Ndugu Rais, umebarikiwa wewe kwa sababu unatambua uwepo wa ukweli. Wakati wengine wakisema ukweli unauma, wewe umeihubiri kweli bila kuchoka. Mwenyezi Mungu akuimarishe ili uiishi hiyo kweli. Kweli ni dhahiri yaani bila uongo. Yako mengi yaliyosemwa juu ya kweli. Kamusi kuu ya Kiswahili imeandika, “Ni vizuri kusema ukweli hata kama utasababisha madhara kuliko kusema uongo”.

Wacha Mungu wanasema, “msemakweli mpenzi wa Mungu”. Akidhihirisha nguvu kubwa ya kweli, marehemu Shaaban Robert anasema, “Kweli itashinda kesho kama leo haitoshi”. Ni imani tu ya sisi wanao kuwa, kwa sababu tu ya kwamba wewe ndiye baba yetu kwa sasa katika nchi hii, ukweli wa kifo cha mtumishi wako Akwilina Akwilini unapaswa kuujua wote!

Nakiri Akwilina sikumfahamu! Pia, wananchi wengi sana hawakumfahamu Akwilina kabla ya kifo chake. Akwilina hakuwa Mtanzania maarufu. Isitoshe hakuwa kati ya wale watu wachakarikaji ambao mtu hulazimika kumfahamu kwa makeke yake tu. Lakini Akwilina kifo chake kimempatia umaarufu mkubwa sana. Nayaona mageuzi makubwa mbele yetu sababu ya kifo hiki! Ile namna Akwilina alivyouawa iligusa nyonyo za Watanzania wengi sana! Serikali kwa ushiriki wake wa nguvu kubwa katika mazishi yake ilijizolea maswali mengi ambayo wananchi bado wanasubiri majibu. Hii ilikuwa ni bahati mbaya kwa sababu huko mbele yanaweza yakawa ushahidi.

Hadi leo kuna watu bado wamejawa simanzi kwa kifo cha Akwilina. Hata hivyo, pamoja na kwamba msiba hausahauliki, lakini kadri siku zinavyozidi kusonga mbele baadhi ya machungu huonekana kupungua au kupotea. Cha kuzingatia ni kujaribu kuyakwepa yote yanayoweza kukumbusha juu ya huo msiba na hivyo kukurudishia msiba upya. Na kwa sababu hiyo tunasema ni vema tukajaribu kadri tuwezavyo kuyaepa yote yanayoweza kutuletea majonzi mapya kwa kifo cha Akwilina.

Baba, yaliyomo katika vifua vya wananchi ni kama walivyokuwa wanaambiwa tangu siku Akwilina alipouawa; Kuwa alipigwa risasi na polisi waliokuwa wanawatawanya waandamanaji. Alipigwa risasi na kuuawa akiwa ameketi kitini ndani ya daladala! Akwilina hakuwa kati ya waandamanaji wala hakuwa sehemu ya maandamano yale! Zaidi ya hayo hata daladala yenyewe aliyokuwamo Akwilina haikuwa sehemu ya maandamano yale!

Ndiyo kusema kama kuna watu ambao walisababisha maandamano hayo hawawezi tena kuwa ndiyo waliosababisha mauaji ya watu ambao hawakuwa sehemu ya maandamano yale. Baba, kupiga risasi ndani ya basi la daladala lililosheheni abiria ndiyo kunako leta hukumu! Hakuna mwelewa anayeweza kusema lengo lilikuwa ni kuwatawanya waandamanaji. Ndani ya daladala abiria wanaweza kuandamana vipi, hata kama wangetaka kufanya hivyo? Ni polisi waliowaambia wananchi kuwa polisi kadhaa walikuwa wanashikiliwa kuhusiana na mauaji hayo. Baadaye wakaambiwa hawajamwona aliyemuua Akwilina, faili likafungwa. Wananchi kwa unyonge wao hawakuwa na la kufanya, bali kumshitakia Muumba wao! Ah! Inauma sana tukiwaunga mkono! Kuhukumu siyo kazi yetu, tumwachie Muumba! Lakini ombi lao wanao kwako baba wanasema, kwa kuwa Akwilina ameishauawa na aliyemuua hajulikani, basi wanaomba aachwe apumzike kwa amani! Lakini hilo ni ombi tu kwako baba kutoka kwa wanao. Si kama ni lazima ufanye watakavyo wanao, bali mapenzi yako yatimizwe!

Baba sisi wengine tunaojichanganya na wananchi huku mitaani na vijijini ndiyo tunajua kiwango cha joto wanalokuwa nalo wananchi kila jambo kubwa katika nchi linapowagusa. Ndiyo maana tunasema wanaoanza upya kumtajataja Akwilina hawatutakii mema. Hakuna faida tutakayoipata kwa kujaribu kulitumia jina la Akwilina kwa njia yoyote ovu.

Kujiingiza katika mradi wenye madhara mengi kuliko faida, wa kuwatafuta wengine badala ya kujitafuta wenyewe eti ndiyo waliosababisha Akwilina auawe kwa kupigwa risasi ni kuzidi kuwajaza hasira wananchi dhidi yetu! Inaweza kuwa siyo sasa, lakini huko tuendako tutakuwa tumejikusanyia hasira nyingi za wananchi kwa jambo hili.

Tutakapokabiliana na hukumu ya wananchi wenye hasira kali ndipo tutajua kuwa majuto ni mjukuu, lakini tutakuwa tumechelewa. Mpaka hapa wauaji wamekwishajulikana mbele ya wana wa nchi. Kujaribu kuwatafuta wauaji wengine, tunajiumiza wenyewe kwa sababu tunawajaza wananchi hasira dhidi yetu wakituona kama vile tunawadhania kuwa ni wajinga.

Haya yote baba yangeweza kufunikwa kwa sanda nyeusi na kuyafanya yasionekane japo kwa muda. Tuliona ilipotangazwa kuwa faili la Akwilina limefungwa, mapigo ya mioyo ya wananchi wengi, yaliongezeka.

Hii ilidhihirisha kuwa wananchi wengi walikubaliana na waliosema mwenye uwezo wa kulifunga faili la Akwilina kama ilivyo kwa mafaili yetu wote, ni Mwenyezi Mungu peke yake! Walisema aliyelifunga hakujua atendalo! Ameyafunga makaratasi yaliyoandikwa na wenzake kama kazi ya mikono ya wanadamu. Mwenyezi Mungu ana faili la kila mja wake ambalo si la makaratasi na siyo kazi ya mikono ya wanadamu. Na kwa sababu ya mafaili hayo hakuna nafsi kati yetu itakayokosa kuionja hukumu ya Mwenyezi Mungu! Kila mja wake atakwenda kwa wakati wake kusimama mbele ya haki. Muumba wake atamhukumu kila huyo akiwa amesimama peke yake.

Hukumu ya Yeye Muweza wa yote haihitaji ushahidi. Kwa Mwenyezi Mungu ushahidi dhidi yako, unakwenda nao mwenyewe! Aliyemuua Akwilina mwenyewe anajijua kwa sababu tangu siku ile amezongwa na nafsi yake!

Furaha aliyokuwa nayo kifuani mwake haitofautiani na majuto, akiijutia kazi yake. Baba kwa wengine haya walidhani yamekwisha nao walimwachia Muumba wao kwa hukumu. Sasa haya ya kuwatafuta watu wengine na kusema wao ndiyo waliosababisha Akwilina auawe kwa kupigwa risasi yanatoka wapi?

Tusipokuwa makini hapa ndipo kama mbwa tunajipeleka wenyewe kwenye mdomo wa chatu. Kama kuna wabaya wetu tunayo mengi ya kuwashitaki kwayo. Hili la Akwilina tuliondoe kwa sababu linatukusanyia sisi hasira nyingi kutoka kwa wananchi bila sababu. Wewe utakuwa ni mtu gani katika jamii ambaye kila utokeapo hadharani, watu wanakutema mate? Lakini ni hili ndilo linalowavutia huruma ya wananchi, na kutufanya sisi tuonekane kama watu katili tuliokosa mfano wake! Kuzitumia jitihada ovu ni kuzidi kujichafua! Baba Akwilina amekwisha uawa, kwanini tusimwache apumzike kwa amani?

 

2549 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!