Haraka haraka baada ya kuanguka kwa jengo lenye ghorofa 16 katika Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam, viongozi wa Serikali wakatoa amri ya kukamatwa kwa Mkandarasi, Mhandisi Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Ukaguzi wa Majengo wa Manispaa ya Ilala.

Tunaoujua utendaji kazi wa staili ya zimamoto, wa vyombo vyetu mbalimbali nchini, hatukushangazwa kwa hatua hiyo. Naandika makala haya wakati watendaji hao wakiwa bado hawajafikishwa mahakamani, kwa hiyo naomba ieleweke kuwa sikusudii kuingilia uhuru wala faragha ya mahakama.


Kukamatwa kwa viongozi hao ni uonevu. Nasema ni uonevu kwa sababu katika Taifa letu, sidhani kama kuna mahali au mtendaji anayeweza kumnyooshea kidole mwenzake.


Dk. Kitila Mkumbo, katika moja ya makala zake juu ya kushangaa kwetu matokeo ya kidato cha nne, aliuliza; “Ni sekta gani katika nchi hii matokeo yake yangebandikwa ingefaulu?’ Tupo hoi kuliko tunavyofikiria, katika sekta zote! Hata ungefanya leadership audit ya viongozi wetu katika nyanja mbalimbali sijui wange-score ngapi.”


Hoja ya Dk. Mkumbo ni nzito, na kwa kweli inapaswa kuwa mwongozo wa kila mmoja wetu kabla hajachukua dhima ya kuwakamata au kuwahukumu wengine.

 

Katika sakata hili la kuporomoka kwa majengo, kiongozi wa kwanza aliyestahili “kukamatwa” na kuhojiwa, ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda (pichani). Lakini nani mwenye jeuri hiyo?


Wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2008/2009, Pinda alitumia rejea kutoka matokeo ya Tume iliyokuwa imeundwa na mtangulizi wake, Edward Lowassa, alisema, akasema kati ya maghorofa 505 ambayo waliyakagua, 147 yalikutwa hayana nyaraka za ujenzi.


Lowassa aliunda Tume baada ya jengo la Hoteli ya Chang’ombe Village Inn iliyopo Keko, Dar es Salaam, kuanguka mwaka 2006 na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.

 

Pinda aliliambia Bunge kuwa Tume hiyo ilibaini maghorofa 81 yalikutwa yamekiuka masharti ya ujenzi huku MAGHOROFA MENGINE 22 WENYEWE HAWAKUPATIKANA na yalikuwa yamejengwa bila kuzingatia sheria za ujenzi.

 

“Can you imagine, mtu kaamua kupandisha ghorofa lake hapo bila kufuata taratibu za mamlaka husika, hii ni hatari kubwa,” alisema Pinda.

 

Alisema maghorofa mengi yanayojengwa Dar es Salaam yanajengwa holela bila kufuata taratibu za ujenzi, hivyo kuyafanya kuwa hatari kwa maisha ya binadamu. Alionya kwamba kama hatua za haraka hazitachukuliwa na serikali, kuna hatari ya watu wengi kupoteza maisha kwenye maghorofa hayo ambayo yanachipuka kama uyoga katikati ya Dar es Salaam.


“Tatizo ni kubwa…kuna hatari ya kupoteza maisha ya Watanzania wengi zaidi kuliko hili lililotokea juzi kama tukiendelea kuwaachia Manispaa suala hilo,” alisema Waziri Mkuu. Alisema.


Akasema Serikali inaandaa utaratibu mzuri ili kuhakikisha maghorofa yanayojengwa yanakuwa bora kwa kufuata taratibu zote za ujenzi. Tangu Pinda alipotoa ahadi hiyo mbele ya wabunge mwaka 2008, bado “Serikali inaandaa utaratibu!”

 

Ndiyo maana nasema kama ni mzembe wa kwanza kumhoji kwenye hili jambo, ni Waziri Mkuu. Hawa “dagaa” wa Ilala waliokamatwa ni kuwaonea tu kwa sababu aliyepaswa kuwashughulikia, alibweteka.

 

Pili, unaona hapo akikiri kuwa kuna maghorofa 22 ambayo wenyewe hawakupatikana! Haya ndiyo maajabu ya Tanzania! Ni Tanzania pekee ambako hata ghorofa linaweza kuibuka kwa staili ya nguvu za “kimungu” na mwenyewe asijulikane! Kweli Serikali inaweza kusema kuna maghorofa ambayo wenyewe hawajulikani? Je, imeyataifisha? Haya yanatokea Tanzania pekee.

 

Kama alivyosema Dk. Kitila, katika jamii yetu sasa karibu kila mahali ni bure tu. Mahakama matatizo, Polisi matatizo, ufaulu shuleni matatizo, ajali barabarani matatizo tu, utapeli kila mahali, uchakachuaji kwa wajenzi ni matatizo, Magereza shida tu, Usalama wa Taifa upo kwa ajili ya kuwapokea na kuwalinda viongozi – si Usalama wa kubaini upuuzi na kuushughulikia kabla madhara hayajatokea.


Kwa hili la ghorofa kama Pinda hatahojiwa, hao waliokamatwa watakuwa wanaonewa tu! Kama mwenyewe anavyopenda kusema, “Liwalo na liwe”, nami nasema hivyo hivyo liwalo na liwe.

By Jamhuri