Ndugu Rais hakuna aliyeumbwa kwa bahati mbaya

Ndugu Rais, mwanetu Atosha Kissava katika wimbo wake wa Moyo wangu, aliimba, “Moyo wangu utakusifu wewe Baba, utakusifu milele! Najua uliniumba nitimize kusudi lako Baba. Siko hapa kwa bahati mbaya’’, yuko Mtanzania mwenzetu ambaye kwa asiyemjua, kwa jina lake peke yake hawezi kujua kama ana dini au la, amesema Serikali imewasilisha katika Mahakama ya Rufani kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu takatifu iliyotolewa na Mahakama Kuu kuwazuia Wakurugenzi (DEDs) kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mei 10, mwaka huu Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu weledi, Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhaji Masoud na Firmin Matogolo ilibatilisha kifungu cha 70(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka NEC kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi. Ikabatilisha pia na kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa wasimamizi wa uchaguzi. Mahakama Kuu imesema vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi. Huyu anayekata rufaa Watanzania wamueleweje? Hatufai! Anayezuia haki isitendeke katika nchi yetu, Watanzania tuunganishe nguvu zetu wote tumpinge kwa hoja! Tumeona katika nchi za wenzetu watendaji kama  hawa ndiyo wanaosababisha viongozi kuzomewa hadharani na wananchi na hata kutupiwa mawe! Tuwakemee hadharani hawa ambao mbunge Sugu anawaita ‘poyoyo’. Na viongozi wetu wawakemee wateule wao ambao wanaonekana dhahiri kuwa wanawaabudu bila kutumia fahamu.

Wanaokata rufaa wanawakumbusha Watanzania ile aibu kubwa iliyoipiga Mahakama ya Rufani baada ya kushindwa kutoa hukumu juu ya mgombea binafsi. Kuirudia aibu ile kwa sasa ni ngumu. Tunaye Jaji Mkuu mwingine makini anayeona baadhi ya watangulizi wake wanavyotazamwa katika jamii yetu baada ya kustaafu!

Mahakama Kuu chini ya majaji watatu weledi waliojaa utu imetoa hukumu kuwa vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi hivyo ni batili kwa sababu Katiba inasema mtu yeyote aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa. Hawa wako 74 ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki. Maamuma hawakumbuki karipio kali lililotolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Kaskazini juu ya rufaa ilizoziona kuwa zilikuwa hazina umuhimu dhidi ya Godbless Lema. Na hapa majuzi zikawa zinakatwa rufaa kama hizo dhidi ya Ester Matiko na mwenzake. Timamu wangebadilika na kufuata maadili. Jaji Mkuu wetu anatambua kuwa amani ni tunda la haki. Ataitetea amani ya nchi yetu dhidi ya wanaotaka kuivuruga!

Hukumu hii njema ya Mahakama Kuu inatafsiri moja tu –uchaguzi wote uliosimamiwa na watu waliokataliwa na Katiba ya nchi, hawa wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji, haukuwa uchaguzi huru na haki. Ndiyo kusema wote walioingia madarakani kutokana na uchaguzi huo hawana uhalali wa kisiasa. Matokeo yake kama alivyosema Katibu wetu Mkuu wa CCM, Ndugu Bashiru Ally, wanajikuta wanatawala kwa kutumia mabavu. Kuelewa kuwa si sawa kwa wateule wa rais kuwa wasimamizi wa uchaguzi ambao au rais mwenyewe ni mgombea au rais akiwa ni mwenyekiti wa chama kimojawapo kinachoshiriki uchaguzi huo, hakuhitaji elimu hata ya darasa la kwanza! Linapokuwa gumu kueleweka kwa msomi wa sheria hapo kuna tatizo. Wako watu ambao linapokuja suala la maslahi yao hawaoni tabu kuchojoa. Hawa wamechojoa hadharani, kwa pamoja tuwaeleze kuwa wanachofanya si sahihi.

Ndugu Rais, wakati hawa wanahangaika na rufaa, binti yetu Atosha anaimba kuwa hakuna aliyekuja kwa bahati mbaya! Kila mmoja wetu aliumbwa kwa kusudi fulani! Tujiulize, ni lipi lilikuwa kusudi lake Mwenyezi Mungu kutuleta hapa duniani? Tusije tukawa ndiyo sababu ya mateso makubwa kwa watu wake?

Baba, tulishauri tujifunze kutoka Makambako, ambako kijana aliinua bango lake ili baba yake alisome. Walinzi katili walichukua sheria mkononi na kuanza kumshushia kipigo cha mbwa koko mbele ya Rais wa wanyonge. Kijana akasulubiwa bila kuwa na hatia! Umati wenye hasira ukaingilia kati kumwokoa. Lakini kama mkosi ikasikika kauli ya bahati mbaya ikisema, “Mwacheni wamshughulikie’’. Umati wote ukasinyaa ghafla! Wakaikumbuka kauli nyingine mbaya zaidi. “Amueni name nitawaunga mkono’’. Katibu Mkuu wa CCM anasema watu wanahifadhi vinyongo vya muda mrefu! Baba, tutakuwa majinuni sisi tunaojipaka kinyesi, siyo wale wanaoizunguka dunia kuwaambia walimwengu watutazame

tunavyojipaka kinyesi! Ikishakuthibitisha dunia itawaamini!

Uliposema mwacheni, mleteni na bango lake nami nitalisoma, umati ulifunguka ukapiga kelele za uchungu. Alitokea mbele yako akiwa hoi kwa kisago! Kwa unyenyekevu mkubwa ingawa kwa maumivu makali, akakupigia magoti na kukuonyesha bango lake. Kumbe “alijitoa muhanga” kama kusulubiwa asulubiwe, lakini jamii yake ipate maji hata baada ya viongozi kuondoka. Huruma ilipokuingia ukaamuru akae jukwaani. Baba, tumejijaza hofu na woga mwingi kiasi cha kuogopa hata unyasi tu kama ule tukidhani ni ‘wapinzani’ ah, samahani, tukidhani ni nyoka. Walikuwapo wabunge wao, madiwani na wenyeviti, lakini nani alikuwa tayari kusulubiwa kwa ajili ya jamii yake? Wote walinywea! Mwaka 2020 wananchi hawatawarudisha madarakani viongozi wanaowafanya waishi kwa hofu.

Hatukuona akituzwa japo buku! Baba, kama mpaka leo wale katili waliomshushia kipigo mwanamwema yule, ukishuhudia, bado hawajaadhibiwa, wanao wanaoizunguka dunia kule nje wakiiambia kuwa serikali yetu imechafuka, wataonekana ndiyo wazalendo wa kweli kwa kuwa wanawasemea wananchi! Hawa nao ni watu wasiojulikana?

Basi, wanao watadhani watu wasiojulikana ni kati ya hao!

Kumbe wanajulikana! Matumaini pekee ya Watanzania yamebaki kwa

Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Bashiru Ally. Mzee wangu mstaafu aliniuliza, “Huyu mbona anaongea busara kubwa wakati anaonekana ana umri mdogo?’’

Nikamwambia hatufahamiani, lakini kuna wakati tulikuwa tunachangia pamoja fikra zetu kwenye vyombo vya habari vya nje, BBC, DW, Radio France International, VOA na vingine. Akasema, tumuombee asije akafanana nao!