Waswahili siku zote husema adaa ya mja kunena, muungwana ni kitendo. Serikali ya China ni mfano mzuri wa kuigwa kwa jinsi inavyosimamia sheria, sera na taratibu zake kwa vitendo. Natamani serikali ya China ingekuwa Tanzania ili, pamoja na mambo mengine, ishughulikie kwa vitendo watumishi wanaotumia vibaya madaraka na ofisi za umma.

Wiki iliyopita, serikali hiyo iliweka historia ya kipekee ilipomfukuza kazi ofisa wake kwa kosa la kutabasamu katika eneo la ajali iliyoua watu 36, Agosti 26, mwaka huu. Ofisa huyo, Yang Dacai (55), alivuliwa usimamizi wa masuala ya usalama na ujumbe wa kamisheni ya nidhamu ya Chama cha Kikomunisti cha China, Jimbo la Shaanxi.


Shirika la Habari la China (Xinhua), lilisema serikali iliona kitendo cha kutabasamu katika tukio la majonzi ni utovu wa nidhamu kwa mujibu wa sheria, sera na taratibu za utumishi wa umma. Serikali ilikataa utetezi wa Dacai kwamba alitabasamu kuwafariji maofisa wenzake walioonekana kuelemewa majonzi wakati wakimpatia taarifa za ajali hiyo.


Serikali ya China imetoa adhabu hiyo kali dhidi ya ofisa huyo, kulinda kiapo chake cha kusimamia kwa vitendo taratibu za utendaji wa watumishi wake. Swali: Hivi kama serikali yetu ingesimamia kwa vitendo sheria, sera na taratibu zilizopo, ni watumishi wangapi wangeepuka yaliyomkuta Dacai? Wangapi wangeepuka adhabu za kuvuliwa madaraka, kufukuzwa kazi na kutupwa jela? Jibu: Wengi wangelia!


Tanzania pengine ndiyo nchi pekee duniani yenye watumishi wa serikali ambao mara nyingi huburuza ofisi za umma. Wengi wanadharau, kudhihaki na kupuuza wateja wao (wananchi wanaokwenda kutafuta huduma).  Tembelea ofisi za serikani nchini, zikiwamo halmashauri (za wilaya, miji, manispaa na majiji), vituo vya afya, polisi, mapato, elimu na kadhalika. Watumishi wengi wanaingia, wanatoka na kuhudumia wateja muda wanaotaka!

 

Wengine wamegeuza ofisi za umma vijiwe vya kupiga soga na masimango, kujipodoa, kufanya mawasiliano binafsi, kutazama filamu kwenye kompyuta na runinga, kuomba na kupokea rushwa! Bahati yao serikali yetu si kama ya China. Binafsi nimekuwa nikijiuliza sababu ya serikali yetu kukosa ujasiri wa kufanya uamuzi mgumu dhidi ya watumishi wanaotumia vibaya ofisi za umma. Hivi kweli haijui madhara ya kucheka na nyani shambani ni kuvuna mabua?

 

Wachina ni binadamu sawa na Watanzania. Serikali ya China inaundwa na binadamu sawa na wanaounda serikali ya Tanzania. Kwanini serikali yetu iendelee kukosa dhamira ya kweli ya kusimamia kwa vitendo taratibu utendaji wa wutumishi wa umma?


China hivi sasa inazidi kuweka ushindani mkali kiasi cha kukaribia kuipiku Marekani katika ukuaji wa uchumi. Wengi tunajua mafanikio hayo ya China yanachangiwa na uimara wake katika kusimamia sheria, sera na taratibu ilizojiwekea kwa manufaa ya wananchi wake. Faida za serikali kusimamia kwa vitendo sheria, sera na taratibu zake ni pamoja na kuimarisha uongozi bora unaozingatia sheria na kuwezesha mipango ya maendeleo ya wananchi kutekelezwa kwa ufanisi.


Kusimamia masuala hayo kwa vitendo, maana yake ni kudhibiti mianya ya rushwa, udokozi wa fedha za umma na kero nyinginezo zinazokwaza maendeleo ya wananchi.


Umefika wakati serikali yetu ijifunze kutoka China isimame imara, iwe jasiri na itekeleze ahadi zake kwa vitendo. Isisite kuwafukuza kazi mawaziri, makatibu wakuu, askari polisi, mahakimu, wauguzi na watumishi wengine wanaoburuza na ‘kuchafua’ ofisi za umma.


Kama kwa kitendo cha kutabasamu tu katika eneo la ajali Dacai amekumbwa na adhabu ya kuvuliwa madaraka na kufukuzwa kazi moja kwa moja China, ingekuaje angepatikana na kosa la rushwa? Bila shaka angenyongwa! Hatua iliyochukuliwa na serikali ya China dhidi ya Dacai inadhihirisha jinsi ilivyodhamiria kwa dhati kudhibiti mizaha na mizengwe ya watumishi kazini isiyo na tija kwa wananchi wake.


Ndiyo maana ninatamani serikali ya China ingekuwa Tanzania. Kuna haja ya serikali yetu kujifunza kutoka China iweze kudhibiti watumishi waliojigeuza miungu watu, watega kazi, wenye lugha chafu kwa wateja, wala rushwa na wahujumu mali za umma.

 

Tanzania haiwezi kujengwa na kasumba za kuoneana haya na kulindana, huku wananchi wengi wakikabiliwa na umaskini unaojumuisha ukosefu wa huduma bora za afya na elimu. Chondechonde viongozi wa serikali yetu, chukua hatua. Hakuna lisilowezekana chini ya mbingu.


By Jamhuri