Nimesikia Serikali inatathimini kuweka cable car kwenye Mlima Kilimanjaro ili kuwafikisha wageni kileleni kwa haraka. Cable car ni mfumo wa usafiri unaobeba abiria kwenye behewa dogo linalosafiri kwa kuning’inia kwenye waya zilizopitishwa kwenye nguzo.

Naamini zipo sababu nyingi nzuri za kuishawishi Serikali kuachana na wazo hili. Nitataja chache.

Kwanza, kulinda ajira. Inakadiriwa watu 20,000 wanahudumia wageni wanaokwea Mlima Kilimanjaro na Meru. Kila mgeni anasindikizwa mlimani na wastani wa wahudumu watatu. Uwepo wa mfumo mpya utawafanya baadhi ya wageni kuacha kukwea mlima kwa mfumo uliopo.

Pili, wapo wageni ambao wanakwea Mlima Kilimanjaro kwa sababu ya ugumu wake, siyo kwa urahisi wake. Kwa hawa, kitu rahisi hakina thamani kama kile kinachowatoa jasho.

Kwa kundi dogo sana la binadamu duniani kukwea Mlima Kilimanjaro ni suala rahisi sana, lakini kwa wengi kufika kileleni ni kazi inayohitaji maandalizi na jitihada kubwa. Hii ni sifa ya Mlima Kilimanjaro ambayo itafutwa kwa kurahisisha kufika kileleni.

Sababu moja inayofanya tuwe na tofauti kubwa sana ya bidhaa, mathalani nguo, ni kwa sababu binadamu hupenda kujitofautisha na binadamu mwenzake. Naamini ukweli huu upo pia kwenye utalii. Inapokuwa rahisi kufika kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro mgeni anaweza kuamua kwenda kukwea Mlima Kenya, au Mlima Rwenzori nchini Uganda.

Anayetaka kufika kileleni kwa nguvu zake mwenyewe na yule anayependelea kubebwa ni aina mbili tofauti za wageni. Kuanzisha mfumo utakaoongeza wale wanaotaka kubebwa bila shaka kutapunguza idadi ya wasiotaka kubebwa.

Kama nia ni hiyo, basi mjadala ni mfupi sana, lakini kama nia ni kulinda hadhi iliyopo sasa ya Mlima Kilimanjaro kama eneo la utalii wa ukakamavu basi kuna haja ya kutafakari upya uamuzi huu.

Cheti cha kufika kileleni anachopewa mkwezi sasa kitashushwa thamani sana iwapo njia ya kufika kileleni itarahisishwa na mradi huu mpya.

Nakumbuka mkakati kwenye sera ya utalii ya kuweka tozo kubwa ili kudhibiti wimbi kubwa la watalii ambao wanakimbilia unafuu wa gharama. Sina hakika kama mkakati huo bado upo kwa hifadhi za wanyama ingawa mradi huu unaashiria kama ndiyo lengo mojawapo kwa Hifadhi ya Kilimanjaro. Wingi wa wageni unaweza kuongeza mapato, lakini ukaleta athari kubwa za mazingira.

Lakini kutarajia ongezeko la mapato si suala la uhakika sana kwa sababu, kama nilivyodokeza, mradi huu unaweza kupunguza idadi ya wakwezi ambao huingiza pesa nyingi.

Kwa wageni wa nje gharama za kukwea Mlima Kilimanjaro zinaanzia dola 1,000 za Marekani na hufikia hata dola 4,000 kwa mgeni mmoja. Huyu bado hajalipia gharama za hoteli kabla na baada ya kukwea mlima, gharama za kukodi vifaa, na gharama nyingine ndogo ndogo.

Ili ongezeko la mapato lifikiwe kwenye mradi huu mpya kinachohitajika kutokea ni kwa mapato yatakayopungua kwa kila mgeni ambaye ataamua kuacha kukwea mwenyewe na kuamua kubebwa, au kuamua kwenda Mlima Kenya au Mlima Rwenzori, kufidiwa na tozo za hawa abiria wa kubebwa.

Kwa desturi tozo za cable car ni nafuu. Itahitajika idadi kubwa ya wageni wa kubebwa kuweza kufikia gharama ambazo analipa mkwezi mmoja kwa sasa.

Yajayo hatuyajui, kwa maana hatujui idadi ya wageni watakaoamua kubebwa hadi kileleni au kuhamia nchi jirani, lakini tunayo mifano ya uamuzi ambao ulifanyika kwa nia njema na ukaleta hasara. Mfano mzuri ni kupandikiza mbegu ya samaki aina ya sangara kwenye Ziwa Viktoria na athari mbaya ilivyotokea ya kushambuliwa kwa aina nyingine ya samaki.

Ipo sababu nyingine ambayo inahitaji tafakuri. Kilele cha Mlima Kilimanjaro siyo eneo kubwa sana na kuna kibao kimoja ambako kila anayefika huko angependa kusimama hapo na kupiga picha ya kumbukumbu. Upo msimu wa wageni wengi ambapo inachukua muda kwa mgeni kupata fursa kusimama mbele ya ubao ule na kupiga picha kwa sababu tu ya wingi wa watu.

Nashindwa kutathmini hali ambayo, baada ya uamuzi wa kupitisha mradi huu, kwamba kutakuwa kuna ongezeko kubwa la wageni wanaofika kileleni kwa njia hii mpya, halafu wakajaa eneo la kilele na wale waliotumia siku tano kufika pale wakiwa na uchovu mkubwa wakawa wanasubiri foleni ya kupiga picha.

Nimekwea Mlima Kilimanjaro mara nyingi. Aidha, nimepanda baiskeli ya masafa marefu nikitumia siku nyingi. Mwaka 2014 kwa kutumia baiskeli zetu niliongozana na Mskoti Ross Methven kutoka Butiama hadi Dodoma. Alipomaliza safari yake ya Edinburgh hadi Cape Town alikuwa ameendesha baiskeli kwa kilomita zaidi ya 9,000. Mimi niliendesha kwa kilomita 877 tu.

Unaweza kuwa mmoja wa wale wanaoamini haya mambo hufanywa na watu wanaohitaji kupimwa akili. Mimi sitafanya jitihada ya kukubishia kwa sababu kila binadamu ana wazimu wake. Kabla ya kufika Dodoma tuliulizwa na mtu mmoja njiani: “Kama mnaelekea Dodoma kwanini hampandi basi?”

Suala halikuwa tunataka kufika Dodoma haraka kiasi gani. Suala lilikuwa tunataka kufika Dodoma kwa njia gani.

Kulazimisha kila anayekwenda Dodoma apande baiskeli siyo rahisi, lakini inawezekana kufanya uamuzi wa kimkakati wa kulinda hadhi asilia ya Mlima Kilimanjaro kama pia eneo la utalii wa ukakamavu na kusema kuwa anayetaka kufika kileleni asibebwe.

[email protected]

Please follow and like us:
Pin Share