saba na hamsini na tatu elfu). Ili uelewe faida HALISI unayozalisha kwa mwezi chukua mapato ya mwezi 840,000 kisha utoe na matumizi ya mwezi (753,000). Ukikokotoa hapo utaona faida HALISI ya biashara ya daladala ikiwa una basi dogo kwa mwezi ni Sh 87,000 tu! 

 Najua mahesabu haya yatawashtua wengi na wengi wanaweza wasiyaelewe na kwa kutoyaelewa wanaweza wasiyakubali. Bahati nzuri ni kuwa nimeshafanya biashara hii huku nikiwa na digrii ya biashara kutoka chuo kikuu, hivyo naelewa ninachokisema hapa. Labda nitafsiri maana ya mahesabu hayo hapo juu kwa lugha nyepesi na ya picha. 

  Iko hivi; ukinunua gari la Sh. milioni 20 leo, baada ya miaka 5 linaweza kuwa limeshachakaa kabisa. Wakati huo gari litakapochakaa unatakiwa uwe na fedha mkononi za kununua gari jingine kutoka katika biashara hiyo hiyo na ubakiwe na fedha nyingine ambayo ndiyo tutaiita FAIDA. Ile hela utakayorudishia gari lililochakaa ni mtaji ulioanza nao.

  Kwa mahesabu hayo hapo juu ambako tumeona faida HALISI ya daladala ikiwa unamiliki “Hiace Super Roof” ni Sh 87,000. Kwa faida hiyo ya Sh. 87,000 kwa mwezi itakuchukua Mjasiriamali miaka 19 ili afanikiwe kununua gari jingine la pili!

Mliowahi kufanya biashara ya daladala mtakubaliana name, kuwa ukiona mtu ameongeza daladala ya pili ndani ya mwaka mmoja ama miwili basi uwe na uhakika kuwa fedha ya kununulia gari ya pili hajaitoa kwenye gari ya kwanza kwa asilimia mia moja. Ni ama amechukua mkopo au fedha ameongezea kutoka vyanzo vingine. 

  Naomba nieleweke vema hapa. Sisemi kuwa biashara ya daladala hailipi, la hasha! Lakini faida HALISI iliyopo kwenye daladala ipo tofauti sana na vile Sumatra na abiria wanavyoitazama ama kuifikiria. Mtazamo na mawazo ya wadau hawa ndiyo yamekuwa yakisababisha kuwakatalia wenye daladala ama kuwakubalia kwa mbinde kila wanapotaka kuidhinishiwa kupanda kwa nauli.

  Mathalani, kilainishi (oil) ambacho mwaka 2006 kilikuwa kikiuzwa Sh. 19,000 leo kinauzwa Sh. 45,000. Tairi ambalo wakati huo liliuzwa kwa Sh. 85,000 leo linauzwa Sh. 165,000. Gari lililokuwa linauzwa Sh. milioni 12 mwaka 2006 leo linauzwa Sh. milioni 22 (Toyota Hiace Super Roof). Kwa mabadiliko hayo nauli za daladala zilitakiwa zipande kwa asilimia 236 kutoka mwaka 2006 hadi leo. 

  Lakini hali ni kinyume, kwani maeneo mengi nauli ya daladala imeongezeka kwa kati ya shilingi 50 hadi 100; ongezeko la kati ya asilimia 25 hadi 50 tu. Ndiyo maana Sumatra na baraza la watumiaji walipowagaragaza wamiliki wa daladala kwa kufutilia mbali madai yao ya kupandisha nauli, nilijichekea na kusikitika tu.

  Hata hivyo, sina neno na wala sina lawama kwa Sumatra wala baraza la watumiaji; kwa sababu wenye daladala wenyewe walishindwa kujitetea utetezi wenye nguvu za hoja. Ukitaka kuanza biashara ya daladala ni vema ukayajua haya. Tukutane wiki ijayo!

By Jamhuri