Nichukue fursa hii kutoa salamu zangu za dhati kwa mtu ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la mlalahoi miaka michache baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini.

Jina hili tulipewa kundi fulani na wanasiasa wetu kwa lengo la kutuonyesha tofauti tuliyonayo sisi na baadhi ya wafanyabiashara au wafanyakazi wakati huo. Walalahoi tulijijua bila hata kuuliza, kwa maana ya kuthibitisha. 

Kwanini tuliitwa walalahoi? Zipo sababu nyingi, lakini chache za wakati ule ilikuwa ni mlo wa shida na aina ya kazi ambazo zilikuwa zinatukabili dhidi ya malipo yaliyokuwa yakitolewa. Ili uwe mlalahoi ilikuwa lazima uwe katika kundi la kupata mlo mmoja kwa siku au miwili ya kubahatisha.

Ilikuwa mlalahoi anafanya kazi kwa muda mrefu zaidi kwa siku na kazi ngumu ambayo ilikuwa hailingani na malipo yanayotolewa. Mlalahoi alikuwa hapati huduma nyingi za kijamii, mbali ya chakula kilichokamilika kiafya, pia vitu kama maji salama, huduma za afya, shule, usafiri na vinginevyo ilikuwa ni simulizi kwa maisha yake.

Mlalahoi alikuwa akipata maji katika mitaro ya mafuriko ya maji huko mijini na vijijini, alikuwa akipata maji katika vidimbwi vilivyokuwa vikibaki na maji, hasa maji ambayo walikuwa wakishirikiana na wanyama wa porini na wale wa kufugwa.

Mlalahoi wa kweli nyakati hizo alitafsiriwa kama mtu ambaye anazijua na kutibiwa na tiba mbadala zaidi kuliko tiba za kisasa, mlalahoi alizijua dawa nyingi za mitishamba tofauti na yule ambaye hakuwa mlalahoi.

Suala la shule kwa mlalahoi, hasa watoto wake, lilikuwa si la kujua sana, watoto walimaliza darasa la saba wakiwa hawajui kuandika. Shule za watoto wa walalahoi zilikuwa zikijulikana na zikapewa majina maalumu ya kuudhi.

Shule zile zilikuwa zinaweza kujitofautisha na shule za kweli za kusoma kwa kuangalia watoto jinsi ambavyo wanawajibika, wakati wetu wakibeba mifagio, makopo na vizibo vya soda, zile zingine walikuwa wakibeba vitabu na sharubati na kufuatwa na mabasi.

Kuna sababu nyingi ambazo zilisababisha kuwa na tofauti hiyo, lakini ilikuwaje? Baadhi ya viongozi walikuwa hawawajibiki kwa wananchi, viongozi wengi walikuwa kama wafalme na wlinunua madaraka kwa bei ndogo na kuamua kutudharau wapiga kura, walikuwepo viongozi ambao walitengeneza mfumo wa utawala utakaowaweka madarakani kwa kadiri wapendavyo, lakini kibaya zaidi waliamua kuwa machifu wa kuwaachia madaraka watoto au ndugu zao.

Kwa wakati ule matumaini yetu yalikuwa mikononi mwa mikono ya huruma tu ya kiongozi anayetawala wakati huo, tulikuwa na viongozi ambao kila siku wapo safarini hadi wakati wa uchaguzi utakapowadia, walikuwepo ambao walikuwa wakishinda kwenye vikao vya kutengeneza dili na vikao vya kunywa, huu ni ukweli unaouma lakini ni lazima tuukumbuke.

Wakulima tulisubiri pembejeo kama zawadi wakati tukizinunua kwa bei ya juu na tulikuwa hatupati kwa wakati, wakulima tuliwaona maofisa ugani wakiwa katika magari yao ya kifahari na walikuwa mara nyingi wanafanya utafiti huku wakiwa ndani ya suti, walikuwa ni mwiba sana kwetu, walikuwa maofisa ambao hawakusogelewa na watu wachafu, hawakujali mazao yetu wala kilimo cha mazao yetu, kwa maana ya masoko. 

Hali kadhalika wafugaji waliswaga mifugo yao iliyokuwa na afya mbaya kwa kukosa dawa za minyoo na kukosekana kwa majosho, waliishi kwa kutembea na mifugo mingi badala ya kuishi mahali pamoja na mifugo michache inayofugwa kisasa, maofisa waliokuwa wanahusika na jambo hilo walikuwa katika vikao na kufungua maduka ya dawa za mifugo na kuziuza kwa bei isiyo elekezi, hii ndiyo ilikuwa fimbo kwa mlalahoi mfugaji. 

Wafanyakazi wa serikali nao si kweli kwamba walikuwa hawamo katika kundi hili, wachache waliopewa madaraka walikuwa miungu watu na walitumia muda wao kujinufaisha badala ya kuifanyia kazi jamii ya Watanzania ambayo kimsingi ndio walikuwa waajiri wao, hiki ni kipindi ambacho mfanyakazi alikuwa akipata mshahara anadumu nao usiku mmoja na siku inayofuata anaanza kukopa, ni maisha magumu sana.

Kundi la wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama ‘wamachinga’ ilikuwa ni zahama nyingine mpya, ni kama vile walikuwa waajiriwa wa wale walioitwa wafanyabiashara wakubwa, nao walikuwa walalahoi tu kwa kufanya kazi kama madalali badala ya wamiliki halisi wa biashara zao. 

Najiuliza, sasa hivi ulalahoi tulionao ni upi? Wote tunafanya kazi lakini malipo yanafanana? Shule zinasomesha lakini watoto wanaelewa? Ufalme upo tena? Au ndiyo kumtafuta mchawi na wadogo wanazidi kuumia? Vipi kuhusu maji? Yapo lakini wanapata? Dawa je? Umeme? Usafiri?

Huenda tupo katika kipindi cha maradhi ya kuugulia maumivu ya mabadiliko, kila la heri mlalahoi yule unayepitia maumivu makali.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share