Ndugu Rais, huku mitaani wananchi wako wanasema wewe ni mkali sana.
Wakati mwingine tunaonekana tukiongea kwa ukali na kufokafoka tu bila sababu za msingi kiasi cha kuwatia watu wetu kichefuchefu na wengine kuwafanya wajisikie hadi kizunguzungu. Lakini kwa ufisadi mkubwa uliofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kuwapelekea watoto wako shuleni vitabusumu, kwa hakika, wameigusa mboni ya jicho lako! Kwa hili ukali wako ni muhimu sana.
Onesha ukali wako hapa baba kama kweli tunataka kuinyosha nchi.
Tumesoma katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu kuwa Mwalimu Mkuu -Ngowe Boniface alikuwa mkali sana kiasi kwamba alipomkazia mtu macho yake, alitisha kama simba. Lakini alipendwa sana na wanafunzi wake wote, walimu wenzake wote na wananchi wote walioishi jirani na shule yake. Haikuwa kawaida kwake kutoa adhabu, lakini alipolazimika wanasema adhabu ilikuwa kali na ilitisha kama nini!
Ndugu Rais, si busara kuzipuuza habari kwa kigezo tu kuwa ni za mitaani. Unaposema hizo ni habari za mitaani tayari unakiri kuwa hizo ni habari. ‘Uhabari’ wa habari hautokani na kule inakotoka. Hivyo mwanamwema aliponiambia kuwa; “Mwalimu Mkuu, kuna tofauti ndogo sana kati ya neno Bunge na neno Bangi, ukitaka kuthibitisha hilo nenda Dodoma”; ilinifikirisha sana, lakini sikulipuuza. Nilijiwa na fikra kuwa, kama maneno hayo yasingekaribiana kwa maana yoyote ile, Bunge letu lisingepitisha bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi mpaka pale ambako lingehakikishiwa kuwa vitabusumu walivyopelekewa watoto wa masikini shuleni vikawaharibu, vimekwisha ondolewa katika shule zote! Ana heri mwanamwema yule aliyesimama bungeni kwa ujasiri na kusema anaishikilia shilingi katika mshahara wa waziri mpaka waziri atakaposema hatua zitakazochukuliwa. Waziri hakuwa anajua achukue hatua zipi.
Hatua ambayo ingekuwa ya kwanza ilikuwa ni waziri kuamuru vitabusumu vyote viondolewe shuleni mara moja. Unafanya uchunguzi huku sumu ikiendelea kusambaa mwilini, ndiyo akili gani? Rais mara nyingi unasema; “Unachunguza nini, meno ya tembo anayo mkononi, au unataka rushwa?”
Waziri Joyce Ndalichako na Katibu Mkuu wake wanataka kukuambia ndugu Rais kuwa ufisadi wa kutisha kama huu na wenyewe wameujulia bungeni?
Kwanini hawakuchukua hatua mapema? Waziri Ndalichako alipokataa kuwasikiliza viongozi wa wachapishaji walipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kumweleza juu ya ufisadi huo, alikuwa anaifukuza bahati au alikuwa anajua kilichokuwa kinaendelea kuwa ni cha kwake? Kuchukua hatua baada ya shilingi kutoka katika mshahara wake kung’ang’aniwa bungeni, kumemwonesha kuwa angalau kwa hili hakuwa mtendaji wa kuendana na kasi yako Ndugu Rais. Kama hawahusiki, basi wamekosa vigezo vya kuwa wasimamizi kwa ngazi walizonazo. Baba onesha ukali wako hapa wananchi wako wajue kuwa kweli umedhamiria kuinyosha nchi.
Ndugu Rais vitabusumu hivi havirekebishiki. Kama zilivyo dawa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu; ni vya KUCHOMA MOTO! Tumekuwa tukikuhurumia baba, tunapokuona unavyohangaika huku na huko kutafuta fedha ili watoto wa masikini wasome bure. Mabilioni uliyokusanya kwa ajili hiyo yawe ya serikali au ya wafadhili, yaliyotumika kuchapisha mpaka kusambaza vitabusumu hivi, sasa yanaenda kuchomwa moto! Kama ni wafadhili, sijui watauelewaje utawala wako. Hawa, wameigusa mboni ya jicho lako! Baba, hakuna namna, ukali wako hapa, utawaaminisha wananchi kuwa kweli dhamira yako ni kuinyosha nchi!
Waziri Ndalichako aliambiwa ofisini kwake kuwa baadhi ya viongozi waliomtangulia walikuwa mizigo walioifisadi elimu ya nchi hii! Walipoona wameshindwa kufaulisha wanafunzi walifanya ujinga wakapanua milingoti ya magoli. Aliporudisha milingoti ya magoli mahali pake alionesha dhamira yake njema ya kuirudisha hadhi ya elimu katika nchi yetu. Wananchi walishikamana naye. Na katika kumtia moyo tukamwambia jitihada zake ndizo zilizomwezesha binti yangu kupata division one.
Ndugu Rais, si bungeni au nje ya Bunge – hakuna popote waziri alipoahidi kuviondoa vitabusumu hivyo kutoka shuleni. Sumu inaendela kusambaa. Watoto wa masikini wanazidi kuathirika! Haitashangaza kuona yaliyotamkwa bungeni kuhusu vitabusumu hivyo yakawa yameishia bungeni.
ESCROW, LUGUMI na ufisadi mwingine vimeishia wapi? Tuliokulia maisha ya shida tunazijua baadhi ya dawa za mbu ambazo ukipuliza chumbani, mwanzoni utadhani mbu wote wamekufa kumbe wamelewa tu. Baada ya muda hurudi na kuendelea kushambulia. Wako wabunge waliozungumza kwa uchungu mkubwa kama walivyozungumza juu ya ufisadi mwingine kama ESCROW na LUGUMI, lakini leo hata hawajui yameishia wapi.
Ndugu Rais, ufisadi ulianza kwa kuivunja EMAC ambayo ilikuwa ndiyo chujio la kuchuja vitabu. Kitabu kilichopita katika matundu ya EMAC kilikuwa kitabu bora shuleni. Hivyo hata vingepitishwa vitabu 10 kuwa vya kiada lazima vingekuwa vinafanana kwa ubora kitaaluma kwa maana vyote vimepita kwenye chujio lile lile! Walipoongeza hoja kuwa kiwepo kitabu kimoja tu cha kiada kwa shule zote nchini ndipo walipoibua hisia kuwa hawa walikuwa wamemtayarisha mtu au kampuni au njama ya kuchapisha kitabu hicho. Walijua wakiwaachia wachapishaji kushindanisha vitabu vyao, cha kwao hakitaweza kushindana kwa ubora. Hii imethibitishwa kwa haya yaliyotokea sasa.
Ilishangaza kusikia wizara inakusanya watu eti waandike vitabu! Ulafi ukimfunika mtu humtoa ufahamu. Iweje Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wasiwe na ufahamu wa kujua kuwa uandishi ni sanaa? Sanaa ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa maandishi, michoro au uchongaji! Hivi ni vipaji, mtu hasomei. Huzaliwa nacho. Kukusanya watu waandike vitabu mpaka vya watoto si sahihi kabisa. Ni uroho tu wa fedha kwa baadhi ya wenye uamuzi kutaka kujinufaisha kwa njia za semina, warsha na marupurupu mengine.
Ndugu Rais, uchapishaji ni taaluma. Wachapishaji wa Tanzania wameifanya kazi hii kwa weledi na umahiri mkubwa kwa miongo kadhaa kiasi cha kuwavutia hata majirani zetu kama Malawi kuja kuona mfano. Lakini watu wameingiwa na tamaa ya mali hata kwa gharama ya elimu ya wana wa masikini wa nchi hii! Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alituambia tunao maadui watatu, lakini UJINGA ndiyo kiongozi wao. Ndugu Rais, iokoe elimu ya nchi yetu tutakupa ushirikiano. Hawa wamekujaribu, usikubali kujaribiwa! Anza na hawa kuinyosha nchi na Mungu atakusaidia!

1195 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!