Ndugu Rais tumejitoma katika vita dhidi ya dawa za kulevya. Ni kwa bahati mbaya sana vita yetu hii imeanza kwa kuzua zogo kubwa katika nchi. Watu wamevurugana na kugawanyika. Vita inayopiganwa na wapiganaji waliogawanyika haijawahi kushinda popote duniani. Kama tunadhani nchi yetu ni ya muujiza tusubiri tuone kama jua litachomoza kutoka magharibi!

Sheria ya vita duniani ni moja- kushinda au kushindwa. Tuna uzoefu wa vyote. Tulipigana vita ngumu ya Kagera tukashinda kwa sababu katika vita ile Watanzania tulikuwa kitu kimoja. Tulipigana kuitetea nchi yetu na kuutetea utu wetu uliokuwa umedhalilishwa na nduli Iddi Amin Dada. Tulikuwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, lakini katika kupigana Watanzania wote tulipigana. Kwa moyo ule nina hakika hata kungekuwako na vyama vingi bado visingeuteteresha msingi wetu mkuu wa upendo, umoja na mshikamano! Tulipigana kwa lengo na nia njema! Inauma sana kusema moyo ule sasa haupo! Umekwisha kwenda! Umekwenda na viongozi wema waliotuongoza badala ya kututawala! Wamebaki waheshimiwa wanaotutawala badala ya kutuongoza!

Manabii wa uongo waliipiganisha nchi kwa miaka zaidi ya mitatu vita hewa dhidi ya ufisadi wakashindwa. Wapiganaji wa vita ya vua gamba walishindwa kwa aibu kubwa inayowaandama mpaka leo! Vita hivi vilishindwa kwa sababu pamoja na maneno ya kuvutia, lakini nia ilikuwa ovu! Hii ya dawa za kulevya inafanana na vita ipi hapa?

Ndugu Rais, tukupongeze kwa kumteua Rogers Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya. Bila kukurupuka hapa ndipo tulipotakiwa kuanzia vita hii dhidi ya dawa za kulevya na siyo kule tulikoanzia. Vita dhidi ya ufisadi na ile ya vua gamba havikufaulu kwa sababu vilibeba sura ya chuki binafsi na hivyo vikaonekana ni vita vilivyobuniwa na watawala wabovu wachache kwa maslahi yao au kundi lao. Na hiyo ndiyo picha iliyokujanayo vita hii ya dawa za kulevya. Kwa historia yetu vita hii isingeshinda, bali ingeishia kuleta vurugu kubwa katika nchi! Baba hongera!

Ndugu Rais, umesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa hajui kama yeye ni Mwenyekiti wa Baraza la Kudhibiti Dawa za Kulevya kama ilivyobainishwa kwenye sheria. Na kwamba hata mawaziri wake ambao ni wajumbe wa Baraza hilo walikuwa hawana taarifa. Ukamtwisha msalaba wake Waziri Mkuu wa kuongoza mapambano haya mpaka Golgota! Mtu sahihi kwa kazi sahihi!

Ulipoendelea na kusema hata wewe hukuletewa mapendekezo ya kumteua Kamshina Mkuu wa Mamlaka hii ukanikumbusha ujumbe niliotumiwa kutoka kwenye namba 0755030451 ambayo usajili wake unaonesha ni ya Gerand Hando ambaye simjui, kuwa: “Hivi unapoandika unatumikishwa na TISS au Idara gani? Maana yake naishi na maofisa wanne kwangu wa Usalama wa Taifa. Nalisoma JAMHURI kwa sababu yako tu. Nasoma Tanzania Daima kwa sababu yako tu. Umetoa ushauri mwingi kwa Rais wangu ambao hautafanyiwa kazi. Acha kumshauri Rais!”

Baba, huyu hataki wanao tukushauri ili uharibikiwe na nini? Anaotaka wakushauri si ndiyo hawa ambao hawakukuletea mapendekezo ya kumteua

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za kulevya! Limewashuka kwa sababu walidhani bila mapendekezo yao, utapuyanga! Huyu anayejidai kuishi na maafisa Usalama wa Taifa wanne na hawa ambao hawakukuletea mapendekezo, wanakumulika mchana. Wahenga walisema, “Akumulikaye mchana usiku atakuchoma”. Nakushauri, wachunge sana!

Baba ubarikiwe sana pale uliposema: “Lazima tuwe wakweli, tusijifanye malaika kwa kuficha ukweli!” Tukiri kuwa tulipungukiwa busara na hekima na kwa kuwa tulikosa weledi tuliianzisha vita hii kubwa, kitoto!

Kama aliyeanzisha vita hii alijua kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa hajui kama yeye ndiye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya kama ilivyobainishwa kwenye sheria, kwanini hakumtaarifu?

Watakaosema tuliamua kuianzisha vita hii ambayo haikuwa na hadhi yetu, bali hadhi ya Waziri Mkuu, kuwa lengo letu lilikuwa ni kujitafutia ujiko huku tukiufahamisha umma kuwa Waziri Mkuu wetu alikuwa hajui majukumu yake, tuwakatilie vipi? Tulikurupuka!

Mwanamwema Sianga ametangaza kuwa kama mtu ametajwa, lakini ikabainika aliyetajwa hahusiki, yule aliyemtaja kama amembambikia tutamchukulia hatua kwa sababu hatutamwonea mtu. Kuna watu wanatoa majina kwa nia ya kuwakomoa watu.

Heshima ya kiongozi ni kuyaishi matamko yake mema! Sianga anza kwa kusafisha wapiganaji wako waliokwishatajwa. Hadhi ya Kamanda Simon Siro katika vita hii ni kubwa. Kwa kuwa alikwishatajwa msafishe kwanza kwa kumchunguza ili ikithibitika kuwa aliyemtaja alimbambikia, basi aliyemtaja achukuliwe hatua kama ulivyowaahidi wananchi upate kulinda heshima ya Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya na wewe mwenyewe! Kazi takatifu haiwezi kupiganwa na watu ambao tayari wamekwisha pakwa uchafu.

Ndugu Rais, kuna vikundi vimejiingiza katika uongozi wa nchi, lakini havitambuliwi na katiba ya nchi. Vikundi aina hii ni vya kihuni hata kama vingine vinatumia heshima ya dini zetu! Kuvishirikisha katika vita hii takatifu ni kuinajisi vita yenyewe! Walewale waliosema aongezewe ulinzi sasa wanamkana na kusema; “Hatukumtaja Freeman Mbowe, tulitaja Billicanas.” Tatizo hapa ni hawa waliosema walitaja Billicanas na siyo Freeman Mbowe au ni yule aliyemtaja Freeman Mbowe badala ya Billicanas aliyotajiwa?

Hivi ni vikundi kama vua gamba na wale manabii wa uongo vilivyotengenezwa na baadhi ya viongozi wabovu wachache waliopita.

Uhuni ni sifa apewayo mtu anayefanya mambo ya kihuni bila kujali kama mtu huyo ni Bwana Shamba, Sheikh, Askofu au muuza mkaa! Wanachosema ni kwamba wao walikata mkia kutoka kwa mbwa, lakini hawakumkata mbwa!

Baba kukataa kukutana nao uliongozwa na Roho wa Mungu! Akujalie ujasiri wa kufuta mabaki yote ya vikundi vya kishetani vilivyotengezwa na tawala zilizopita!

Ndugu Rais, tusimlaumu mtu tumsaidie kwa kumshauri akae pembeni. Na kama kuna aliyemtuma tumwombe ampangie kazi nyingine! Malumbano yametamalaki kati ya aliyetaja na waliotajwa. Mtajaji anashutumiwa kwa kutomtaja kimwana wake. Mtajwa mwingine anakiri ni mwenzake kibiashara. Baadaye kimwana anawapelekea wenzake meseji; “Imeishakuwa soo nakwenda central kuhojiwa.” Uadilifu uko wapi? Zikishinda kesi zote hizi zinazofunguliwa, sijui nchi itabaki na nini!

1970 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!