NEC itekeleze agizo la Waziri Mkuu

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutenda haki katika kutangaza washindi wakati wa uchaguzi.  

Majaliwa ameyasema hayo Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devotha Minja, wakati wa kipindi cha ‘maswali kwa Waziri Mkuu.’

Minja akatoa mfano kuwa uchaguzi mdogo uliofanyika katika kata 43 Novemba mwaka jana, ulionekana kuwa na dosari nyingi akidai Chadema ilihujumiwa kutokana na NEC kuwatangaza wagombea wa udiwani kadhaa kupitia CCM kuwa washindi licha ya kuwa walishindwa kwa kura nyingi.

Tunalazimika kuunga mkono tamko la Waziri Mkuu Majaliwa na kuisihi NEC na wadau wengine kutekeleza wajibu wao ipasavyo hasa katika kuwatangaza washindi wa uchaguzi, ili matokeo husika yasiwe chanzo cha mifarakano.

Suala la uchaguzi huru linagusa maeneo na wadau wengine wakiwamo wanasiasa, polisi, wasimamizi wa uchaguzi, japo kuwataja kwa uchache.

Kwa hali hiyo, tamko la Waziri Mkuu Majaliwa linaweza kuvuka mipaka ya NEC na kuwahusisha wadau wakiwamo tuliowataja hapo awali, na tume hiyo ikabaki kuwa mratibu katika kuhakikisha mshindi anayetokana na kura nyingi, ndiye anayetangazwa.

Mathalani, kama wanasiasa watashindwa kutumia hoja zenye ushawishi ili waungwe mkono na kupata kura nyingi, badala yake wakashirikiana na wadau wengine kupanga na kutekeleza njama za kuuhujumu uchaguzi husika, haipaswi kuvumilika.

Ama kama polisi watakubali kutumika kwa namna yoyote, na mdau yeyote katika uchaguzi unaofanyika nchini, kusimamia na kuuhujumu uchaguzi husika, hawatapaswa kuvumiliwa.

Ndivyo inavyopaswa kufanyika kwa wadau wote, kwa maana uzoefu unaonesha kuwa uchaguzi ni miongoni mwa vyanzo vikuu vinavyosababisha na kuchochea vurugu na mifarakano kwa jamii.

Tanzania imewahi kushuhudia machafuko yaliyotokea Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, na kusababisha raia wa nchi hii kukimbilia kwenye kambi ya wakimbizi Shimoni nchini Kenya.

Kadhalika, kumekuwapo vurugu katika chaguzi kadhaa, hata kama zikiwa katika kiwango kidogo, lakini zinaathiri taswira ya nchi, mahusiano na amani ya nchi. Tanzania isiyokuwa na migogoro inayotokana na matokeo ya uchaguzi, inawezekana.

Tunarejea kuisihi NEC, irejee na kulitumia agizo la Waziri Mkuu Majaliwa kama mwongozo wa kuliweka Taifa katika hali ya amani, umoja na mshikamano kwa kuwatangaza washindi halali wa uchaguzi na si vinginevyo.

Uchaguzi wowote wa viongozi na wawakilishi wa wananchi nchini, unawahusisha raia wa Tanzania wenye sifa zinazotambuliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Hivyo, Watanzania wanaposhiriki uchaguzi ili wachaguliwe na Watanzania kuwaongoza ama kuwawakilisha, isiwe chanzo cha mifarakano katikati yao na namna ya kuepukana na hatari hiyo ni kwa NEC kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Majaliwa.