Neno la Pasaka kutoka kwa Askofu Bagonza

IJUMAA KUU – KANISA KUU LUKAJANGE 2019

MATHAYO 27: 27-31, 39-40

“Ndipo askari wa Liwali wakamchukua Yesu ndani ya Proitorio,* wakamkusanyikia kikosi kizima. Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhiaki, wakisema: ‘Salaam, Mfalme wa Wayahudi!’ Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga – piga kichwani. Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulubisha.

Nao waliokuwa wakipita njiani, wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, wakisema: ‘Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe mwana wa Mungu, shuka msalabani’.”

Wapendwa katika Bwana, Neema na iwe kwenu, na Amani itokayo kwa Mungu Baba, na kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo – Amina.

Leo ni siku ya kukumbuka mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Tendo hili ndio msingi wa imani ya Kikristo. Katika somo la siku ambalo nimesoma sehemu yake, tunasikia maelezo marefu sana kuhusu mateso ya Bwana Yesu. Katika somo la pili (Mt. 16) tunasikia Bwana Yesu akimkatalia Petro anapojaribu kumzuia asiteswe. Alitaka kumwepusha msalaba. Na kwa kweli ya kibiblia, alitaka kuzuia ukombozi wetu.

Sisi wanadamu hatupendi mateso, tunapenda kutesa watu wengine. Kukwepa mateso ni ishara ya ushupavu na ujanja, na yule anaye yaendea mateso kwa moyo mkunjufu anaonekana mjinga. Ndugu zangu naomba mpaka hapa tuelewane: Yesu alijua mateso ni lazima ili ukombozi upatikane lakini hilo halitoi ruhusa kwa wanaotesa wenzao. Kumtesa mtu ati kwa sababu na Yesu aliteswa ni uzushi wa kiimani, kwa sasa unamfanya mtu huyo kuwa Yesu ambacho ni kinyume cha amri: Usitengeneze sanamu na kuiabudu. Na hii mara nyingi watesaji hawaijui. Kwamba, wanawaabudu sana wale watu wanaokuwa wanawatesa. Utesaji ni kama bangi, ukiishaingia mwilini unajenga mazoea ya kupenda kutesa tesa watu hata bila sababu!

Yako maelezo mengi juu ya nini kilitokea siku hiyo ya Ijumaa. Ni zaidi ya miaka 2000 imepita, lakini ndugu zangu, Wakristo na Watanzania wote, tendo bado linasumbua Imani za watu wengi. Sisi Wakristo, tunaamini kwa dhati kuwa tendo hili linasimama katika misingi miwili mikuu ya kibiblia:-

Upendo: Kwamba Mungu aliupenda ulimwengu na watu wake, hata akamtoa mwanae wa pekee Yesu Kristo ili afe/ awe sadaka/ badala/ kwa niaba/ na kwa ajili yetu.

Kwamba, Yesu afe badala ya sisi kufa kwa dhambi zetu,

Kwamba, Yesu afe kwa niaba yetu kwa ajili ya dhambi zetu,

Kwamba, Yesu afe kwa ajili yetu, kwa sababu ya dhambi zetu. Maneno haya: badala, kwa niaba, na kwa ajili – yanasisitiza UPENDO wa Mungu kwetu. Kwamba, yeye alitupenda sisi kuliko hata mwanawe Yesu Kristo. Huu ni upendo wa ajabu – wa kutoa – siyo kupokea. Tumezoea kupokea kama ishara ya upendo, yeye Mungu alitoa kuonyesha upendo wake!

Upendo wa MUNGU kwetu ndio uliomweka Yesu msalabani – hata kama angekuwa yeye binafsi hataki – Baba yake alitaka na yeye akatii. Upendo wa Mungu, siyo misumari – ndio ulimshikilia Yesu msalabani. Kwa misumari tu, angeweza kudondoka kwa maumivu. Upendo ndio uliombakiza msalabani mpaka anakata roho.

Upatanisho: Wapendwa watu wa Mungu, dhambi tuliyotenda ilileta uhasama kati ya wanadamu na Mungu. Ili kurejesha uhusiano huu uliopotea bustanini Edeni, hatua mbalimbali zilifanyika awali na kushindwa kurejesha uhusiano mwema na Mungu.

Kuteswa na kufa kwa Yesu, ni kafara halisi ya kukomesha dhambi. Badala ya kuku, ng’ombe, kondoo, nyoka, albino, wenye vipara, wafupi n.k. Yesu alikufa ili awe kafara ya kweli kuokoa wanadamu lakini pia hata uumbaji wake.

Kabla ya hapo, Adhabu – moto, maji, utumwa, vyote vilishindwa – uhasama ukabaki. Ndipo Mungu akamtoa mwana wake awe sadaka moja na kamili. Afe ili sisi tupone! Kwa njia hii Mtume Paulo anasema: “Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake”. Sasa ndugu zangu sijui kama mnapata picha hapa?!

Kwamba, ndani ya Kristo alikuwemo Mungu.

Alishuka akawa mwanadamu ili atupate kirahisi.

Hakupenda kusubiri ili sisi wenye dhambi twende kutubu au kuomba radhi.

Alishuka akiacha ubaba, utukufu, enzi, mamlaka – akafa msalabani kama mhujumu uchumi, kama mhalifu, kwa ajili yetu.

Alibeba dhambi zetu na kuonekana ni mhalifu.

Akakamatwa, akashtakiwa na kuhukumiwa.

Alipochukua dhambi zetu – sisi tukawa watakatifu (tulibadilishana) yeye akawa mtumwa – sisi tukawa mabwana! Yote hayo ili tupatane naye. Na mpaka hapa hakuna lolote ambalo mwanadamu amechangia ili kujikomboa

Dhambi katenda yeye.

Hakwenda kutubu.

Mungu kashuka ili kumtafuta mwenye dhambi.

Mwenye dhambi akamgeuka mkombozi na kumuua.

Tunajifunza nini katika upendo huu na upatanisho huu?

1.  Tupendane kwa sababu wote tu watumwa tuliokombolewa. Tufurahie ukombozi, tuuchukie utumwa. Tusitamani kurudi huko. Tuishi maisha ya shukrani kwa mkombozi wetu. Jamani, wewe umeiba. Umekimbia na kupotea. Kakamatwa mwingine. Anahukumiwa na kuuawa. Wewe unaangalia tu na kuchekelea?

2. Tujitoe kwa ajili ya wengine (volunteerism)

Kujitolea na kujitoa ni mambo yanayozidi kupotea ndani ya Kanisa na taifa. Kila kitu ni fedha!

– Tujitoe (mali, wakati, vipawa).

– Tujitolee (nafsi zetu) ili kulitumikia Kanisa na Taifa.

Kujitoa na kujitolea ni ibada kamili. Vikifanyika kwa usahihi na mwongozo ama wa uzalendo au kibiblia, vinaongeza thamani ya utu wetu na thamani ya uumini wetu mbele za Mungu. Bwana Yesu alitoa damu yake isiyo na hatia ili kutukomboa. Nakumbuka nikiwa kijana wa shule ya msingi huku huku Karagwe, miaka ya katikati ya 70; tulihamasishwa kutoa damu ya kwenda Msumbiji! Fikiria, mtoto wa darasa la sita na saba, anatoa damu na kuambiwa inakwenda Msumbiji kumkomboa ndugu yake! Kabla ya kulala kwenye kitanda kutoa damu, unatamka BINADAMU WOTE NI NDUGU ZANGU NA AFRIKA NI MOJA. Mpaka leo sijasahau. Thamani ya damu katika uhusiano na upatanisho.

3. Tuonyeshe tofauti kati ya watumwa waliokombolewa na walio bado utumwani.

Watumwa waliokombolewa huwa ni watu huru, wana furaha, wanajiamini, wanachukia utumwa, hata wakiwa huru, hawafurahii kuwaona wengine wakiwa utumwani.

Lakini pia kukombolewa halafu wewe ukawa mfuga – watumwa

ni jambo la aibu mno. Siku moja Musa alilazimika kuua baada

ya kumwona mtumwa Muebrania anaonewa na Mmisri (Kutoka

2:11-12). Cha ajabu, mtumwa yule akamtishia Musa kuwa

atamshtaki kwa Farao. Musa akatoroka (Kutoka 2:15). Tabia

moja ya kuzoea utumwa, ni kupenda kubakia utumwani. Na ya pili ni kupenda kumiliki watumwa!

Ndugu zangu, ukombozi unaotokana na kifo cha Bwana Yesu msalabani, unatutaka tuwe chachu ya kupenda uhuru kwetu sisi wenyewe na kwa wengine pia. Na hapa kwa kuwa ninaongea na Watanzania wote, niseme kwa fahari. Tunu moja tuliyojaliwa kuwa nayo chini ya uongozi wa Baba wa Taifa hili, ni pale tulipotangaza kuwa uhuru wetu hauna maana kama bado kuna nchi ziko chini ya ukoloni na utumwa. Tukatumia rasilimali nyingi kuwasaidia wenzetu waondokane na ukandamizaji, ukoloni na utumwa. Sisi wa Mkoa wa Kagera, tunakumbuka kwa fahari jinsi taifa letu lilivyoingia vitani kwa gharama kubwa kupinga udikteta katika nchi ya jirani. Ulituhusu nini ule udikteta? Kwa sababu tuliona uhuru wetu hauko kamili ikiwa kuna jirani anayeteseka. Kuteseka kwa Yesu ni tamko la kukomesha mateso kwetu na kwa jirani katika nyakati zetu.

4. Tumtii aliyetukomboa – Bwana Yesu anasema: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” (Yohana 14:15-20). Aliyetukomboa na kutuweka huru anatuagiza tushike amri zake ambazo zinatuweka salama. Tukishika amri zake, tunafaidika sisi – siyo yeye bali sisi. Wako watu wanaodhani kwamba kwa kukataa kukombolewa, wanamkomoa anayetaka kuwakomboa. Ni ajabu! Hata wana wa Israeli walipokuwa jangwani wakaumwa njaa, walimgeuka Musa na kuyakumbuka makombo na masufuria ya nyama waliyokuwa wanakula kule utumwani Misri. Wakadhani wanamkomoa Musa kwa kuutukuza utumwa! Ndugu zangu wapendwa, Bwana Yesu anapoteswa na kufa msalabani kwa ajili yetu – lengo lake ni kutuweka huru sisi. Tukigoma kukombolewa, tunajikomoa wenyewe. Hatumkomoi Yesu hata kidogo. Tunaalikwa kuupokea ukombozi huu unaogharimu damu ya mwenye haki. Na kama mjuavyo, damu ya mwenye haki haimwagiki bure – isipokomboa, inaangamiza. Tuwe macho sana kwa sababu, kutukuza, kushabikia, kushiriki, kukalia kimya, au kukumbatia umwagaji damu isiyo na hatia, kuna madhara kwetu sisi na vizazi vyetu vinne huko mbele! Kazi ya damu isiyo na hatia ni kukomboa/kutakasa. Isipofanya hivyo, inaangamiza. Waweza usiangamie wewe uliyeshiriki, uliyetukuza, uliyeshabikia, uliyekalia kimya au kukumbatia. – wakaja kuangamiza uzao wako na taifa lako.

Ndugu zangu wapendwa, napenda kuwaalikeni nyote, tumtazame Yesu anayeteswa kwa ajili yetu. Tumtazame kwa makini ili kubaini nia yake. Yeye alikuwa na kila kitu. Yeye alikuwa Mungu, lakini kule kuwa sawa na Mungu, hakupenda kujivuna kwa ajili ya huo ukuu. Alinyenyekea mpaka akapatwa na mauti ya msalaba. Ameweka mfano kwetu. Tuufuate hata kama una gharama.

Hata leo hii katika Taifa letu na Kanisa letu, wanahitajika watu walio tayari kuteseka ili kupunguza mateso ya watu wengi hasa wanyonge.

Tunalia na rushwa, ufisadi, ubadhirifu, uonevu, umaskini, maradhi, ujinga n.k. Wapatikane watu walio tayari kuteseka ili kukomesha madhambi hayo. Lakini kwa hili napenda kwa unyenyekevu wote niweke angalizo: Unyonge wetu si mtaji wa wasaka tonge. Bwana Yesu hakunufaika na mateso yale. Tulionufaika ni sisi tuliokombolewa.

Kwa hiyo, wanaojitoa kutetea wanyonge, wawe makini kutotumia unyonge wetu kujinufaisha kiuchumi, kisiasa, kiitikadi na hata kiimani. Unakuta mtu anakazana kutetea wanyonge lakini ukimwangalia kwa makini, unagundua ana lake huyu. Inakuwa kama anataka tuendelee kuwa wanyonge ili apate kazi ya kufanya. Bwana Yesu alichukia unyonge wetu. Bila hivyo asingekwenda msalabani.

Wapatikane watu wakubali kuteseka na kupinga upotofu huu. Watukanwe, waitwe majina mabaya, waandikwe magazetini, watishiwe maisha, wazushiwe kila aina ya uongo, lakini waamini kuwa Mungu hawezi kuwaacha kwa sababu hakumwacha mwana wake.

Hili ndilo neno la Mungu.