Jumanne, Mei 7, 2019, wakati nimeketi kibarazani kwangu nasoma Gazeti la JAMHURI, Toleo Namba 397 la tarehe 7 – 13 Mei 2019, alikuja jirani yangu anaitwa Imma, kijana wa miaka 25.

Kabla sijamwonyesha nilichokuwa nasoma, nikamuuliza: “Unadhani Mwalimu Nyerere angekuwepo akaona utendaji wa Rais Magufuli angesemaje?” Haraka, haraka akajibu: “Angempongeza sana!”

Siku hiyo na siku zilizofuata niliendelea kupigiwa simu na kupokea ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kutoka kwa Watanzania wa rika tofauti waliosoma makala yangu ya “MWALIMU ANGEKUWEPO ANGESEMAJE?” iliyotoka kwenye toleo hilo la gazeti la JAMHURI. Wapo walionipongeza na kusema wameipenda makala hiyo na wapo waliotoa maoni yao. Kwa kuwa si rahisi kuandika yote nitachagua machache.

Sms moja ilitoka kwa Elia Yohana mwenye umri wa miaka 29, anayeishi Hai, Kilimanjaro, aliyeniandikia:

“Hongera sana Mama Anna kwa makala yako kwenye gazeti la JAMHURI nimejifunza mengi ambayo nilikuwa siyajui…” Akasema; “Tunafurahi tumepata Rais anayeenzi na kukamilisha sera za Mwalimu, na ambaye amependa Serikali ihamie Dodoma kama alivyotaka Mwalimu.”

Mtanzania mwingine ambaye hakunipa jina lake, aliandika: ”…Yote uliyoandika yana ukweli kwa kiasi kikubwa. Kila mtu ana namna ya kuongoza kulingana na hulka yake binafsi, ila kwa huyu (Rais wetu) analandana sana na Mwalimu Nyerere. Hata hivyo, Mwalimu alikuwa mwanadiplomasia mkali zaidi sana…” Akaongeza: “Watumishi wa Umma wanapaswa kubadilika ili wawe watumishi wazuri wa UMMA.

Tatizo ni kwamba hawakubali kuwa ni watumishi, wanajiona kuwa ni mabosi wa umma. Hilo ndilo tatizo kuu…”

Sms nyingine ilitoka kwa Ndugu Mwaiposa mwenye umri wa miaka 59 ambaye aliniambia kwamba nimefanya jambo jema kwa kuthubutu kuandika mambo makubwa yanayofanywa na mpendwa wetu Dk. John Pombe Magufuli. Akasema: “…Mimi naona picha ya Mwalimu Nyerere, Sokoine na Mzee Mandela ndani ya Magufuli…” Mwisho akasema: “Dada Anna endelea kutumia kalamu yako kutuelimisha. Hongera sana.”

Ndugu Gerry Lufingo aliandika: “Nimeipenda makala yako. Mwalimu angepata faraja kuona jinsi Serikali ya Awamu ya Tano inavyoimarisha huduma za Jamii…”

Naye mfanyakazi mwenzangu enzi hizo, Johnson Rugoye, ameniandiki: “Shalom. Nimesoma makala yako. Umenikumbusha kauli ya Mwalimu kuwa mtabinafsisha hadi magereza!…”

‘Bosi’ wangu sitamtaja jina, ameniandikia: “Tunashukuru na kukupongeza sana. Sasa andaa makala matata kabisa ya miaka 20 bila Mwalimu!”

Ambao sms zao sikuweza kuziandika hapa mniwie radhi, itoshe kusema nathamini sana mawazo yenu na nawashukuru sana kwa pongezi.

Kwa upande wa simu, ya kwanza kabisa ilitoka kwa Mzee Masalakulangwa wa Mwanza aliyeniambia kwamba yeye ni mzee wa miaka 76 aliyeshuhudia awamu zote tano. Akasema anampongeza sana Mheshimwa Rais Magufuli kwa kazi nzuri anyoifanya. Akataka Watanzania tuungane katika kumuunga mkono Rais wetu ili apate wepesi kwenye kazi ya kuliletea Taifa letu maendeleo na tudumishe amani.

Mzee huyu alisema hajaridhika na anachokiona kwenye Makumbusho ya Butiama. Anadhani bado hayamuwezeshi mtu anayetembelea Makumbusho hayo kumwelewa vizuri Mwalimu na kazi yotealiyoifanya kwa Taifa letu na Afrika kwa ujumla. Alisema aliwahi kujaribu kupata taarifa juu ya “Mulungushi Club”, lakini hakufanikiwa.

Simu nyingine ilitoka kwa Mwalimu Augustine Kasase wa Butimba TTC Mwanza, yeye naye aliniambia ameifurahia makala yangu. Mwalimu Augustine alizungumzia siasa za Mwalimu Nyerere kwa kusema kwamba UTU ndio nguzo kuu kwenye siasa iliyopuuzwa ya Ujamaa na Kujitegemea. Akasema kwamba

“Utu” kwenye siasa ya Ujamaa wa Mwalimu ndio msingi wa upendo na mshikamano uliojengeka miongoni mwa Watanzania ambao pamoja na tofauti zetu  unaendelea kuwepo hadi leo hii. Upendo na mshikamano huu huwezi kuukuta kwenye nchi yoyote ile barani Afrika, hivyo inabidi tuuthamini na kuulinda.

Mwalimu Augustine anasema yeye huwa anawafundisha wanafunzi wake kwamba Ujamaa wa Mwalimu ni Ujamaa uliojengwa katika fikra za Utu, wakati Ujamaa wa Karl Max ulijengwa katika fikra za kiuchumi.

Rais Magufuli anapojaribu kuyaishi yale ya Mwalimu Nyerere, Watanzania tunapaswa tuielewe nia yake njema na tumsaidie ili tumrahisishie kazi ngumu aliyonayo ya kuliongoza Taifa na kuwatafutia wananchi maendeleo wanayostahili kupata.

Miongoni mwa walionipigia simu kuhusu makala yangu, mmoja wao alilalamika kwamba Taasisi ya Mwalimu Nyerere haisikiki, inasikika pale viongozi wake wanapoonekana kwenye matukio ya watu wengine, ofisi za Taasisi mikoani zimefungwa na kwamba uongozi wa Taasisi ‘umechoka’ inabidi vijana wapewe nafasi waiongoze.

Kwa kuwa niliwahi kufanya kazi kwenye Taasisi ya Mwalimu Nyerere, napenda kuandika machache.

Taasisi ya Mwalimu Nyerere ni Taasisi moja muhimu sana katika kusimamia, kutunza na kusambaza yale yote aliyoyafanya Mwalimu katika uhai wake na uongozi wake uliotukuka, uliojikita kwenye Amani, Umoja na Maendeleo yanayolenga Watu.

Taasisi hiyo ilianzishwa na mwenyewe Mwalimu Nyerere, baada ya kustaafu aliombwa na Watanzania waliokuwa na nia njema kabisa ya kumuenzi. Bodi ya Taasisi iliteuliwa na mwenyewe Mwalimu, mpaka leo ipo, imesheheni watu ‘wazito’, watu makini sana, watu ambao walikuwa viongozi wa ngazi za juu nchini mwetu na ambao Mwalimu Nyerere aliwaamini sana kutokana nauadilifu  na utumishi wao uliotukuka. Mwenyekiti wa Bodi akiwa Dk. Salim Ahmed Salim, mwanadiplomasia mahiri aliyeipa nchi yetu heshima kubwa kimataifa na Afrika. Wote hawa Mwalimu aliamini kabisa kwamba wataendeleza ‘legacy’ yake, na ndivyo wamekuwa wakijitahidi sana kufanya kwa miaka yote hii. Lakini, zimekuwapo changamoto mbalimbali ambazo mwishowe zimefanya Taasisi isisikike ipasavyo.

Changamoto moja ni kutokuwa na uwezo wa uhakika wa kifedha na usimamizi mzuri wa mapato.

Mwalimu aliamini sana kwenye suala la Kujitegemea. Kikao cha kwanza kabisa cha Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere kilifanyika mwaka 1996. Napenda kujivuna kwamba nilikuwepo kwenye kikao hicho na nilikuwa nachapa yote yaliyokuwa yakizungumzwa kwenye kikao (enzi hizo iliitwa audio typing). Moja alilosema Mwalimu ni kwamba yeye hakuwa hodari wa kuomba-omba, kwa hiyo alitaka Taasisi ijitahidi kuwa na chanzo cha mapato cha kuweza kufanya ijiendeshe yenyewe, IJITEGEMEE! Nadhani, Taasisi ilichelewa kubuni miradi ya kufanya ijitegemee badala yake imekuwa ikitegemea ‘huruma’ za wasamaria wema waliompenda Mwalimu.

Kuhusu vijana kutokushika hatamu ya uongozi wa Taasisi nadhani ziko sababu nzuri tu. Kwanza, naamini Wajumbe wa Bodi wangependa kuiacha Taasisi chini ya uongozi mpya ulio madhubuti na IKIJITEGEMEA kama Mwalimu alivyotamani.

Pili, naona Mkurugenzi Mtendaji, Mzee Ndugu Joseph W. Butiku, aliyeaminiwa na kukabidhiwa na Mwalimu jukumu la kuiendesha Taasisi anapata mtihani mgumu. Kwa muda mrefu amekuwa akitafuta na naamini angependa sana kupata mtu atakayetosha kwenye ‘viatu’ vya uendeshaji bora wa Taasisi; mtu atakayeonekana ana Mwalimu ndani ya moyo na akili zake!

Mwisho kabisa, nadhani huu ni wakati muafaka wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuweza kumsaidia Rais aliye madarakani aliyejipambanua kurejea yale aliyoyasimamia Mwalimu Nyerere katika azma yake ya kujenga Tanzania Mpya. Kwa kufanya hivyo, naamini Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake wataisaidia Taasisi kufanya kazi inayopaswa kufanyika.

Nawashukuru sana wote walioipenda makala yangu ya “Mwalimu Angekuwepo Angesemaje?” na waliotoa mawazo yao. Mungu awabariki sana.

Anna Julia Chiduo-Mwansasu,

Mstaafu,

Mkazi wa Yange-yange, Kivule,

Dar es Salaam.

0655 774 967

818 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!