Ndugu Rais hekima ya mwanadamu ni kuchagua ya kusema

Ndugu Rais imeandikwa, usisemeseme hovyo ewe mdomo wangu bali uvilinde vilivyomo ndani yangu. Maneno mabaya yanachafua moyo na roho pia, kinywa changu ukayatangaze mema yampendezayo Mungu. Hekima ya mwanadamu huchagua ya kusema. Tuitawale midomo yetu ili isitugombanishe; tuitawale midomo yetu ili tusimkwaze Mungu.

Maelekezo tuliyokwisha kuelekeza kwa midomo yetu ni mengi lakini mengine yanaweza kuwa ya kusikitisha. Matokeo ya baadhi ya maneno hayo ndiyo haya ambayo leo dunia inatutuhumu kwayo kuwa kuna uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu nchini mwetu.

Wanawema, tuhuma tunazotuhumiwa kwazo na baadhi ya sehemu ya dunia ni nzito sana na kwa kweli zinatisha.

Baadhi ya wanaosambaza tuhuma hizo huko duniani Mwenyezi Mungu alipowaleta hapa duniani aliwajalia uwezo mkubwa wa kufikiri na kujieleza. Ukifuatilia sana yanayosemwa katika mitandao, utagundua kuwa mwanzoni dunia ilishtuka tu, lakini sasa kwa bahati yetu mbaya dunia imeanza kuwaamini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Palamagamba Kabudi, amekuwa mkweli na muwazi. Ameliambia Bunge kuwa nchi yetu ilipata fursa ya kukutana na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Akasema kwamba waliitumia fursa hiyo kufafanua tuhuma nzito za ukiukwaji wa haki za binadamu nchini mwetu ambazo dunia inaituhumu nchi yetu. Kwa kusema hivyo alikiri dunia inaishutumu nchi yetu kwa ukiukwaji wa haki za binadamu. Wengi wanaona kwanza ilikuwa ni lazima kuzikanusha kwa nguvu zetu zote tuhuma hizo mbele ya baraza hilo kwa kusema kuwa hazina ukweli. Halafu kuzifafanua kungefuata. Kuzifafanua ni kuzikumbatia, jambo ambalo linaweza kuwafanya wengine wakadhani tumezikubali kuwa ni za kweli. Unaweza kuzikubali tuhuma kwa sababu umeonyeshwa ushahidi wote uliopo na kwamba umewasilishwa vizuri.

Tuhuma za uongo timamu huzitupilia mbali mara moja. Kuzikumbatia na kuanza kuzifafanua ni kukiri. Hivyo kuanza hoja ya kuzifafanua ni kujaribu kutafuta huruma ya dunia wakati dunia siku zote husimama katika haki. Na kwa sababu hiyo sasa dunia inatuhukumu. Kufafanua peke yake maana yake ni nini? Kufafanua si kusema hayo mnayotutuhumu si kweli. Kufafanua ni kupanua yaliyosemwa ili yaeleweke vizuri zaidi.

Kufafanua si kukataa. Hivyo tulipopata fursa, tena juu ya jukwaa muafaka kabisa, hatukuitumia vema fursa hiyo kukanusha tuhuma hizo.

Wanasema usipokanusha tuhuma zinazotolewa dhidi yako unazikubali. Ni bahati mbaya sana kwa baadhi ya wenzetu ambao labda kwa ufinyu wao wa fikra wanasema dunia inatutuhumu kwa kuvunja haki za binadamu kwa sababu tu inatuonea wivu kwa mambo makubwa yanayofanyika nchini mwetu.

Wakisema hivyo wanadhani wamekanusha kweli kweli. Tuwe wakweli, tuonewe wivu sisi kwa lipi? Haya ambayo sisi tunaona tunafanya ni makubwa, tukiyalinganisha na yanayofanywa na wengine duniani, yatakuwa na ukubwa gani wa timamu aone wivu?

Wanasema mabeberu wanatuonea wivu. Ajabu ni kwamba wote wanaopiga kelele nyingi wakidai kuna watu mabeberu ni wachanga ambao wakati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anasema juu ya mabeberu, wao hawakuwapo. Sasa ndiyo wanajionyesha kuwa hawajui hata maana ya mabeberu. Ni vigumu katika hili kuyasahau maneno ya Baba Askofu Bagonza. Anasema wajinga wengi hujulikana pale wanapojieleza. Katika majina matatu ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alituambia kuwa ndiyo maadui wetu wa taifa letu, jina mabeberu halimo. Aliwataja hao maadui watatu kuwa ni ujinga, maradhi na umaskini. Mabeberu kwa baadhi ya hawa wenzetu ni njonzi. Mambo ya kufikirika ambayo mtu huyaona anapokuwa usingizini.

Dunia kukushutumu kwa kukiuka haki za binadamu hakuwezi kuchukuliwa kama jambo la mzaha hivi. Dunia imeshuhudia mwisho mchungu wa baadhi ya viongozi ambao walikengeuka wakaanza kutawala kama wafalmebadala ya kuongoza.

Wakaanza kusema utawala wangu, bila kuweka fahamu kuwa kuna mwisho. Wanapoanza kuonja uchungu wa siku zao za mwisho ndipo huanza kutaka kubadilika ili waonekane ni viongozi wema, lakini wanakuwa tayari wamechelewa. Busara ni kuomba mabadiliko hayo sasa. Lakini kwa watawala wengi tuliowaona katika historia ya dunia na hasa katika nchi zetu hizi za Afrika, ambao hujiona wana nguvu za Kiungu, hiyo kwao huona haiwezekani mpaka hukumu inapowakuta.

Basi kwa dhati kabisa tumshukuru Waziri wa Mambo ya Nje kwa ufafanuzi alioutoa aliposhiriki mijadala katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Tuhuma hizi nzito, ni tuhuma zetu wote kama taifa. Yatupasa tuzikabili kwa pamoja.

Watanzania tujipange nyuma ya baba yetu ili kwa pamoja baba atuongoze tukazikanushe. Hii ni vita. Vita ya kuitafuta kweli. Tuwe ngangari hata kama mwishoni tunaweza kuonekana kama mwizi wa kuku ambaye mahakama inamtia hatiani huku yeye akizidi kudai kuwa hakutendewa haki japo kuku mwenyewe angali amemshikilia mkononi.

Labda tuliyafanya mengine kwa kutokujua kama tulikuwa tunavunja haki za binadamu. Au nia na dhamira yetu ilikuwa njema tukidhani tunaiokoa nchi yetu. Tukasahau kuwa katika zama hizi tulizonazo kila tulifanyalo,tunalifanya juani, dunia ikishuhudia.

Tutazame nyuma, ni maovu gani yanayosababisha tutuhumiwe? Je, yaweza kuwa ni yale tuliyojisemea wenyewe kuwa ‘ya Makambako yawe ni fundisho kwetu?’ Mkutano wa Makambako uliingia katika kumbukumbu ovu za nchi yetu.

Umati ulikuwa mkubwa mno huku viongozi wa kutetemesha wakiwa wamejaa jukwaa kubwa. Ulinzi wa Makambako ulikuwa ni wa kufa mtu. Mwanamwema akiwa na bango lake, na kwa nia njema kabisa akataka kuliinua juu ili baba yake, baba wa wanyonge alisome, walinzi walimdaka na kuanza kumshughulikia kwa kipigo cha kikatili cha mbwa koko. Wananchi walipoingilia kumuokoa, sauti kali ikaamuru: “Mwacheni wamshughulikie.” Ah! Mdomo kweli ulikiponza kichwa. Alipokea kipigo cha kikatili huku baba yake akishuhudia. Iliposikika: “Mwacheni aje,” kijana wa watu alikuwa tayari ‘nyakanyaka’. Hatamaniki. Kumbe maskini hakuwa mpinzani na shida haikuwa yake.

Alikuwa anaitetea jamii yake ipate maji. Dunia ilishuhudia tukio hili la kikatili la Makambako. Je, ni hili tunalotuhumiwa kwalo? Au kuna maovu ya kutisha zaidi tuliyokwisha kuyafanya? Baba tuongoze wanao twende tukakanushe tuhuma hizi huko duniani.