Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema hajahongwa kiasi chochote cha fedha na wadau mbalimbali akiwamo Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, kama inavyodaiwa.

Taarifa zilizopo zinadai kwamba Mramba amehongwa Sh. bilioni 4 na Lowassa ambaye kwenye harakati za kuisaka Ikulu anaungwa mkono na vyama vinavyopigania Katiba yenye maoni ya wananchi (Ukawa).

Taarifa hizo zilithibitishwa na Mramba mwenyewe kwamba amesikia akitajwa kwamba amehongwa kiasi hicho cha fedha ili kufifisha nguvu za CCM iliyomsimamisha Dk. John Magufuli kwenye urais.

Taarifa ambazo zilimtikisa Mhandisi Mramba hadi kutoa ufafanuzi, zinadai alipewa fedha hizo Agosti 30, mwaka huu katika Hoteli ya Bahari Beach iliyopo Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari hizo, Lowassa amempatia kiasi hicho Mramba ili kuhakikisha Dk. Magufuli anakosa kura za mjini ndani katika uchaguzi uliofanyika juzi Jumapili ili kufifisha ndoto ya CCM kutawala katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Tuhuma kama hizo zimewahi kuelekezwa pia kwa aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

Wakati Mramba akizungumza hayo, JAMHURI ilifanikiwa kuzungumza na Msemaji wa Lowassa, Aboubakar Liongo, kuzungumzia taarifa hizo ambako pamoja na mambo mengine, alijibu: “Hilo jambo ni jipya kwangu na kwa bosi wangu.”

Akaendelea kusema: “Sisi hatujasikia jambo hilo na wala hatulijui. Mimi binafsi silijui wala mheshimiwa mwenyewe halijui. Kama unavyofahamu tupo katika kipindi cha kampeni…Hatuko aware (hatujui) na hizo habari kabisa na kama unavyofahamu leo tupo katika harakati za kuhitimisha kampeni zetu,” anasisitiza Liongo.

Akijibu hilo, Mramba amesema meseji hiyo ameiona na tayari amesharipoti polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili ufanyike uchunguzi mtu aliyetuma meseji hiyo akamatwe na kuhojiwa ukweli kwa aliyoyaandika.

“Labda nieleze, jamani mimi sina ugomvi na mwanasiasa yeyote, na hao ni wanasiasa tu. Mheshimiwa Lowassa sijawahi hata kukaa naye kama tulivyokaa tangu nizaliwe… na yeye akiulizwa atathibitisha hilo.

“Na hilo la kukutana naye Bahari Beach limenishangaza maana hata kwenye diary yangu nimeangalia kwamba siku hiyo ambayo naambiwa nilikutana naye ilikuwa Jumapili, na mimi ni muumini naweza kwenda kanisani,” amesema Mramba na kuongeza:

“Lakini jambo jingine; hizo shilingi bilioni 4 sijawahi kuzishika na hata nusu bilioni sijawahi kuishika, najiuliza hizo bilioni 4 nilizibeba kwenye pick-up, au niliweka kwenye akaunti? Sijui.

“Sasa huyu mtu aliyetuma taarifa hiyo naomba niseme kwamba nimeripoti jambo hilo kwenye vyombo vya dola na nashukuru wanalifanyia kazi na bila shaka mtu huyu atapatikana… naamini watamkamata athibitishe hilo kwa umma.

“Maana mambo haya huwezi kukaa tu kitandani kwako ukatunga uongo ilimradi ukawa na simu ukatunga uongo na ukatuma kwenye WhatsApp. 

“Na huwezi kunichafua kwa kiwango hiki kwa sababu utanifanya mimi kesho nikipita barabarani uwafanye  watu waseme huyo ndiye jamaa aliyepewa hela, utanifanya mimi kesho nikipita barabarani watu wajiulize kwamba huyu si jamaa aliyepewa hela? Utanifanya nipigwe mawe, kwa hiyo kwa jambo kama hili siwezi kukaa kimya itabidi vyombo vya dola vimkamate huyu mtu,” amesema Mramba.

Ameongeza kwamba si tuhuma hiyo pekee ambayo inaelekezwa kwake kwake, nyingine ni ile ambayo inaeleza kwamba kwa kuwa yeye ni Mchagga basi atakuwa Ukawa.

“Siyo hilo tu watu wamesema maneno mengi, wapo watu wanaosema kwamba huyo jamaa ni Mchagga ni Ukawa huyo jamani, sisi kimaadili taasisi kama Tanesco ni taasisi ya umma hivyo tunahudumia watu wote kwa haki bila upendeleo wowote, na hivi ninavyosema umeme umerudi Dar es Salaam na hakuna mgawo. Sasa kwa hali hii tukiuliza Dar es Salaam wanakaa watu wa chama kipi? Si wote tunakaa tu?

“Na labda kwa taarifa tu wakati umeme haupo hata mimi nilikuwa sipati umeme, na mimi kuna siku nilikuwa nawaambia watu kwamba mimi sina umeme nyumbani kwangu na niliwaambia watu wangu wasiniwekee jenereta ili siku unapokosekana na mimi nijue kwa sababu watu wengine hatuishi mbinguni tunaishi hapa hapa, kwa hiyo maneno mengine yanatia simanzi sana,” amesema Mramba.

CCM kuhujumu siasa za CCM

Kuhusu madai ya umeme kukatika katika wakati wa kampeni lakini hasa wakati wa uzinduzi wa kampeni wa Chadema, mkurugenzi huyo amesema hali hiyo ilitokea kwa karibu vyama vyote.

“Kwanza mimi nashukuru matatizo yametokea upande wa CCM na upande wa Upinzani. Kama ingetokea wakati wa kampeni za chama tawala basi ingeonekana Tanesco inakihujumu chama tawala… Hayo ni matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza wakati wa shughuli yao,” amesema Mramba.

Pamoja na hilo, amewapongeza viongozi na wanachama wa vyama vyote viwili vya siasa kutoka CCM na Upinzani kwa kulizungumzia hilo, akisema wana haki ya kuzungumza mengi.

“Siku ya uzinduzi wa kampeni za Ukawa, Tanesco tulifanya kazi kubwa kuhakikisha umeme haukatiki, ingawa tuliweka mipango mizuri, lakini tulipofuatilia tuligundua umeme ulikatika kwa kutokea kwenye laini ya Zanzibar ambako kulisababisha umeme kukatika katika maeneo mengi nchini,” amesema Mramba.

Amesema na umeme ulirudi katika saa tofauti na kwamba haukurudi baada ya kampeni kumalizika bali kilichotokea kilikuwa nje ya uwezo wao.

“Baada ya umeme kukatika, kesho yake niliunda tume ya kuangalia tatizo la kukatika kwa umeme lilitokana na jambo gani na baadaye walipata taarifa kwamba laini ya kwenda Zanzibar ndiyo iliyoleta tatizo la kukatika kwa umeme huo,” anasema.

Pamoja na mambo mengine, Mramba amesema umeme wa gesi umeingia katika kipindi kizuri hivi sasa, vinginevyo nchi ingekuwa kizani.

Amesema shughuli inaendelea kufanyika mikoani na anaamini kabla ya mwisho wa wiki hii mikoani wataona mabadiliko zaidi. Anasisitiza ndani ya muda mfupi tatizo la kukatika kwa umeme litakuwa limekwisha nchini.

“Ilitegemewa Aprili, mwaka huu bomba la gesi lingekuwa limekamilika, lakini bahati mbaya haikuwa hivyo, kwa hiyo sababu ni nyingi zilizosababisha ujenzi wa  bomba hili kuchelewa kukamilika.

“Unafahamu kwanza kitu kimoja ambacho nimejifunza katika siku za hivi karibuni ni kwamba kuna watu wana maneno mengi ya uongo na kuna watu wanatoa maneno ya uongo na kuyasambaza,” alisema na kuongeza: “Kwanza watu walisema hiyo gesi inayotoka Mtwara inayotokea ni chafu haiwezi kuzalisha umeme, lakini ukweli ni kwamba gesi ya Mtwara ndiyo bora zaidi (mitambo ya Mtwara ni ule mtambo wa Mnazi Bay na Mimbati),” amesema Mramba.

Ameeleza kwamba Serikali imenunua mitambo mipya ya kisasa kutoka Kampuni General Electric ambayo ni bora kwa kutengeneza vitu vikubwa ikiwamo mitambo ya ndege. Kwamba mtambo huo una uwezo wa kuendeshwa na watu wanne kwa kupitia teknolojia ya hali ya juu na kufanikiwa kuona kitu chochote kinachotokea mahali popote,  akitolea mfano majanga ya moto na kuuzima, kufanya mawasiliano na watu wengine.

“Kampuni ya Lama International ya Ujerumani ndiyo kampuni ya ushauri (consulting firm) na tumewafundisha wataalamu wetu mambo yote,” amesema Mhandisi Mramba.

Mhandisi Mramba ameshangazwa na hatua ya watu kuzungumza kuhusu kukatika kwa umeme nchini, akisema ingawa kunatokana na kukamilika kwa mitambo ya gesi, hilo si jambo la ajabu. 

“Namshukuru Mungu gesi imepatikana sasa, isingepatikana nchi ingekuwa kizani… Naomba Watanzania walielewe hili maana kuna watu mahodari wa kutangaza mambo ya uongo,” amesema Mhandisi Mramba.

Ameeleza kwamba kuna nchi kama vile Afrika Kusini, Zambia, Uganda, Nigeria na Ghana ambazo zina mgawo mkubwa wa umeme pamoja na kuwa na kampuni kubwa za kimataifa ambazo zinawezesha upatikanaji wa umeme, lakini kwa hapa nchini ipo  jitihada ya dhati ambayo imepatikana ya kupatikana gesi kwa ajili ya kuzalishia umema.

Kuhusu habari kwamba Tanesco imefilisika, Mramba amesema: “Si kweli. Hazina ukweli habari hizo, na kwamba hata Rais Jakaya Kikwete amezungumza hilo hivi karibuni.

“Nakumbuka Mheshimiwa Rais Kikwete alilizungumza vizuri sana sana kwamba kama tatizo la mgawo ni mabwawa kukauka ataelewa lakini si vinginevyo. Mimi naomba niseme kwamba Tanesco haijafilisika lakini hata Tanesco ingekuwa na fedha kiasi gani kama huna megawati 560 na huna jinsi ya kuzipata utafanyaje? Escom (ya Afrika Kusini) ni shirika kubwa lakini nchi yake ina mgawo mkubwa, itakuwa Tanzania!

“Sasa hivi tuna zaidi ya asilimia 40 ya Watanzania wanaoishi mjini na vijijini ambao wanatumia umeme, lakini mwaka 2005 tulikuwa na asilimia 10 ya Watanzania wanaotumia nishati hiyo,” amesema Mramba.

Mramba amewataka Watanzania kuepuka kuzungumza maneno yasiyokuwa na msingi ambayo hayana tija. 

1749 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!