Ndani ya Dk. Magufuli namuona Mwl Nyerere

MAGUFULINimepata muda wa kukaa na Dk. John Magufuli, kwa nyakati mbalimbali tangu akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi hadi sasa anapowania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwanasiasa huyu anayepewa nafasi kubwa ya kushinda kiti cha urais, ni mfuasi mzuri sana wa fikra za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa yeyote anayekaa na Dk. Magufuli, ni nadra mno kumaliza nusu saa ya mazungumzo bila kumsikia akilitaja kwa mazuri jina la Mwalimu Nyerere.

Kwake yeye, Mwalimu ni role model wake kisiasa na kiutendaji kazi. Ni kwa sababu huyo, Dk. Magufuli anatajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaopenda kusoma maandiko na kusikiliza hotuba za Mwalimu Nyerere, kwa kiwango cha juu kabisa.

Mapenzi ya Dk. Magufuli kwa Mwalimu Nyerere yalianza kudhihirika pale alipoamua kukamilisha ujenzi wa uzio wa nyumba ya Mwalimu pale Msasani. Wakati huo mimi nilikuwa katika Idara ya Ugavi wizarani hapo.

Watu walio karibu na familia ya Mwalimu Nyerere wanasema miaka kadhaa baada ya kifo cha mwasisi huyo wa Taifa, Mama Maria alianza kujenga uzio kuzunguka makazi ya Msasani kwa kutumia fedha zake. Mama Maria hakuweza kukamilisha kazi hiyo baada ya kuishiwa fedha. Hatua hiyo inaelezwa kumsikitisha sana Dk. Magufuli, na akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alihakikisha zinapatikana fedha za kukamilisha kazi hiyo.

Kama ilivyo ada yake, Dk. Magufuli alisimamia mpango huo hadi mwisho na kumwezesha Mama Maria kupata uzio ambao unasaidia masuala ya ulinzi pale nyumbani Msasani.

Kana kwamba hilo halitoshi, Dk. Magufuli, aliingilia na kusaidia kurejeshwa kwa kiwanja kilicho mbele ya makazi ya Mwalimu Nyerere pale Msasani.

Kiwanja hicho kilikuwa kimetwaliwa na mfanyabiashara wa matofali na kujimilikisha. Ikumbukwe kuwa sehemu hiyo iliachwa wazi kwa matumizi ya wananchi, hasa vijana kwa ajili ya michezo.

Mfanyabiashara huyo, akitumia jeuri ya fedha, alijimilikisha kiwanja hicho na kuamua kukitumia kwa ajili ya ufyatuaji matofali ya biashara. Akajenga vyoo, ofisi na hata akapata huduma za umeme na nyingine.

Dk. Magufuli baada ya kufuatilia ukweli wa mambo alibaini kuwa mfanyabiashara yule hakuwa na haki ya kulitumia eneo hilo. Akampatia notisi ya kuhama, lakini akakaidi. Ndipo Dk. Magufuli, kwa mamlaka aliyopewa kisheria, akaamuru mfanyabiashara aondolewe kwa nguvu. Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Jiji na Wizara, walihakikisha operesheni ya kumwondoa mvamizi huyo inaanza saa 9 usiku, na ilipofika saa 1 asubuhi uwanja ukawa mweupe.

Tukio hilo liliungwa mkono na wananchi wengi ambao walitambua ubabe wa mfanyabiashara aliyeingia kwenye eneo la Mwalimu kinyume cha sheria.

Kwa hakika ulikuwa ni uamuzi sahihi wa Dk. Magufuli, kwa ajili ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Lakini ni kipindi hicho hicho ambacho Mama Maria alikuwa amepokwa kiwanja chake pekee katika Jiji la Dar es Salaam kilichopo Mikocheni karibu na nyumbani kwa Dk. Kairuki. Baada ya taarifa zake kuandikwa mara kadhaa kwenye vyombo vya habari, Rais Benjamin Mkapa, kwa mamlaka aliyokuwa nayo kisheria alifuatilia suala hilo na kubaini kuwa ni kweli mmiliki halali ni Mama Maria kwani alikuwa na nyaraka zote za umiliki.

Dk. Magufuli, hakuishia Dar es Salaam pekee, bali itakumbukwa kuwa akiwa Waziri wa Ujenzi alihakikisha anajenga barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 11.5 kutoka Kyabakari hadi Butiama.

Hapa ni vema ikakumbukwa kuwa hadi Mwalimu anafariki dunia mwaka 1999 Butiama haikuwa hata na mita moja ya lami! Mwalimu hakuwa kiongozi wa kujipendelea kama walivyo wengi hii leo.

Watu wote walioshiriki msiba wa Mwalimu walipigwa butwaa kuona hadi kiongozi huyo anaondoka duniani, nyumbani kwake hapakuwa na kipande cha barabara ya lami.

Dk. Magufuli, kwa kutambua heshima na mchango mkubwa wa Baba wa Taifa, akahakikisha zinajengwa kilometa hizo za lami ili kuwawezesha wageni wanaozuru Butiama japo kuepuka usumbufu wa barabara mbovu.

Kwa maneno mengine ni kwamba endapo binadamu wangekuwa wanafufuka, na kama ingemtokea hivyo Mwalimu Nyerere leo, bila shaka angestajabu kuiona lami kijijini Butiama, na ni wazi angemtambua na kumsifu Dk. Magufuli kwa msaada huo.

Lakini ni wakati huu huu wa Dk. Magufuli, akiwa Waziri wa Ujenzi, alipohakikisha Serikali inaanza ujenzi wa Barabara ya Mto wa Mbu – Loliondo – Mugumu – Butiama – Makutano. Pamoja na vikwazo vya hapa na pale kuhusu barabara hiyo kwa kipande kidogo kinachopita ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), msimamo wa Dk. Magufuli, ni kuhakikisha kuwa barabara hiyo inajengwa na kukamilika.

Ukiyatafakari haya yote, unaona kabisa namna Dk. Magufuli alivyo na mapenzi ya dhati kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Binadamu hupenda kufanya mambo ili waonekane mbele ya hao wanaowafanyia. Bahati nzuri ni kuwa Dk. Magufuli, ameyafanya haya na mengine mengi mazuri, Mwalimu Nyerere mwenyewe akiwa hayupo duniani. Kwa maneno mengine ni kwamba ameyafanya haya, si kwa kujipendekeza, au kutafuta fadhila, bali ni kwa kuonyesha namna alivyomheshimu na anavyoendelea kuheshimu mchango mkubwa wa Baba wa Taifa katika ujenzi wa nchi yetu.

Wala Dk. Magufuli hakufanya haya ili siku moja aje kuwa mgombea urais ambaye ataketi kwenye kiti na katika ofisi ambayo ilitumiwa na Mwalimu Nyerere, yaani Ikulu.

Mtu yeyote anayefuata nyayo za mtu fulani anayependezwa naye, mtu huyo anathibitisha kwa vitendo, na si kwa nadharia mapenzi yake kwa huyo anayemuiga.

Mwalimu Nyerere, anabaki kuwa kiongozi wa pekee katika Tanzania, Afrika na ulimwengu. Anabaki kuwa na sifa ya utu na mpenda maendeleo ya jamii nzima. Hakupenda kuona watu wakinyanyaswa, wakionewa au kupuuzwa kwa sababu za unyonge wao.

Dk. Magufuli kwa kuamua kuwa mfuasi wa Mwalimu, ni matumaini yangu na wengine wengi kuwa atakuwa na tabia na hulka zinazoendana na sifa hizo.

Watanzania wanatarajia kumuona Dk. Magufuli akiendelea kuwa mchapakazi hodari, mpenda watu, msikivu na aliye tayari kuutumia muda wa maisha yake yote kuwatumikia Watanzania na walimwengu wenye mahitaji.

Ingawa anaweza asifikie umaarufu kama aliokuwa nao Baba wa Taifa, kuna dalili za wazi kuwa Dk. Magufuli atakuwa Rais wa kupigiwa mfano katika nchi yetu na katika Bara la Afrika.

Hotuba zake anazozitoa majukwaani zinaaksi hiki ninachokisema hapa. Amekuwa akizungumza namna alivyo na dhamira ya kuijenga Tanzania mpya. Amekuwa akitoa kauli zenye mwelekeo wa kukosoa dosari zilizopo sasa katika utendaji kazi wa Serikali ya sasa. Hizi ni kauli thabiti na kiongozi jasiri zinazowapa mwanga wananchi wa kuanza kuwa na shauku ya kushuhudia mabadiliko makubwa na yenye tija kwa Watanzania hasa wanyonge ambao kwa muda mrefu wameumizwa.

Matarajio ya Watanzania ni kuona Dk. Magufuli, anatenda yale anayoamini na anayowaahidi wananchi bila kuwa na kigugumizi wala kuwaonea haya watendaji wazembe, waonevu, wahujumu uchumi na wasiowajibika.

Anaposema: “Hapa ni Kazi Tu”, hakika ni kazi tu. Mapenzi yake kwa Mwalimu Nyerere ni jambo linalowapa faraja kubwa sana Watanzania ambao wameanza kurejea namna walivyofaidi upendo na utendaji kazi uliotukuka kutoka kwa mwasisi huyo wa Taifa letu.

Watanzania wameanza kuona kuwa Dk. Magufuli akiwa Rais wa Tanzania, vita dhidi ya ufisadi, wizi na aina zote za ufedhuli itakuwa imempata jemedari asiyeogopa. Kwa wagombea urais, nashindwa kuficha mapenzi yangu kwa Dk. Magufuli, na kuwaomba wapigakura waniunge mkono kuhakikisha Oktoba 25, anatapa kura nyingi zitakazomwezesha kuingia Ikulu na kuunda Serikali.

Kwa maneno mengine, ndani ya Dk. Magufuli, anaonekana Nyerere mwingine.

 

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa ni msomaji wa JAMHURI. Anapatikana kupitia simu 0789 117 972