Wachezaji watano wamependekezwa kuwania tuzo ya BBC ya Mchezaji Bora wa soka barani Afrika mwaka 2018. Wachezaji wote wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Wachezaji walioorodheshwa mwaka huu ni Medhi Benatia (Morocco), Kalidou Koulibaly (Senegal), Sadio Mane (Senegal), Thomas Partey (Ghana) na Mohamed Salah (Misri).

Upigaji kura ulianza rasmi Novemba 17, saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki na utakamilika Desemba 2, saa tano usiku.

Mshindi wa tuzo hiyo atatangazwa katika kipindi cha BBC World News Desemba 14, saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki. Orodha ya waliopendekezwa imeandaliwa na jopo la wataalamu wa soka kutoka barani Afrika.

Wasifu wa wachezaji waliopendekezwa

Beki wa kati wa mabingwa wa Seria ‘A’ ya nchini Italia, Juventus, Medhi Benatia, 31, ameshinda taji la ligi hiyo mara nne mfululizo mwaka huu, tuzo mbili kati ya hizo amezipata akiwa na mabingwa wa Bundesliga, Klabu ya Bayern Munich na mbili nyingine akiwa Juventus.

Benatia alikuwa nahodha wa Morocco katika michuano ya Kombe la Dunia lililochezwa nchini Urusi na kuishuhudia timu ya taifa ya Ufaransa ikishinda taji hilo baada ya miaka 20.

Mlinzi wa Klabu ya Seria ‘A’, Napoli, Koulibaly, 27, alicheza vema katika mchezo dhidi ya vigogo wa ligi hiyo ya Italia, Juventus,  kinyang’anyiro cha fainali ya Ligi ya Serie ‘A’ ya Italia ikiwa ni pamoja na ushindi maarufu dhidi ya miamba hao wa ligi ya mabingwa. Koulibaly aliichezea Senegal dakika zote 270 katika michuano ya Kombe la Dunia.

Mshambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane, 26, pia aliichezea Senegal katika michuano ya Kombe la Dunia, ambapo aliiongoza timu yake kushinda mechi dhidi ya Japan, pamoja na hayo timu hiyo haikusonga mbele katika hatua ya 16 bora.

Alikuwa mfungaji bora wa pili katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu uliopita – aliifungia Liverpool mabao 10, ikiwa ni pamoja na bao moja alilolifunga walipochapwa 3 – 1 na Real Madrid katika mchezo wa fainali.

Kiungo wa kati wa Klabu ya Atletico Madrid  ya nchini Hispania, Partey, 25, alichaguliwa kuwa katika kikosi cha kwanza cha Diego Simeone baada ya kuonyesha umahiri, ikiwa ni pamoja na kuwa mchezaji wa ziada katika fainali ya Kombe la Europa, ambapo waliishinda Marseille.

Aliifungia Ghana katika mechi ya kimataifa ya kirafiki walipochuana na Japan na Iceland.

Mshambualiaji wa Liverpool, Mohamed Salah, 26, alishinda taji la mfungaji wa mabao mengi zaidi (32) katika Ligi Kuu ya England mwezi Mei. Sawa na Mane, alifunga mabao 10 katika Ligi ya Mabingwa kuelekea fainali. Aliifungia Misri mabao yote ya Kombe la Dunia.

Mshambuliaji wa Liverpool, Salah, ndiye aliyeshinda tuzo ya mwaka jana. Wachezaji wengine walioshinda tuzo hiyo ni pamoja na Jay-jay Okocha, Michael Essien, Didier Drogba, Yaya Toure na Riyad Mahrez.

By Jamhuri