Ndugu Rais, Mfalme Suleiman ametajwa na vizazi vingi kwa hekima kubwa

aliyokuwa nayo.

Mwenyezi Mungu alimwambia amwombe chochote, naye angemtimizia. Alimjibu akisema, “Ee, Mwenyezi Mungu naomba unijalie hekima!”

Aliomba hekima! Hakuomba mali wala maisha marefu au nguvu ya majeshi. Na sisi tumwombe Mwenyezi Mungu atujalie hekima!

Tunaposubiri uchunguzi wa mauaji ya Akwilina anayepumzika katika nyumba yake ya milele, wapo wanaoamini kuwa aliyefyatua risasi ndani ya basi lililokuwa na abiria akiwamo

Akwilina, iwe ni kwa uamuzi wake mwenyewe au kwa kutumwa, alikusudia kuua!

Na kwa sababu hiyo, wameistahili hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa maana yeye anawajua! Kama mlengwa alikuwa ni Akwilina au mtu mwingine yeyote, hilo tunasubiri uchunguzi.

Lakini jambo moja liko dhahiri, yeyote aliyehusika na mauaji hayo, laana yake lazima itamtafuna, kama siyo leo basi kesho!

Wanasema Mwenyezi Mungu akitaka kumpiga mwanadamu kofi, hakosei. Daladala ilijaa abiria, lakini risasi ya wauaji ilikwenda moja kwa moja kwa binti mdogo asiye na hatia yoyote, ikafumua kichwa chake.

Mungu alitaka kuwaonyesha Watanzania na ulimwengu kwa ujumla roho za kinyama walizokuwa nazo baadhi ya wanadamu!

Daladala ilikuwa inaandamana vipi mpaka nayo itawanywe kwa risasi? Hivi Akwilina ndani ya daladala alikuwa anaandamanaje mpaka naye atawanywe kwa risasi?

Mikono yao imetapakaa damu isiyo na hatia! Enyi wanawema mliojaliwa kubeba risasi ndani ya bunduki zenu, zitiini amri mnazopewa kwa uhodari mkubwa, kwa maana hiyo ndiyo kazi yenu.

Mwenyezi Mungu alipompatia kila mwanadamu akili ya kupima na kuamua mwenyewe, alikuwa anamwondelea sababu yakusema, ‘Oh! Nilikuwa natii amri!’Jehenam halali yako!

Ndugu Rais, mwanzoni tu baba nilikuomba uwaite raia wako wote uliogombea urais pamoja nao, ili mshauriane jinsi ya kuimaliza miaka mitano, nchi ikiwa na amani na utengamano.

Katiba inaweza kuwa mbovu lakini nchi ni ya watu wote! Katika maridhiano huku kutekana, kutesana na mauaji kama hivi, visingekuwapo!

Makubwa tuliyoyafanya, sasa yamechafuliwa na mauaji ya kinyama ya Akwilina. Na kama kuna

tunayoyafanya sasa, tusiwashangae watakaoona ni ubatili mtupu.

Tuliwaona baadhi ya viongozi wengine wa dunia, walioamua kutumia risasi na kuziona bunduki kama fagio la njia walimopita.

Leo, hawako tena! Akwilina umetangulizwa, ukatuombee busara za Rais Uhuru Kenyatta ili

wasema kweli watakapoyaita mapanki na makinikia kwa majina yake, wasije

wakaitwa wachochezi.

Minofu ilikwenda, tunahangaika na mapanki; dhahabu nayo ilikwenda tunapambana na makinikia.

Lakini ni bora angalau kinafanyika kitu sasa. Vikao vya Bunge huja na kuisha lakini

vya makinikia vingali vinaendelea.

Baba ulipowaambia Watanzania kuwa yule Yohani wa kizungu amekubali kulipa kila kitu, wenye vihelehele vyao hawakukawia.

Wakaja na hesabu zao kuonyesha kuwa kila Mtanzania ataibuka na Noah moja na chenji

itarudi.

Watanzania wakasema, Nabii si huyu! Wenzetu njiani wamekuwa wanabadilisha viongozi mpaka ikafikia hesabu kwamba kila Mtanzania

sasa, amepata sana, ataambulia bia saba bila chenji.

Lakini Baba, si ndio hawahawa ambao wameitangazia dunia kuwa kuna mnada mkubwa, wanauza vitendea kazi vyao vyote?

Walipoitwa kujieleza wakasema wataendelea kuchimba mpaka 2020. Watakuwa wanachimbia nini, vidole?

Kweli wajinga ndio tuliwao! Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu imeandikwa, “Sisi ni mtandao!” Watakaokuja kununua hiyo mitambo na mali zingine ni haohao wenzao ambao kwa kweli watakuwa wananunua vilivyo vyao!

Ndugu Rais, ubarikiwe baba kwa kutupatia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Tunamshukuru zaidi Mwenyezi Mungu kwa kumjalia mwanamwema huyu busara iliyo njema.

Kama Waziri Mkuu asingekuwa amewakemea hadharani waliokuwa wanawakataza wananchi walioonyesha mabango kule Tabora, na kuamuru waruhusiwe kuyaonyesha kila wakutanapo.

Hali niliyoiona siku ya kumuaga Akwilina pale Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, kama waonyesha mabango wangezuiwa, mwenye kujua hali ya nchi leo ingekuwaje ni Mwenyezi Mungu pekee.

Bango moja liliandikwa, “Tumechoka kuuawa!” Lingine lilisomeka,“Wauaji wasiwe wachunguzi”. Baba, dereva akisikia abiria wanapiga kelele, anapaswa kusimamisha gari ili kuwasikiliza! Isiwe gari linaungua!

Dunia imemwona Rais Uhuru Kenyatta akiwa ameshikana mikono na mshindani wake mkuu wa urais, Raila Odinga.

Lakini hazijapita siku nyingi tangu tumshuhudie Raila Odinga akijiapisha mwenyewe kuwa Rais

wa Wananchi wa Kenya.

Kwa busara zake, Rais Kenyatta aliyaona hayo yote kama kelele za mlango. Hazikumzuia kulala. Alichofanya ni kuimarisha ulinzi ili sheria za nchi zisivunjwe na Raila naye

ajiapishe kwa amani.

Leo wawili hao wamekumbatiana, huku Raila akimwita Rais Uhuru Kenyatta, ‘ndugu yangu’ na Rais Uhuru Kenyatta akimwita Raila, ‘Kaka yetu mkubwa’!

Kuongoza watu inahitajika busara!Tujiulize, leo ndugu Edward Lowassa angetangaza tu, wala asijiapishe, kuwa atajiapisha kuwa Rais wa watanzania, kwa vihelehele vyetu, hapa

nchini patakalika?

Kwanini woga wakati wote kama tuna mali ya wizi? Kuna wakati madege ya kivita kwa gharama kubwa yaliruka juu ya vichwa vya wananchi, eti yakibomoa ukuta ambao kwa kweli, haukuwako!

Kutegemea maendeleo ya nchi katika fikra za hofu kama hizi, ni sawa na kutegemea

machweo, mashariki.

Najisikia aibu nchi kutikiswa hata na utete dhaifu utikiswao na upepo dhaifu umtokao mpiga mluzi! Maandamano yakufikirika yamewafanya wengine waweweseke saa zote.

Tayari wako wanaosema kuna wanaotaka kupindua Serikali! Jamani, kirahisi hivi? Tujifunze kwa yaliyopita.

Kwanini tusikae nao tuwaulize wanadai nini. Shida yao hawa siyo maandamano. Bila kujua wanachodai, tutaweza kuzuia maandamano hata kwa damu nyingine, lakini madai yao kama ni ya haki, yatabaki yamesimama kama yalivyosimama ya waafrika weusi wa Afrika Kusini.

Walitekwa na kuteswa. Na wengi zaidi waliuawa! Lakini kwa busara kubwa Nelson

Mandela alikuja na meza ya maridhiano! Leo Afrika Kusini ni ya wote, weusi na weupe!

Ndugu Rais, Muumba wetu aliniumba nimuabudu! Namsujudia atujalie busara! Ulisema wewe ndio niko ambaye niko milele iliyopita na milele ijayo.

Nchi yetu inahitaji huruma yako sasa Ee, Mungu wangu! Ewe uketiye juu ya vyote maombi haya yafike kitini pako na sala yangu hii, ikawe manukato kama ilivyokuwa sadaka ya Abel na zaburi ya Daudi.

1597 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!