Wiki iliyopita mjadala mzito uliotawala hapa nchini, ni taarifa au tuhuma zilizoibuliwa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa. Mchungaji Msigwa amemtuhumu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kuwa anasafirisha pembe za tembo nje ya nchi.

Msigwa anasema Kinana anasafirisha pembe hizo kupitia kampuni yake ya kusafirisha mizigo nje ya nchi iitwayo Sharaf Shipping Agency. Kwamba pembe  hizo zilikamatwa nchini China zikiwa safarini kuelekea Hong Kong. Hakika baada ya kauli hii, Msigwa amechafua hali ya hewa.

 

Nguvu iliyotumiwa na Serikali na wabunge wa CCM kumsafisha Kinana imeacha maswali mengi kuliko majibu. Imeamsha mijadala vijiweni, na mjadala mmoja nilioukuta Banana, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ndiyo ulioniacha hoi. Mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo alisema hivi: “Si Kinana, ni Msomali na Wasomali ndiyo wanaomaliza tembo wetu?”

 

Ikumbukwe fikra kama hizi zinakuja kutokana na ukweli kwamba ilipofanyika “Operesheni Uhai” mwaka 1989 kusafisha majangili, asilimia kubwa ya watuhumiwa waliokamatwa, kufurushwa au kuuawa ilithibitika kuwa walikuwa na asili ya Kisomali. Mimi sitaki kulizungumzia hili la Usomali wa Kinana, kwani wajihi na matendo ni vitu viwili tofauti.

 

Sitanii, nimeandika makala haya kutokana na utetezi dhaifu uliowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher ole Sendeka, na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, wote hawa wakimtetea Kinana. Orodha ni ndefu wengine nitawaacha maana nao wameingia mkondo huo huo.

 

Sendeka alieleza kushangazwa kuwa kambi ya upinzani bungeni inageuza makosa ya kampuni kuwa makosa ya mmliki. “Ni kama leo unakwenda katika ukumbi wa Bilicanas, unakwenda chooni na kumkuta mvulana anavuta bangi, huwezi kumshtaki Mbowe (Mbunge wa Hai-Chadema), unashughulika na mhalifu,” alisema.

 

Kagasheki naye alitumia mfano sawa na Sendeka, ila akatumia Shirika la Ndege la Precision.

 

Nchimbi yeye alisema: “Kampuni ya Shipping Agency duniani kote ni kumwakilisha mwenye meli, agenti hawezi kuwa mwenye meli ila anamwakilisha mwenye mali, kuna shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye meli.

 

“Kuna mambo ya kuhudumia watumishi kwenye meli, kuwapelekea chakula watumishi, kufanya usafi, kuwapelekea mahitaji muhimu lakini wapo watu wanaofanya ‘clearing and forwarding’ na  Kiswahili chake ni kupeleka na kutoa.

 

“Hawa ndiyo wanaopeleka mizigo bandarini na kule ndiko kwenye utaratibu wa upekuzi, kwa hiyo, huko hahusiki mtu wa shipping agency. Sina mashaka hata kidogo kuwa Mchungaji Msigwa analijua hili ila amelifumbia macho kwa makusudi na kwa maslahi yasiyokubalika kwa taifa,” alisema.

 

Nchimbi aliwataja watuhumiwa waliohusika na pembe hizo za tembo kuwa ni Eradius Tesha, Shaban Abura, Eric, Issa Abubakar na Omar Hussein. “Mheshimiwa Spika, hawa ndiyo waliopelekwa mahakamani na uchunguzi ulijidhihirisha kuwa hawa ndiyo watuhumiwa wa kesi hiyo na kambi ya upinzani inalijua hili,” alisema.

 

Nchimbi ameongeza kuwa wakati kesi iko Kisutu, ulihitajika ushahidi kutoka nchini Vietnam, na nchi hiyo imesema haina ushirikiano na Tanzania katika mambo ya jinai. “Hivi sasa tunazungumza na Ubalozi wa China utupe kibali cha kufanya upelelezi ili kesi hiyo iweze kuendelea, na kwa msingi huo Mahakama ya Kisutu inataka ushahidi huo ili kesi iendelee na hili wapinzani wanalijua,” alisema.

 

Sitanii, Kinana kwa upande wake amekaririwa akisema: “Lakini mimi sina nafasi yoyote ya kiutendaji na wala sishughuliki na uendeshaji wa kampuni hiyo. Kwa kweli sikujua na wala sikuhusika kwa namna yoyote ile na usafirishaji wa makontena hayo na mengine yoyote,” alisema Kinana.

 

Alisema anachojua yeye ni kwamba, maofisa wa kampuni hiyo waliuliza na kuambiwa kuwa shehena iliyokuwa katika makontena hayo ni plastiki zilizotumika. Alifafanua kuwa wenye wajibu na mamlaka ya kukagua shehena zote zinazosafirishwa nje ya nchi ni mamlaka za serikali na si kampuni ya uwakala wa meli.

 

Sitanii, ukisoma maelezo ya viongozi hawa kuna kitu wasichokisema. Ni kweli wote wanasema si kazi ya kampuni hii kukagua mizigo. Ni kweli wote wanasema zipo mamlaka zenye jukumu la kukagua mizigo, ila wanachonisikitisha ni kutotaja wazi ni nani huyo mwenye mamlaka ya kukagua mizigo aliyeliangusha taifa letu na kulitia aibu kwa ujangili huu.

 

Ninavyofahamu katika eneo nyeti kama la bandari, mizigo inayofungwa kwenye makontena inapaswa kukaguliwa na mamlaka nyingi. Idara ya Uhamiaji, Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Usalama wa Taifa, Wizara ya Viwanda na Biashara na kwa nchi makini mwakilishi wa Wizara ya Fedha.

 

Bandarini ni mahala salama, lakini pa hatari mno. Ukiruhusu vitu kupitishwa hovyo hovyo bila ukaguzi wa kina, basi ujue fika kuwa ipo hatari kubwa kama nitakayoitaja hapa chini. Kinana, kwa upande wake, anasema watu wake waliuliza wakaambiwa kuwa ni plastiki zilizotumika.

 

Sitanii, najua Kinana hatanichukia kwa kulisema hili, kama mkurugenzi wa kampuni hii anao wajibu kisheria kufahamu kampuni yake inafanya biashara gani na kwa utaratibu upi. Ndiyo maana kuna Bodi ya Wakurugenzi. Zamani ilikuwa kampuni zinafanya makosa wakurugenzi wanaachiwa hivi hivi, lakini mambo yamebadilika.

 

Nchini Marekani, kampuni zilikuwa zikijiendesha kwa utaratibu huu. Mwaka 2001 kampuni kubwa ya kuzalisha umeme Enron ilifilisika na kuwatia hasara ya dola bilioni 11 wanahisa. Kampuni hii iliyokuwa na mali zenye thamani ya dola bilioni 63, isipokuwa ilikuwa ikidanganya mizania yake ya hesabu kuonesha inatengeneza faida katika miradi ambayo wakati mwingine haiifanyi.

 

Baada ya hasara hiyo ya mwaka, mwaka uliofuata 2002 ilitungwa sheria ya uhasibu iitwayo Sarbanes Oxley Act of 2002. Sheria hii iliwasilishwa bungeni na wabunge binafsi; Seneta Paul Sarbanes na Mwakilishi Michael G. Oxley. Kwa heshima yao sheria hii ikaitwa Sarbanes-Oxley. Ilibadili mchezo wa uendeshaji wa kampuni.

 

Sheria hii ilifanya kazi ‘retrospectively’ (kwa kushughulikia makosa yaliyotendeka kabla ya kutungwa kwake), ambapo wakurugenzi wa kampuni ya Enron walifungwa jela na kampuni ya uhasibu ya ukaguzi wa hesabu ilihukumiwa adhabu kali. Tangu wakati huo, nchi karibu zote duniani zimebadili sheria zake, tukiwamo sisi kwa kuwataka wakurugenzi wa kampuni au mashirika kusaini hesabu za mashirika, kwa nia ya kuthibitisha kuwa taarifa ndani ya shirika wanalosimamia au kumiliki ni za kweli.

 

Sitanii, Sendeka anatuona sote katika taifa hili ni mambumbumbu. Kwamba katika sheria tuko sifuri. Anataka kutuaminisha kuwa sheria haijabadilika na hivyo Kinana ajifiche katika kinachoitwa corporate veil (kinga ya kikampuni). Nasema hapana. Ikiwa Sendeka analijua hilo, basi alipaswa kulijua na hili pia linaloitwa vicarious responsibility (uwajibikaji wa kiuwakilishi).

 

Naomba nirahisishe lugha kidogo hapa ili niweze kueleweka. Ninaposema uwajibikaji wa kiuwakilishi ni sawa na mtu anayemiliki gari au pikipiki. Dereva akikutwa anaendesha gari, pikipiki au baiskeli isiyo na bima; hati ya njia au tairi kipara; mmiliki anawajibika moja kwa moja kwa makosa hayo. Mfano huu ukiuhamishia kwenye kampuni unapata jibu.

 

Kinana hawezi kutwambia kuwa kampuni yake hata kama ingeingiza bunduki nchini haoni sababu ya kuuliza kwa sababu vyombo vya dola vipo vyenye wajibu huo. Watumishi ndani ya kampuni wanafanya kazi kwa niaba ya mmiliki. Ni kwa mantiki hiyo makosa wanayoyatenda yanachukuliwa kuwa na baraka za mmiliki.

 

Kwamba leo Mbowe ikikutwa Bilicanas vijana wanavutia bangi au dawa za kulevya chooni, na wafanyakazi wa Bilcanas wasiwazuie, ni wazi kisheria chini ya vicarious responsibility, Freeman atawajibika moja kwa moja. Hivyo, kwangu maelezo yoyote yanayotaka kumwondoa Kinana katika kadhia hii hayakubaliki.

 

Sitanii, kiungwana Kinana anaweza kufanya moja kati ya mawili baada ya kumkumbusha mfano huu. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alijiuzulu. Alijiuzulu si kwa sababu ‘alipiga dili’ katika sakata la Richmond, la hasha, bali kwa sababu wasaidizi wake walibainika kushiriki kadhia hii. Hili ndilo alilosema Dk. Harrison Mwakyembe.

 

Lowassa naye alipotua Monduli na kupokewa na maelfu ya watu, alisema hivi: “Hili suala lina mambo mengi ajabu. Hivi wewe Waziri Mkuu unamwita Waziri (wa Nishati na Madini Dk. Ibrahim Msabaha) unamwambia tukutane ofisini saa 12:30 asubuhi, anasema ‘nitakuja mzee’. Unakaa saa 2, hajafika, unampigia tena simu anasema ‘Nakuja’, unakaa saa tano, tisa, 12 jioni humuoni. Unajiuliza huyu waziri anapata wapi nguvu hii?”

 

Ukiyapima vyema maneno ya Lowassa, unabaini jinsi wasaidizi wake walivyotenda ndivyo sivyo. Ila aliwajibika. Akajiuzulu. Huu ndiyo uungwana. Kinana ikikupendeza, unaweza kuiga mfano huu, au la kama ni mgumu, unaweza ukajitokeza hadharani, ukatuomba radhi Watanzania kwa kampuni yako kutumika vibaya. Ukisema neno ‘samahani’ tu au ‘kunradhi’, Watanzania tutakusamehe na kuendelea kukupima kama hakika umejutia makosa yako au unaendelea na kamchezo.

 

Bila Kinana kufanya moja kati ya hayo, ni wazi kuwa wananchi wataendelea milele kuamini kuwa alikuwa sehehmu ya mchezo huu, na ndiyo maana ruhusa ya kupata mashahidi kutoka Vietnam haipatikani. Kinana pima uzito, kwa pamoja tushirikiane kulinda tembo wetu wanaoteketea nchini.

 

1247 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!