Wiki iliyopita, katika mfululizo wa makala haya, mwandishi alieleza namna Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyoshirikishwa na wazee wa Dar es Salaam na Bagamoyo katika masuala mbalimbali ya kulikomboa Taifa. Alikomea kwenye maelezo ya Mwalimu alivyoumwa kichwa, lakini akapona baada ya kufuturu nyumbani kwa Mzee Ramia. Endelea.

Jamani, nilinogewa sana na stori ya Mwalimu ndiyo sababu nimeinukuu kwa kirefu. Mwalimu aliwaenzi wazee na kuwaheshimu kwa kule kumuunga mkono katika harakati za kuanzisha TANU – chama kilicholeta Uhuru wa nchi hii. Kumbe wazee tangu enzi za TANU walibweteka kwa kule kuenziwa kimaneno, lakini hawakuandaliwa utaratibu wa kupata stahili zao kimaisha.

 

Wao mradi walikutana na Mwalimu wakala naye chakula wakajiona wako sawa sawa. Kihistoria wazee waliachwa ‘solemba’. Sijui wazee wangapi tunakumbuka juu ya Umoja wa Vijana (TYL) na Umoja wa Wanawake wa TANU na ulivyoanzishwa na vijana hao hao siku zile.

 

TANU iliona umuhimu wa vijana na kina mama, ndiyo maana iliwajengea mazingira mazuri ya kuwa ndani ya Katiba ya chama na kwa utaratibu maalum. Sehemu hizo mbili za chama zina Katiba zao, zinatoa kadi maalumu kwa wanachama wake na zaidi zilipewa nafasi za upendeleo katika Bunge.

 

Hadi leo hii mapokeo yale ya nafasi za upendeleo katika Bunge zingali zinatumika kwa vyama vyote vya siasa. Enzi za chama kimoja zilikuwapo nafasi tano za upendeleo kwa vijana na nafasi kama hizo za upendeleo kwa kina mama.

 

Mapokeo haya yameingia hadi katika Serikali za Mitaa (local government) ndiyo maana kunasikika katika Halmashauri zipo fedha kutoka serikalini kwa miradi kwa vijana na kina mama.

 

Huu ni utamaduni uliojengeka katika nchi yetu na unaendelea kutumika kupitia ubunifu wa chama tawala wa siku hizo. Hakuna fedha za miradi kwa wazee na wala hakuna viti maalumu vya Bunge kwa wazee!

 

Katika Katiba ya TANU kulikuwa na mengineyo. Sura ile ya V.

FUNGU LA V: MENGINEYO: (uk. 28 Katiba ya chama) Sehemu za chama hapo zimeandikwa zifuatazo:-

Sehemu ya TANU Youth League

Sehemu ya Wanawake

Sehemu ya Wazee

Na kumetolewa maeleza mafupi tu pale.

Lakini zipo Katiba maalumu za sehemu hizo za chama. Basi, kuna KATIBA YA BARAZA LA WAZEE wa TANU chini ya fungu la V 40 (i) (uk. 1 Katiba ya Baraza la Wazee).

 

Humo ipo tafsiri ya neno “mzee” na neno “mwenyekiti”. Kwa mujibu wa Katiba ile maneno haya yalikuwa na maana ifuatayo:-

 

“Mzee” maana yake ni mtu mume au mwanamke ambaye umri wake haupungui miaka 50 na kuendelea.

 

“Katibu” maana yake ni Katibu wa Chama (TANU) wa Makao Makuu, Makuu Makuu ya Mkoa, Makao ya Wilaya, na Makao Makuu ya Tawi.

 

Hivyo basi, Baraza la Wazee wa TANU halikuwa na mtiririko wetu wa leo kiserikali (no chain of command administratively, yet theirs was politically).

 

Kwa mtizamo huo nchini hapakuwa na chombo cha kitaifa cha wazee wote.

 

“Mwenyekiti” maana yake ni Mwenyekiti wa TANU wa Mkoa, Wilaya au Tawi.

 

“Jina” Jina la sehemu ya wazee wa TANU ni Baraza la Wazee wa TANU.

 

Katiba hiyo hiyo ya TANU ilitamka Imani za Baraza, Madhumuni ya Baraza na Uanachama. Lakini ile ibara ya 11 ya Katiba inatamka waziwazi “HAKUTAKUWA NA KADI ZA BARAZA LA WAZEE!” Hapo ndipo tatizo lilipoanza. Katika Umoja wa vijana wana kadi zao za uanachama, Umoja wa Wanawake wana kadi zao za uanachama. Wazee hapana – hawakuhitaji kadi maalum zile zile kadi za TANU au siku hizi CCM zilitosha. Basi, kwa mazoea yaliyopo wanakubalika (are well-contained).

 

Matokeo ya mapokeo haya tunayaona hadi siku hizi. Umoja wa Vijana una viongozi wake wakuu wa kitaifa – Mwenyekiti, Katibu Mkuu na kadhalika. UWT una Mwenyekiti wa Taifa na Katibu wake Mkuu wa Taifa, lakini wazee pwaaa! Sasa kila kukitokea wazee kutakiwa kuzungumza na mkuu wa nchi, basi utaratibu ule ule wa matawi ya chama tawala kuarifiana kwa mdomo na mwitikio unakuwa mkubwa kama zamani pale.

 

Wazee bado wanaamini viongozi wao vijana kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere. Hapakuwa na haja ya utaratibu maalum kwa wazee kuomba au kudai haki zao.

 

Hali ikoje leo katika nchi yetu? Bado wazee tunangojea hisani na uaminifu wa vijana hata katika suala hili la pensheni kwa wazee wote. Kama vijana walioko serikalini wanathamini uzee hiyo pensheni kwa wote itapatikana hivi karibuni.  Tuamini na tutazamie hivyo. Lakini mbona vijana hao hao sasa wamejiandalia mafao ya uzeeni mazuri na wakatusahau sisi wazee wao? Iko namna hapo.

 

Wengi mngali mnakumbuka Oktoba 1978 Baba wa Taifa alipolitangazia Taifa juu ya uvamizi wa nduli Idi Amin. Tulijaa pomoni mle ukumbini mwa Diamond Jubilee na akatutangazia “…TUNAYO KAZI MOJA TU WATANZANIA SASA, NI KUMPIGA. UWEZO WA KUMPIGA TUNAO, SABABU YA KUMPIGA TUNAYO NA NIA YA KUMPIGA TUNAYO”. Si mliona namna ukumbi ule uliofurika ulivyolipuka kwa hamasa, vifijo na makofi? Chama kilikuwa na uwezo wa kukusanya wazee wote na wananchi wengine kupokea ujumbe muhimu kama ule.

 

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alipochaguliwa kwa kishindo mwaka 2005, wazee wa Dar es Salaam wanakumbuka Alhamisi ya Januari 31, 2006 tulikutana na kumpongeza  pale Ukumbi wa Diamond Jubilee. Wazee na wakazi wa Dar es Salaam tulijaa kweli ule ukumbi mkubwa. Mzee Mtulya aliongoza wazee wa Dar es Salaam siku ile. Rais alizungumzia hali ya chakula nchini kutokana na ukame kwa ukosefu wa mvua, alizungumzia tatizo la umeme unaokatikatika, alizungumzia juu ya bei ya mafuta inayozidi kupanda na hali mbaya ya amani nchini kutokana na uhalifu unaongezeka.

 

Wazee kama tungali tunakumbuka tulimweleza eti aangalie ile tabia ya wabunge kudai nyongeza ya mishahara na marupurupu. Sisi wenyewe hatukuomba pensheni! Si kuwa tulijisahau, bali ni yale mazoea ya enzi za chama kimoja ya kungojea hisani ya vijana! Ama kweli aliyezoea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi! Walisema wahenga zamani. Mambo yakamalizikia hapo. Hatukutamka ombi lolote kwa Rais siku ile hasa hili la hali ugumu ya maisha ya wazee vijijini.

 

Februari 21, 2013 pale Mzee Mwai Kibaki, Rais wa Kenya alipokuja kutuaga ndugu zake na jirani zake wa Tanzania, wazee tulikusanyika katika ukumbi wa PTA katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Temeke. Tukazungumza naye. Alituaga wazee wa Dar es Salaam, lakini kwa kweli aliaga wananchi wote wa Tanzaia kupitia sisi wa Dar es Salaam.

 

Kwa nini nimekumbusha historia hii ndefu ya wazee? Nilitaka kuonesha kuwa kipo chombo kilichozoeleka kimapokeo kinachotuwezesha wazee wa Jiji la Dar es Salaam kukutana na kufanya jambo. Chombo kile kwa utaratibu uliozoeleka hapa nchini hasa Dar es Salaam ni BARAZA LA WAZEE WA CHAMA TAWALA. Je, yupo anayepinga hilo? Chombo gani dhidi ya wazee hawa wa chama aliowaheshimu Mwalimu Nyerere na kuwaenzi kina ubavu wa kutukusanya wazee wote namna hiyo?

Je, huo sasa ndiyo tuite Sauti ya Umoja wa Wazee? Sidhani. Wala haiji akilini na haifikiriki. Ndipo linakuja lile swali langu. Kuna Umoja wa Wazee nchini Tanzania? Ipo sauti moja ya wazee kweli katika nchi hii?

 

Kipo basi chama chochote cha wazee kushughulikia kilio cha wazee, kuwasemea wazee na wakasikika kama Umoja wa Vijana au Umoja wa kina mama au Umoja wa Wafanyakazi (TUCTA) au Umoja wa Wazazi (TAPA)? Hakuna!

Swali la pili kwanini hali namna hiyo itokee? Mbona tupo wazee wasomi wengi tu wenye uwezo mkubwa wa kuongoza?

 

Itaendelea

 

By Jamhuri