Watanzania tunakinyanyasa, tunakibeua Kiswahihi – 6

Katika makala iliyotangulia niliwagusa baadhi ya Waswahili wanaokinyanyasa Kiswahili, wakiwamo wabunge na wanasiasa. Leo nawatupia macho wafanyakazi katika taasisi na asasi mbalimbali ambazo watendaji wake ndiyo wanaokibeua Kiswahili.

Walimu wa shule za msingi hadi vyuo vikuu, waandishi wa habari, watangazaji wa redio na runinga, na hata watunzi na waandishi wa vitabu nao wameanza kukibeua na kukiharibu Kiswahili.

 

Nimetaja makundi hayo kwa sababu ndiyo wahusika wakubwa katika kufundisha elimu yoyote, kuhabarisha taarifa zozote, kuunda matangazo, kutunga nyimbo na misamiati mipya kutokana na lugha kaya, maskani n.k.

 

Wote hao ni walimu na watunzi wa lugha ya Kiswahili. Lakini, la ajabu na la kushangaza walimu hao, wako katika kundi la wanaokinyanyasa na kukibeua Kiswahili katika maandishi, mazungumzo na simulizi zao.

 

Kwa mfano, mwandishi wa gazeti moja la udaku toleo Na. 1004 la Mei 1-3, 2013 ameandika; “Katika purukushani baba Asha alimpa kibano mwizi wake hadi akamchana usoni na kumng’oa meno ya mbele, jambo lililosababisha kutokwa na damu nyingi.”

 

Kisanifu, ujumbe umepotoshwa kwa kutumia visivyo neno ‘purukushani’.  Purukushani maana yake ni hali ya kujitia hamnazo; hali ya kudharau jambo kwa kusingizia kutosikia, kutoelewa au kutokuwa na habari; hamnazo, mwapuza. (Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la pili-TUKI)

 

Je, kwa maana ya neno hilo, baba Asha alikuwa hamnazo au alikuwa anafanya dharau alipompa kibano mwizi wake hadi kumchana uso na kumng’oa meno ya mbele na kutokwa damu?

 

Kwa mtazamo wangu, maandishi ya neno purukushani ni vurugu, vurumai au kukurukakara. Hiyo si sahihi. Amekosea na anakibananga na kukibeua Kiswahili. Si yeye tu, wapo wengi katika tasnia hii ya habari wanaotumia visivyo neno purukushani.

 

Mara kadhaa kwenye magazeti, redio na runinga tunasikia na kusoma habari mbalimbali zenye matumizi yasio sahihi ya neno purukushani. Kwa mfano, majambazi wawili wameuawa katika “purukushani” za kurushiana risasi na polisi.

 

Swali: Polisi na majambazi walikuwa hamnazo, au upande mmoja ulikuwa ukidharau upande mwingine, au wote walikuwa hawana habari kwamba walikuwa wakirushiana risasi?

 

Aidha, tumepata kusikia au kusoma kwenye vyombo vya habari maneno kama sindano za ‘masaa’. Saa haina wingi kama neno wakati – nyakati.

 

Watu nane (badala ya kusema watu wanane). Maneno kama hayo yanapotumika kwa makusudi kwa dhamira ya kuiga kabila fulani, au kufanya mbwembwe hata pengine dhihaka, ndipo wanapokibananga Kiswahili.

 

Maneno kama hayo na mengine ya aina hiyo, ukweli yamekera masikio na kutia kichefuchefu yanapotamkwa.

 

Inakuwaje mtangazaji mwenye kipindi maridhawa redioni au katika runinga kukazania kusema – wababa, wamama, wadada na wakaka muwe waaminifu katika ndoa zetu. Badala ya kutumia Kiswahili sanifu na kusema akinababa, akina mama, madada na makaka muwe waaminifu katika ndoa zenu.

 

Kiswahili sanifu hakina wababa, wamama, wadada na wakaka. Kutamka hivyo ni kuharibu lugha kwa makusudi na kukataa kufuata utaratibu na utamaduni wa lugha ya Kiswahili.

 

Katika Kiswahili sanifu hakuna neno ‘dhumuni, dhehebu, dhabahu wala neno dhubuti. Kuna maneno madhumuni, madhehebu, madhabahu na madhubuti. Ndivyo yalivyo, hayana umoja kama neno dhambi wingi wake ni madhambi, dhalimu wingi wake ni madhalimu.

 

Watumizi wa lugha ya Kiswahili ambao pia hutumia lugha ya kigeni, hasa hawa Waswahili wenyewe, wako radhi kuvunja utamaduni wa lugha ya Kiswahili, lakini hawako radhi na wanaheshimu utamaduni wa lugha ya kigeni. Huu ni ulimbukeni wa lugha.

 

Mtumiaji Kiswahili huona raha kutamka neno dhehebu badala ya kutamka madhehebu. Lakini hayuko radhi kutamka neno ‘sheeps’ la kigeni, badala ya ‘sheep’. Utamaduni wa lugha ya kigeni neno ‘sheeps’ ni hilo hilo katika umoja na wingi. Hilo analizingatia sana.

 

Hayuko tayari kuzingatia neno madhehebu au madhumuni kuyatumia kama yalivyo katika umoja na wingi. Anachofanya ni kuvunja utamaduni wa lugha ya Kiswahili na kulipa umoja neno dhehebu, dhumuni n.k. Jambo ambalo si sahihi.

 

Kwa leo nakamilisha makala haya kwa shairi la K.H. Akilimali alilolitoa katika kikao cha pili cha mwezi cha Jumuiya ya Taaluma ya Kiswahili Tanganyika, tarehe 3 Oktoba, 1953 Tangamano, mjini Tanga.

 

Tamu njema ya asali, mtumia lugha yake,

Asemapo kiasili, maneno yafikirike,

Waone kama asali, wengine waitumike,

Lugha kama Kiswahili, milele itumike.

Mjinga wa kutumia, lugha ambayo si yake,

Hapati kujikunjua, na hana faraja zake,

Lugha nyingine udhia, katu haishi makeke,

Ingawa inatumiwa, wachache mahaba yake.

 

Itaendelea…

 

Please follow and like us:
Pin Share