*Wajanja watajirika huku serikali ikiambulia ‘makombo’

*Wachimbaji Mirerani wavamia Epanko

*Mkuu wa Mkoa akiri udhaifu, asema wamewasiliana na mamlaka

 

NA ANGELA KIWIA

Wakati serikali ikirekebisha sheria ya madini ili kunufaika na rasilimali  hizo za taifa, hali ni tofauti kabisa kwenye machimbo ya madini ya Spinel yanayochimbwa Epanko, Ulanga, mkoani Morogoro.

Uchunguzi wa gazeti la JAMHURI, umebaini kwamba wafanyabiashara wa madini hayo wameendelea kuchimba na kuuza madini, bila mwakilishi wa serikali kuwepo eneo husika hivyo kusafirishwa nje ya nchi bila serikali kupata stahiki zake.

Uchunguzi huo umegundua wafanyabiashara hao wamekuwa wakichimba madini hayo Kijiji cha Epanko, Wilaya ya Ulanga Mkoa wa Morogoro na kuyasafirisha kwenda Mkoani Arusha kisha kuyauza nje ya nchi.

Carat moja ya Spinel nyekundu kutoka Epanko, inauzwa kati ya dola za Marekani 200 hadi 500 kutegemea na ubora wake. Soko lake kubwa liko nchini Kenya, Thailand na Australia.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini madudu kadhaa, ikiwemo biashara hiyo kufanywa na raia wa kigeni ambao wamekuwa wakifika Mahenge na kununua madini kisha kuyasafirisha bila kuwepo kwa utaratibu maalum kama ambavyo wanunuzi wa tanzanite wamekuwa wakifanya kabla ya kujengwa ukuta.

Vyanzo vya habari vimelieleza JAMHURI kuwa yupo mzungu mmoja kutoka Australia amekuwa akifika mahenge tangu mwaka 2013- 2016 na kununua madini kwa kificho na kuondoka nayo huku maafisa wa serikali wakiwa hawajui lolote.

JAMHURI halitataja jina la mzungu huyo kutopkana na kutofanikiwa kumpata na kuzungumza naye. Lakini vyanzo vyetu vimesema amekuwa akifika Mahenge na kutumia vijana ambao wamekuwa wakimfanyia udalali na wachimbaji wadogo ambao humuuzia madini hayo kwa bei rahisi.

“Unajua hapa kwetu wanakuja watu wengi wananunua madini kwa bei ya chini na kuondoka nayo. Hao wanaochimba nao hawalipi chochote kwa serikali kwani madini yanaondolewa hapa na kupelekwa Arusha na matajiri, serikali haiambulii chochote,” mmoja wa wachimbaji wadogo ameliambia JAMHURI.

Mfanyabiashara huyo raia wa kigeni, ametajwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na mfanyabiashara mmoja jijini Dar es Salaam anayemiliki ofisi Ada Estate, Kinondoni ambaye anaelezwa kuwa na mtandao wizara ya madini.

“Huyu mfanyabiashara wa Kinondoni ndiye amekuwa akimsaidia mzungu kwenye kusafirisha mzigo wake nje ya nchi. Yeye ndiye anayefahamiana na watu wa madini wizarani na uwanja wa ndege,” kimesema chanzo chetu.

Uchunguzi wa JAMHURI, umebaini kwamba wengi wa wanaojihusisha na uchimbaji wa madini hayo, wanatoka kwenye mgodi wa tanzanite ulioko mkoa wa Manyara.

Pia wachimbaji wengine ni pamoja na raia wa kugeni anayetajwa kwa jina moja la Mark ambaye anachimba madini kwa kutumia leseni ya mzawa, anayetajwa kuwa mshirika wake kibiashara.

Mchimbaji mwingine ni Almas Salim ambaye anachimba katika mgodi wa Alqaeda ambaye amechimba hapo kwa mwaka mmoja sasa na kupata madini mara nne katika kipindi hicho. Mgodi wa Alqaeda ulikuwa chini ya mmoja wa wamiliki wa uchimbaji tanzanite huko Mirerani, Manyara.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake mjini Mahenge, Salim Alaudin Hasham (Salim Almas) ameliambia JAMHURI, kwamba amekuwa akichimba katika mgodi wa Alqaeda kwa mwaka mmoja sasa na amepata madini mara nne tu katika kipindi hicho.

Alipohojiwa ni kiasi gani cha madini amesema kwamba hakumbuki ni kiasi gani alichokipata na kwamba amekuwa akifanya biashara ya madini tangu mwaka 2004. Amekiri kwamba yeye ni mwekezaji katika mgodi wa Alqaeda ambao leseni yake inasomeka kwa jina la Paschal Mpandule pamoja na watu wengine wanne.

Amesema kwamba madini yakipatikana wamekuwa wakigawana kutokana na mkataba uliopo baina ya wabia hao, ambapo amekuwa akigawa asilimia 30 kwa wanahisa na yeye kubaki na asilimia 70 ambazo zinahusisha gharama za uzalishaji pamoja na faida.

Alipoulizwa iwapo amekuwa akiishirikisha serikali na kulipa kodi kutokana na madini yanayopatikana katika mgodi wake amesema, “Tunapopata madini tunalazimika kuyabeba kuyapeleka Dar es Salaam wizarani ili yakakadiliwe tuweze kulipa kodi.”

Alipoulizwa  ni mara ngapi amepeleka madini wizarani kukadiliwa kodi amesema kuwa amepeleka madini hayo mara moja tu na kwamba mara ya kwanza wakati anauza madini alikuwa anatakiwa kuwasilisha risiti ya mauzo ambayo hutumika kufanya makadirio ya kodi.

“Siku zote nilikuwa natakiwa kupeleka risiti ya mauzo ya madini ndiyo wananikadilia kodi, sasa Novemba mwaka jana ndiyo niliambiwa nipeleke madini, niliyapeleka nikakadiliwa kodi kutokana na madini hayo,” amesema Salim Almas.

JAMHURI lilimuuliza baada ya kupeleka madini alikadiriwa kulipa kodi kiasi gani, amesema hakumbuki lakini madini hayo aliyauza kwa dola za Marekani 30,000 (sawa na Sh milioni 67).

Hata hivyo gazeti JAMHURI, lilipata habari kwamba kumekuwepo na unyanyasaji kwa baadhi ya wafanyakazi wa mgpodi wa Alqaeda, kuwa wamekuwa wakivuliwa nguo kwa madai ya kufanyiwa ukaguzi pindi wanapokuwa wanatoka mgodini amesema kwamba hana taarifa hizo.

“Hilo silijui na sijawahi kusikia, huwa tunawavua viatu na kuwakagua mifukoni. Kuhusu kuvuliwa nguo hilo sijawahi kusikia na mimi nilitoa maelekezo ya kukaguliwa lakini sio kuvuliwa nguo kama unavyosema,” amesema Salim Almas.

Salim Almas ameliambia JAMHURI kwamba alianza kufanya biashara ya madini mwaka 2004 na anamiliki kampuni ya Rubi International amekuwa akichimba na kuuza madini. Madini hayo amekuwa akiyauza mkoani Arusha kwenye kampuni ya Prima Gems.

JAMHURI limefanya mahojiano na mmoja wa mkazi wa Epanko na ambaye pia ni mmoja wa wamiliki wa leseni ya mgodi wa Alqaeda, Flora Lyaupe (Mama washoka) ambaye amesema ni mzaliwa wa Epanko tangu mwaka 1960.

“Kuna mchungaji mzungu alikuja alikuwa anaitwa Manfred kutoka Uswiss. Alikuja mwaka 1971 na kutueleza uwepo wa madini eneo letu, hivyo mwaka 1992 tulienda Morogoro mjini kuomba leseni ya uchimbaji ingawa hatukuwa tukijua ni madini gani. Mkoa ulimtuma afisa madini aliyekuwa anaitwa Kikungulilo akatupimia kila mmoja kwa ukubwa wa 900/900 kila mtu,” amesema Flora.

Amesema miaka kumi baadaye, wakaomba tena kibali cha uchimbaji kwa jina la Jonas Mpandule (Washoka). Walikataliwa kupewa leseni mpaka walipofika Dodoma na kuambiwa waende Dar es Salaam, Mnazi Mmoja kwa John Bosco ambaye aliwasaidia wakapimiwa upya huku wakibaki na usumbufu wa kupata leseni.

“Februari 7, 2009 tulikwenda kumuona Rais Jakaya Kikwete, kufikisha kilio chetu. Mwaka 2010 aliagiza tupewe leseni ambayo tulisaidiwa kulipiwa na John Toga na Joseph Mtoga ambao ni wamiliki wa Haleluya Company. Baada ya kutusaidia kulipia leseni tukawafanya wabia,” amesema Frola.

Epanko yatoa jiwe lililoweka rekodi

Flora Lyaupe amesema yeye na wenzake wakiwa katika harakati za kushughulikia leseni, mwaka 2007 kwa mara ya kwanza kampuni ya Franone, ambayo ilikuwa inachimba mgodi unaomilikiwa na Kamota,  ulitoa jiwe kubwa lenye uzito wa kilo 52 lililokuwa ni madini ya Spinel.

Amesema yalikuwa mawe matatu makubwa ambayo yaliondolewa mgodini hapo huku mawe mengine mawili yakichukuliwa na John Ntoga.

Madini hayo yanadaiwa kuuzwa kwa Sh bilioni 45 kwa Hussein Gonga ambaye naye aliuza kwa mfanyabiashara mwingine wa Arusha aliyetajwa kwa jina moja la Bimel ambaye anaelezwa kununua kwa Sh bilioni 127 kisha kuyauza nje ya nchi.

Hata hivyo, JAMHURI limemtafuta Hussein Gonga, anayesemekana kununua madini hayo li kupata undani wa habari yenyewe, ambaye amesema hajawahi kuwa na mgodi huko Epanko na amesisitiza kwamba hiyo migodi ina wenyewe, huku akisisitiza kwamba hajawahi kununua spinel kutoka Epanko.

Kuhusu jiwe la kilo 52, Gonga amesema, “Si kweli kwamba nilinunua madini hayo…ukweli ni kwamba mimi ni mnunuzi wa madini ya aina mbalimbali, madini yote ninayonunua utayaona kwenye vitabu vyangu. Kama ni spinel utaona nimenunua kiasi gani na kuuza.

“Isipokuwa spinel tunanunua kila siku, ila ni huko nyuma. Sasa haipatikani sana nadhanin uzalishaji umepungua sana, hiyo ya Mahenge sidhani kama nimo kabisa….hizo ni hadithi tu si unajua mambo ya mawe.

“Mimi mwenyewe nililetewa hiyo stori kwamba kuna jiwe limepatikana huko Morogoro, nikaenda nikakuta kulikuwa na kesi pale Polisi, waliokuwa wamepata hayo madini waligombana na kupelekena Polisi, hivyo baada ya kufika pale nikakuta watu wengine wameshafanya hiyo biashara,” amesema Gonga.

Wakati serikali ikiwa haipati kitu chochote katika madini hayo, JAMHURI limeambiwa kwamba mzigo huo baada ya kuuzwa ulisindikizwa kwa ulinzi mkali kwa baadhi ya vigogo wa Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, Lyaupe amesema mbali na madini hayo kupatikana katika eneo leo, bado hakuna manufaa yoyote wanayoyapata kutokana na kazi zinazoendelea kufanyika.

Amesema mwaka 2013/14 lilipatikana jiwe kubwa la madini ambalo lilikuwana ukubwa wa zaidi ya kilo 2, ambalo lilikuwa ni Red Spinel na gharama zake hazikufahamika mara moja lilisafirishwa kwenda Mkoani Arusha.

“Mawe yaliyotolewa yalisafirishwa kwenda Arusha kwa kutumia gari maalum. Nasikia wanasema yaliuzwa Sh bilioni 8, mimi niliambulia Sh milioni 8 tu. Hawa watu wanachimba madini kwa kutumia leseni zetu, lakini wanatutesa kiasi cha kufikia hatua ya kutupiga. Wanatupiga na hapa nilipo nimenyang’anywa leseni yangu kwa madai kwamba uwa ametoa pesa nyingi,” amesema Lyaupe.

Gazeti la JAMHURI, lilimtafuta mtuhumiwa mkuu wa utoroshaji wa madini, John Ntoga, ambaye amekiri kuchimba madini hayo kwenye mglodi unaomilikiwa na Lyaupe kwa miaka kadhaa hivi sasa, lakini hakuna madini ambayo yameshapatikana.

Wakati akisema hajapata madini yoyote katika mgodi unaomilikiwa na mama huyo, amejikanganya kwa kukiri kwamba kuna madini ambayto yalipatikana mwaka jana huku akisema hayakuwa madini mengi ingawa hakumbuki ni kiasi gani. Alipotakiwa kueleza yaliuzwa kiasi gani alisema kwamba hana kumbukumbu nzuri ila ni kama Sh milioni 30, Sh milioni 14 na Sh milioni 4-6.

JAMHURI lilimuuliza endapo alilipia kodi kama sharia ya madini in avyotaka, Ntoga ameliambia JAMHURI, hakumbuki kama alilipa kodi hiyo.

“Kinachofanyika yakipatikana madini mnakaa wote huko mgodini mnajadiliana ni kiasi gani kinahitajika kisha tunayauza kwa mnunuzi mmoja mkubwa aliyepo hapa Epanko (Jina tunalihifadhi) tunagawana kiasi kinachopatikana, hicho ndicho kinachofanyika,” amesema Ntoga.

Lyaupe ameliambia JAMHURI, kwamba kila mwaka madini yakekuwa yakipatikana madini mengi lakini yamekuwa yakiondolewa mgodini haraka na kupelekwa Arusha bila hata serikali kujua lolote.

Alipoulizwa kuhusiana na mgodi wa Alqaeda kufanya uzalishaji amesema kwamba mgodi huo tangu mwaka 2014- 16 ulikuwa ukitoa mawe ya madini makubwa ambayo yalikuwa yakikimbiziwa mkoani Arusha.

“Tangu mwaka 2017 mgodi huu anachimba Salim Almas ambaye anatumia leseni ya Paschal Mandule (Washoka), Benjamin Makoti na Mateu Ngonyani. Mwisho wa mwaka jana (2017) yalipatikana madini kiasi mimi binafsi nilipata mgawo wa Sh milioni 5, na wenzangu watatu nao walipata kama mimi,” amesema Lyaupe.

Alipoulizwa madini yanayopatikana mgodini hapo yamekuwa yakisafirishwaje anasema kwamba; “Hapa mawe yanachukuliwa kitemi, watu wanafikia hatua ya kutoleana bunduki zao na kutaka kuuana. Tunaiomba serikali itusaidie tuweze kupata haki yetu pia nayo iweze kunufaika na madini yanayopatikana hapa.”

Amesema kwamba katika madini yanayochimbwa na kupatikana mgodini serikali haijui lolote kwani hakuna afisa yeyote wa serikali katika mgodi huo jambo linalosababisha upotevu mkubwa wa mapato.

Hata hivyo ameeleza kuwa kumekuwepo na kundi la wafanyabiashara kuvamia maeneo ya kijiji na kugawana mashamba yao jambo linalosababisha migogoro ya ardhi.

Chanzo chetu kingine ambacho hakikupenda kutajwa jina lake gazetini kwa sababu za kiusalama, kimesema eneo la machimbo ya Epanko limevamiwa na wachimbaji kutoka Arusha ambao wengi wao ni wafanyabiashara wa madini ya tanzanite.

“Serikali haijui kitu chochote kuhusu Spinel, imeelekeza nguvu na akili zote huko kwenye tanzanite wakati huku kuna madini ya thamani zaidi. Usiwaone watu wa tanzanite ukadhani pesa zote wanapata huko, hapana wanapata huku huku Epanko. Hii kitu inashangaza kuona serikali haijui lakini wapo maafisa wa serikali wanaopata mgao wao huku,” kimesema chanzo chetu.

Amesema kwamba wapo wafanyakazi wawili kutoka ofisi ya madini ya mkoa ambao wamekuwa wakikutana mara kwa mara na wafanyabiashara wa spinel kutoka Epanko, Mahenge.

Chanzo hicho kimesema yupo mzungu anayefahamika kwa jina Mark ambaye amekuwa akichimba madini ya spinel tangu mwaka 2009 kwa kutumia leseni ya Peter Chamtitu na msimamizi wake ametajwa kwa jina la Kassim Mpemba. Mark anaelezwa kumiliki kampuni ya Swala Gem Finder iliyopo Mkoani Arusha.

“Kassim ndiye msimamizi wa mgodi wa Mark, amekuwa akishirikiana naye kwa miaka yote hapa mgodini na kila mmoja anajua hilo. Pia ananunua madini nyumbani kwake na kuyapeleka Arusha. Huwezi kumpata Mark bila kupitia kwa Kassim Mpemba,”amesema mtoa taarifa.

JAMHURI limefanya mahojiano na Kassim Mpemba kufahamu ukweli wa uhusika wake katika biashara ambaye amekiri kumfahamu Mark lakini amekana kufanyakazi naye na kwamba anamfahamu kama mnunuzi wa madini kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Amesema kwamba amekuwa akifanya biashara ya madini kwa miaka mingi ambayo amefanya Tunduru, Arusha na migodi mingine mingi kasoro Mererani na kwamba Mark amekuwa akikutana naye mara kwa mara. Mpemba amesema maisha yake yote yanabebwa na madini.

Alipoulizwa kuhusiana na yeye kuchimba madini kwa kutumia leseni ya Chamtitu amekiri na kudai kuwa ameanza uchimbaji kwa kipindi kifupi sana na hajabahatika kupata madini.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na Mark kuchimba eneo hilo hilo analochimba yeye amekiri na kusema ni kweli anachimba kwa Chamtitu

“Kwa vile wewe ni mwandishi wa habari ungefaidika sana, eneo la madini huwezi kuupata ukweli bila kumkuta muhusika ina maana ungekutana na mimi kwa vile wewe ni mwandishi wa habari ungefaidika faida kubwa sana juu ya pale mahenge ninavyoishi na kazi zangu zinavyokwenda ili ukiongea na mtu akakuelekeza hawezi kukwambia kama nitakavyokwambia.

“Labda nitakapokuwa mahenge ukija nitakueleza vizuri, kwa sababu sisi tunakwenda TRA na habari zetu TRA wanazo jinsi tunavyofanyakazi pale Mahenge,” amesema Kassim Mpemba.

Alipoulizwa analipaje kodi ya mapato kutokana na taarifa kwamba ofisi ya madini haijui kinachoendelea, amesema tangu ameingia Mahenge hajawahi kufanya kazi yoyote zaidi ya migogoro ya mashamba.

“Naomba nikukutanishe na wenzangu tuongee. Ninao jamaa zangu ambao ni masikini kama mimi tunafanya kazi pamoja na baada ya kupata migodi kuna watu hawatutaki pale Mahenge na wametufungulia kesi. Sasa tunapambana na kesi na April 20 tutakwenda tena Mahakamani,” amesema Kassim Mpemba.

Alipoulizwa iwapo ananunua madini nyumbani kwake amesema kwamba ananunua madini ‘machafu machafu’ na kuyakata kwani kwa sasa Mahenge ni vigumu kupata madini ya kununua kutokana na wamiliki wa migodi kudhibiti madini yanayopatikana tofauti na ilivyokuwa awali.

Mmoja wachimbaji (Jina linahifadhiwa) amesema kwamba wafanyabiashara wa madini wamekuwa wakichimba madini na kuidanganya serikali ili kukwepa mapato.

Amesema kwamba, mfano mzuri ni kwamba mwaka jana kuna madini yalipatikana kwa miezi mitatu mfululizo lakini hakuna afisa yoyote wa serikali ambaye anajua kilichopatikana.

“Mwezi wa saba walipata mawe safi kilo tatu, mwezi wa nane yalipatikana mawe yaliyobebwa kwenye ndoo ndogo ambayo yalikuwa zaidi ya kilo 20, mwezi wa tisa yalipatikana madini ambayo yalikuwa mawe matatu kati ya kilo 15-20. Yote haya yalipelekwa Arusha,” amesema.

Mchimbaji huyo ameliambia JAMHURI, wakaguzi wa madini wanapokwenda kufanya ukaguzi wamekuwa wakionyeshwa mawe yasiyo na ubora ambayo yanakuwa yamehifadhiwa kwenye kasiki.

“Huo ndio ujanja hapa, ndio kila mchimbaji mkubwa utakayemwona atakwambia hadhithi hiyo hiyo kwamba anaendelea kutafuta kwa miaka kadhaa na bado madini hayapatikani…huo ni ujanja ambao wamekuwa wakishirikiana kukwepa kulipa kodi za serikali,” kimesema chanzo chetu.

Amebainisha kuwa wakaguzi hao huoneshwa vitendea kazi (baruti, milipuko, kamba na mafuta) vichache vilivyohifadhiwa kwenye stoo ili kuidanganya serikali.

“Inafanyika hivi ili kuonesha hakuna kazi inayofanyika na vifaa havijanunuliwa. Vifaa vinavyotumika kufanyia kazi kama walivyooneshwa maafisa wa serikali vinakuwa vimefichwa sehemu nyingine, ukiwaonesha vifaa vingi si wataona unafanyakazi na uzalishaji ni mkubwa hivyo wataanza kuwafuatilia,” kimesema chanzo hicho.

Chanzo hicho kimebainisha kuwa katika kuhakikisha wanaikwepa serikali waliamua kutofanya matengenezo ya barabara hivyo watendaji wa serikali kushindwa kufika mgodini.

“Hii barabara unavyoiona inawezekana kabisa kufanyiwa matengenezo, lakini hawawezi kutengeneza kwasababu TRA itaona kuwa madini yanapatikana hivyo watadai kodi. Barabara ikiendelea kuwa mbaya hakuna mtu wa serikali atakayefika mgodini na kazi itaendelea bila usumbufu,” amesema.

Chanzo hicho kimewataja kwa majina watendaji wawili wa wizara ya madini ambao wamekuwa wakifika mara kwa mara Mahenge na kukutana na wafanyabiashara hao kwa siri.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba katika eneo linalochimbwa madini ya spinel kulikuwa mto ambao umehamishwa mita chache kuwa kutumia mashine za kuvuta maji.

“Miaka mitatu iliyopita, watu wa mazingira (NEMC) kutoka Dar es Salaam walifika mgodini na kuwataka kuacha kufanya uchimbaji eneo la mto kwa sababu sheria za mazingira haziruhusu. Lakini baada ya kukaa na ‘kuzungumza’ nao na hawajawahi kurudi tena,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI limefanya mahojiano na Kaimu Meneja wa Mamalaka ya Mapato (TRA) Wilaya ya Ulanga, Rasoul Mansoul, kuhusiana na upatikanaji wa madini na kodi inayolipwa kutokana na biashara ya madini ambaye amesema kwamba anachofahamu ni kwamba madini yapo lakini unafanyika utaratibu wa kuwaingiza kwenye mfumo wa kodi wafanyabiashara wote wa madini.

Alipoulizwa inakuwaje madini yanapatikana na yanapita bila kulipiwa kodi amesema kwamba waliofungua kampuni tu ndio wanaolipa kodi ambapo aliitaja kampuni moja tu ya Rubi International, kama mlipa kodi kati ya migodi kadhaa iliyoko Epanko.

Mansoul amesema wapo wanaolipa kodi wa kukadiriwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), walipa kodi wa kutengeneza mahesabu kwa msaada wa mshauri wa kodi aliyeteuliwa na TRA na mlipa kodi anayejikadiria na kupeleka makadirio yake TRA na kufuatiliwa iwapo makadirio hayo yapo sawa.

Alipoulizwa kuhusiana na kodi ya madini yanayopatikana mgodini amesema kwamba hilo linaihusu ofisi ya madini ya mkoa kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na ofisi za madini.

“Kuhusu upatikanaji wa madini na serikali kupata haki yake hilo linahusu ofisi ya madini mkoa. Kuhusu madini yanayotoroshwa sina taarifa, ukizingatia wafanyabiashara wengi wa Mahenge wamesajiriwa Arusha,” amsema Rasoul.

Rasoul amesema kwamba kikosi kazi kinachofanya kazi na watu wa madini kipo Mkoani Morogoro hicho ndicho kinachoweza kutoa ufafanuzi kuhusiana na biashara ya madini inayoendelea huko Epanko.

TRA Morogoro wanena

Kaimu Meneja TRA Mkoa wa Morogoro, Martine Shirima, ameliambia gazeti la JAMHURI kwamba TRA imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na ofisi ya madini.

Amesema kwamba ofisi yake inawatambua wafanyabiashara wa madini kutokana na taarifa zinazowasilishwa na idara ya madini mkoa.

“Hili jambo ni complicated (gumu) kidogo. Unajua sisi ni vigumu kuwafahamu wanafanyabiashara wa madini bila kutambuliwa na ofisi ya madini. Hapa pana uzembe unafanywa na watu wa madini.

“Kuhusu wafanyabiashara wa madini wanaotumia leseni za watu wengine ndio nasikia, lakini suala la madini tumewahi kulizungumza kwa kina na Mkuu wa Mkoa na tukatengeneza mpaka mpango mkakati.

“Kuna aina ya madini mfano Tanzanite na spinel ni ngumu kubaini mtu anapokuwa nayo, mpaka Rais John Magufuli amefikia hatua ya kufuatilia kwa karibu sababu ya nature ya madini ilivyo. Spinel ikichukuliwa ni vigumu kuijua,” amesema Shirima.

Shirima amesema utoroshwaji wa madini umekuwa ukiingizia nchi hasara na umekuwa ukifanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu, huku akisisitiza kwamba idara ya madini ndiyo yenye jukumu la kutoa taarifa za mapato TRA ili kodi iweze kulipwa.

“Tatizo lililopo ni baadhi ya wafanyabiashara kujisajili nje ya Mkoa wa Morogoro hivyo hata ukiingia kwenye mfumo wa kodi unaona wanalipa kodi wakati wamepata madini huku na hawajayalipia kodi,” amesema.

Ofisi ya madini Morogoro

JAMHURI limefanya mahojiano na Afisa Madini Mkoa wa Morogoro Bertha Luzabiko kuhusina na uchimbaji na utorishwaji wa madini ya spinel wilayani Ulanga lakini amehoji taarifa hizo zimepatikana wapi na imekuwaje mpaka gazeti la JAMHURI kufika katika migodi iliyoko Epanko.

Luzabiko ameshangazwa na gazeti hili kufahamu uchimbaji wa Spinel Epanko na kwamba ni jambo lisilofahamika kwa Watanzania wengi.

Amesema kulingana na sheria ya madini wafanyabiashara wote hupewa leseni ya biashara ya madini kwa mwaka mara moja tu na kwamba mwaka jana hakuna mfanyabiashara yeyote aliyepewa leseni ya ununuzi wa madini mkoani humo.

Alipoulizwa kama hakuna leseni iliyotolewa mbona kumekuwepo na raia wa kigeni kutoka Sir-Lanka ambao wamekuwa wakinunua madini mpaka Machi mwaka huu, amejibu kuwa raia hao wa kigeni alishawafukuza Mahenge tangu Disemba mwaka jana.

“Wafanyabiashara wa kisirlanka niliwaambia watoke Epanko na Mahenge, wasifanye biashara yoyote kwa sababu hawana leseni tangu Disemba mwaka jana. Kama bado wapo na wanaendelea na biashara basi wanafanya makosa, itanilazimu kuwafuatilia,” amesema Luzabiko.

Alipoulizwa kuhusiana na uchimbaji na upatikanaji wa madini ikiwa ni pamoja na utoroshwaji wa madini unaofanywa na wafanyabiashara amesema kuwa ofisi yake imekuwa ikikusanya mirabaha na wafanyabiashara hao wanatakiwa kwenda ofisini kwake sio kuwafuata.

“Wanajileta wenyewe kusema wamepata nini, changamoto ni kwamba hatujui wanzalisha kiasi gani na hata wakizalisha ni mpaka tusikie kutoka kwa watu na muda unakuwa umeshapita. Mwaka jana walizalisha nilipata taarifa kwa kufanya uchunguzi ndipo nikambana Franone akanambia amepata madini kidogo ya million 43tu hivyo akalipa kodi Sh milioni 2 tu. Na hapa ni baada ya kumbana,” amesema Luzabiko.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za madini hayo kutoroshwa na kupelekwa Mkoani Arusha amesema   ni kweli madini hayo yamekuwa yakipelekwa Arusha, huku akisisitiza kwamba ni kipindi kirefu wafanyabiashara wa Arusha wamekuwa wakichimba Epanko.

Luzabiko amebainisha kwamba mwaka 2014/15 kampuni ya Franone  ilizalisha mawe mengi lakini walipobanwa na maafisa madini walisema kwamba walizalisha madini yenye thamani ya shilingi milioni 200 tu hivyo akatakiwa kulipa kodi ya Sh milioni 10.

“Kuna uwezekano mkubwa sana wa kudanganywa na wafanyabiashara kwani hatujui kinachozalishwa. Wakishabeba madini hayo kwenye magari yao kutoka huko Epanko hawasimami popote unakuja kusikia baada ya wiki mbili mpaka tatu kuwa madini yalichukuliwa kwenda Arusha,” amesema Luzabiko.

Luzabiko ameliambia JAMHURI kuwa mfanyabiashara Salim Almas, Disemba mwaka jana alipeleka madini aliyoyapata katika ofisi za kanda yaliyokuwa na thamani ya Sh milioni 80 tu na alilipa kodi ya Sh milioni 4.8.

“Mpaka sasa najiuliza ilikuwaje akajileta mwenyewe, sijui ilikuwaje mpaka akanambia kuwa amepata madini. Ingawa siwezi kuwa na uhakika kama alipeleka kiasi chote alichopata kwenyed ofisi za kanda,” amesema.

Kuhusu wanunuzi wa kigeni kufika Mahenge na kununua madini bila serikali kuwa na taarifa amesema kwamba taarifa hizo alishazisikia na kwamba aliwafuatilia lakini hakuwapata.

“Unajua kuna mambo mengi ya kushangaza kwenye mambo ya madini. Kuna madini yalipatikana mwaka 2007 ambayo yanaelezwa kuvunja rekodi lakini hapa ofisini kwangu hakuna taarifa zake kabisa na haijulikani kama yalilipiwa kodi. Hapa ndipo utakapoona nilivyo na kazi ngumu sana,” amesema.

Mkuu wa Mkoa Morogoro

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Steven Kebwe amesema suala la Mahenge ni la miaka mingi na linafahamika.

“Tuligundua wapo wachimbaji wadogo zaidi ya 3000, waliosajiliwa ni 78 tu, lakini wanaolipa kodi ni 4 tu ndipo tukaanzisha utaratibu wa kuwasajili na mimi niliwapa kazi hiyo tangu mwaka jana,” amesema Dk.Kebwe.

Akizungumzia maafisa madini amesema kwamba katika wilaya zote saba za mkoa zilizopo hakuna maafisa madini, jambo ambalo ni changamoto.

Amesema kwamba Mahenge ndiyo eneo lenye madini ya vito kwa mkoa wote wa Morogoro lakini mhandisi wa madini yuko mkoani tu hivyo serikali kujikuta ikipoteza mapato.

“Tulishazungumza na wenzetu wa madini tushirikiane, hili suala si mara ya kwanza kutokea walishaandika sana wenzunu kuhusu kutoroshwa madini lakini suala hili lipo wizarani. Mkoa unalifahamu, wizara na serikali kwa ujumla. Suala hili ni serious,” amesema Dk. Kebwe.

Kuhusu wafanyabiashara wa kigeni kuwepo mahenge Dk. Kebwe amesema ofisi yake itafuatilia suala hilo na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.

“Hawa watu nilisikia kuwa walikuwa na kesi kutokana na wizi pia kupatikana na fedha ambazo hawakutakiwa kuwa nazo. Nitawasiliana na afisa madini na watu wa TRA nione wamefikia wapi sababu safari tumeshaianza ili tuone tumefikia wapi,” amesema Dk. Kebwe.

1296 Total Views 5 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!