Polisi, Sumatra wanalea mawakala matapeli stendi ya mabasi Nyegezi  Ukifika kituo cha mabasi cha Nyegezi jijini Mwanza, huwezi kupinga malalamiko kuwa rushwa imenunua utendaji wa maofisa wa Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

Siku hizi Nyegezi, pengine ndipo mahali pekee nchini ambapo baadhi ya mawakala wa mabasi ya abiria wameota makucha ya kuwanyanyasa wasafiri kwa kadiri wanavyotaka!

Kituo hicho kimekithiri mawakala wa mabasi wasio waaminifu. Wanawatapeli wasafiri mchana kweupe kwa kuwakatia tiketi za mabasi ambayo hayasafiri.

Mfano, Mei 4, mwaka huu, watu zaidi ya 60 nikiwamo mimi, tulikata tiketi kwa ajili ya kusafiri kwa kutumia basi la Happy Nation Express kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam siku inayofuta.

Cha kushangaza, tulipofika stendi ya Nyegezi siku ya safari (Mei 5, 2013) kuanzia saa 11 alfajiri tulitafuta basi la Happy Nation Express bila mafanikio. Halikuwapo stendi!

Baada ya kulitafuta basi hilo huku na kule bila mafanikio, tulitumia namba za kwenye tiketi zetu kupiga simu kwa mawakala husika kuuliza lilipo, ndipo tukaambiwa kuna dharura imetokea, hivyo tutatumia basi jingine kusafiria.

Baadaye wengi wetu kwa juhudi zetu binafsi za kuuliza hapa na pale, tulikutana na wapigadebe wakatuonesha basi la Princes-Shabaha kuwa ndilo tutakalotumia kusafiria badala ya Happy Nation Express.

Kuna taarifa kuwa watu kadhaa hawakufanikiwa kutumia basi la Princes-Shababa, hivyo walivurugiwa safari zao na kupata usumbufu wa kudai nauli zao.

Kwa hakika, wengi tulipata usumbufu mkubwa huku tukijiuliza sababu za mawakala husika kushindwa kutujulisha mapema dharura iliyojitokeza kupitia namba za simu zetu tulizoacha ofisini kwao.

Lakini nilifanya juhudi za kudadisi mwenendo wa utendaji kazi wa mawakala wa mabasi ya abiria katika kituo cha Nyegezi, na kubaini kuwa baadhi yao wamejikita katika kuwatapeli na kuwadhulumu wasafiri nauli.

Mfanyabiashara mwenye duka katika stendi hiyo alinidokeza kuwa ni kawaida ya baadhi ya mawakala kutumia majina na picha za mabasi fulani fulani likiwamo la Happy Nation Express kuuza tiketi kwa wasafiri huku wakijua hayana ratiba za safari husika.

Inaelezwa kwamba wasafiri wengi wamekuwa ‘wakilizwa’ na mawakala hao mara kwa mara kwa kudhulumiwa nauli, kuvurugiwa ratiba za safari na kulazimishwa kutumia mabasi ambayo hayakuwa chaguo lao.

 

Kadhalika, kuna kasumba ya mawakala kuwalipisha wasafiri viwango tofauti vya nauli kwa basi moja. Mfano, siku hiyo katika basi la Happy Nation Express baadhi ya walilipishwa nauli ya Sh 50,000, wengine Sh 45,000 na kuna waliolipa Sh 38,000.

Inashangaza kuwa vitendo hivyo vya mawakala wasio waaminifu, vinafanyika huku vyombo vyenye dhamana ya kuvidhibiti — Jeshi la Polisi na Sumatra — vikiwa kimya.

Askari polisi wa kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri na abiria barabarani (trafiki), wanaonekana kwa idadi kubwa katika stendi ya mabasi ya Nyegezi, lakini hawashughulikii kero zinazosababishwa na mawakala wa mabasi dhidi ya abiria.

Sasa basi, katika hali kama hiyo, ni nani mwenye roho ngumu atakayepata ujasiri wa kuwatetea trafiki na Sumatra, kwamba hawajawekwa ‘mifukoni’ mwa mawakala matapeli kituoni hapo? Hayupo.

Mwaka jana, Jeshi la Polisi lilizindua kwa mbwembwe kubwa ubandikaji wa namba za simu za mkononi za wakuu wa vikosi vya trafiki ndani ya mabasi katika stendi ya Nyegezi, lakini makondakta na madereva wa mabasi husika wameshazibandua.

Ubandikaji wa namba hizo ndani ya mabasi, ulilenga kuwasaidia abiria kuwasiliana na kitengo cha trafiki pale wanapoona madereva na makondakta wanawatendea ndivyo sivyo katika huduma ya usafiri.

Trafiki wanajua na kuona kwamba namba zao zimebanduliwa ndani ya mabasi hayo lakini hawajachukua hatua zozote. Hawajawakamata, hawajawahoji wala kuwatoza faini madereva na makondakta kwa makosa ya kuzibandua na kukaidi agizo halali la Polisi na Serikali kwa jumla.

Leo wasafiri wananyanyaswa kwa namna mbalimbali katika stendi ya Nyegezi. Hawana pa kukimbilia kuomba msaada licha ya kituo hicho kuzingirwa na ‘utitiri’ wa trafiki!

Tunapofikia hatua ya Jeshi la Polisi na Sumatra kushindwa kudhibiti kero zinazoendekezwa na mawakala matapeli dhidi ya abiria, tunakosa imani kwa vyombo hivyo na Serikali kwa jumla.

Ndiyo maana hata mimi sioni sababu ya kupuuza malalamiko yanayotolewa na watu wengi kwamba Polisi na Sumatra ‘wamepofushwa’ macho na mawakala matapeli katika stendi ya Nyegezi. Inatisha!

 

Please follow and like us:
Pin Share