Ndugu Rais, imeandikwa kuwa mwanadamu ni mavumbi. Mavumbini ulitoka na

mavumbini utarudi! Ulitoka kwa udongo na utarudi kwa udongo! Kati yetu

sisi wote hakuna atakayekufa halafu jeneza lake lihifadhiwe dalini au juu ya mti kama mzinga wa nyuki.

Haijalishi litakuwa na thamani ya kiasi gani na wala haijalishi kama litafunikwa sanda ya bendera ya

taifa au kaniki. Jeneza letu litafukiwa chini, udongoni! Na huo ndio utakuwa utimilifu wetu.

Ya dunia ni mengi na mengine yanapumbaza na kututia kiburi tusijiulize kesho yetu itakavyokuwa.

Muda wetu wa kukaa hapa duniani ni mfupi sana. Ikizidi miaka makumi saba ni kwa neema tu! Duniani hapa sisi wote ni wapita njia – tunasafiri. Nyumbani kwetu kwa kweli ni kule juu aliko Baba! Lakini huko hakuna chochote kinyonge kitakachoingia. Heri yao waaminio katika uwepo wa Mwenyezi Mungu kwa maana hao wataivuna pepo! Jina la Bwana lihimidiwe.

Imeshindikana nini sisi kuishi katika upendo kama wana ndugu? Kwanini nguvu kubwa na kufokeana? Kati yetu wako waliojaa tamaa ya mali, na wako waliochizika kwa mamlaka walionayo. Kwanini tusikae tuongee kwa upole yaishe kama wanavyofanya ndugu zetu wa Kenya hivi sasa?

Tumetanguliza u-mimi mbele badala ya Mungu. Ole wetu sisi! Labda ingelikuwa ni bora kwetu kama tusingezaliwa!

Ndugu Rais, Mwenyezi Mungu ni mmoja. Wanaohubiri chuki miongoni mwetu ili tuchukiane hawana dini hata kama majina yao mengine yanafanana na yale walionayo wenye madhehebu yao. Kushinda kwenye nyumba za ibada; na kufanya ibada ni vitu viwili tofauti. Shetani wa mtu ni mtu.

Wamepandikizwa ushetani na wamsujudiao shetani. Nao wanaitenda dhambi kubwa kuliko hawa waliowatuma.

Hatuwafokei kwa kukosa ufahamu ya kwamba wanatutengenezea mwisho wa majuto na simanzi kwa maisha yetu yote yatakayobakia. Tuwaambie wana wapotevu hawa, ‘acha’ kwa sababu Mungu ni

upendo. Hawatupambi wanatudunisha mbele ya waliotimamu. Tausi mzuri hahitaji mapambo, hivyo tuchukuliane kwa upole. Nchi hii ni yetu wote katika umoja wetu. Leo tuko hapa kesho hatuko hapa. Tutakuwa wapi wapendwa?

Aliyezifanya nchi kuwa na katiba alikuwa na uelewa mpana kuliko sisi. Katiba ni katiba kuwa mpya, pendekezwa au ya zamani hiyo inategemea na fikra za watu. Wanaosema waliinadi hawana sababu ya msingi mpaka wawaambie watu. Vivyo hivyo, wanaosema hawakuinadi pia hawana sababu ya

kuwaambia watu hilo. Kuinadi au kutokuinadi hakuondoi wala hakuongezi umuhimu wa katiba. Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili, kunadi ni kutoa tangazo kwa sauti ya kusikika. Ndiyo kusema yeyote aliyepata madaraka kwa kuapa kuilinda katiba aliinadi katiba.

Katika Kamusi Kuu ya Kiswahili imetafsiriwa kuwa, katiba ni, ‘Mkusanyiko wa sheria na kanuni zinazotumiwa kuendesha shughuli za nchi, chama au kikundi cha watu wenye malengo yanayofanana.’  Kwa kuwa ni mkusanyiko wa sheria na kanuni, basi zipo sheria na kanuni katika katiba ambazo ni za kudumu. Na zipo sheria na kanuni ambazo kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kiinchi hufika wakati zikapitwa na wakati na kuzifanya zisifae tena. Hali hiyo inapojitokeza halafu baadhi ya viongozi wakaonyesha kutotaka kuziondoa au kuzibadili, viongozi hao hujiondelea wenyewe sababu ya kuwa viongozi halali wa watu. Hubaki kuwa viongozi maslahi ambao watahubiri amani hewa kwa midomo yao na kuivunja amani ya kweli kwa vitendo vyao.  Wataitukuza hofu huku wakiwatesa wananchi wao. Wamesahau kuwa njia yetu ni moja.

Nchi itakapokosa amani watashamiri wanaojulikana na wasiojulikana. Watawateka watu na kuwatesa. Wengine watashambuliwa kwa risasi kama wanyama wa mwituni. Nao wana wa Mungu watakapoyaona haya yakijiri wasiinamishe vichwa vyao chini, bali watambue kuwa njia yetu ni moja.

Wainue macho yao juu waitazame milima wakijua kuwa hapa walipo wamelala juu ya jiwe tu kesho wataendelea kwakuwa hakuna makali yasiyokuwa na ncha.

Wananchi wamemsikiliza sheikh mwema akielezea matamanio ya mwanae katika maisha.

Alisema mwanae alimwambia, “Baba nikimaliza shule nikafanikiwa kazi ninayoitaka ni kuwa polisi tu. Eti Polisi hawakosi hela.”

Katika kuitilia uzito hoja yake sheikh mwema akaihubiri Injili kama ilivyoandikwa katika Luka 3:14. Akasema, “Katika vitabu vilivyotangulia Bwana Yesu alikuwa anafundisha watu waliokuwa wanamsikiliza kwa kuwaambia sifa anazopaswa kuwa nazo mtu ili apate kuingia katika Ufalme wa Mbingu kulingana na kazi anayoifanya mtu huyo’’.

Alisema Bwana Yesu alitaja sifa kwa kazi zote, lakini hakusema kitu kuhusu kazi ya polisi. Polisi walikuwapo. Ndipo askari nao wakamsogelea wakamuuliza Bwana Yesu, “Sisi nasi tufanye nini ili tuurithi ufalme wa mbingu?’’ Yesu akawaambia, “Msimdhulumu mtu na wala msimshitaki mtu kwa uongo.Tena mtosheke kwa mishahara yenu’’.

Wakati sheikh mwema akitoa mahubiri hayo habari njema zilizowafikia wananchi zinasema Mahakama njema kutoka Iringa, imemwona hana hatia na kumwachia huru mshitakiwa aliyeshitakiwa na polisi kwa kosa la kujiteka na kosa la kusema uongo. Kwa hukumu hiyo njema Mahakama hiyo chini ya hakimu mwema imewathibitishia Watanzania na umma wote wa Mwenyezi Mungu popote pale walipo kuwa polisi waliomshitaki yule mwanamwema walimshitaki kwa uongo. Tukizingatia maneno ya Yesu Kristu kama yalivyoandikwa katika Luka 3:14 “… na wala msimshitaki mtu kwa uongo,’’ hawa wamejithibitishia wenyewe tiketi ya kuingia katika lile ziwa la moto, jehenam.

Polisi ni mkono wa serikali. Mkono wa mtu ndiyo mtu mwenyewe. Kushindwa katika kesi hii ni aibu kwa serikali. Katika Biblia imeandikwa, “Amtumae mjinga hunywa hasara na kujikata miguu.’’

Watakaosema serikali imemfanyia raia wake huyu dhuluma, watakuwa wamekosea wapi? Yesu alisema, “Msimdhulumu mtu.’’ Moto wa milele uko dhahiri kwa yeyote anayedhulumu umma wa Mwenyezi Mungu. Ukiona upepo unavuma ujue kuna mahali ukifika utakoma. Mateso yetu ni hapo utakapokoma. Siku zinakuja! Siku za kihoro! Siku za maombolezo na majuto! Siku ya kuhukumiwa kwetu yaja. Katika Kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Hatutahukumiwa kutokana na mamlaka tuliyokuwa nayo, bali tutahukumiwa kutokana na namna tulivyoyatumia mamlaka hayo!’’  Tukumbuke njia yetu ni moja!

1626 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!