Mahabusu 200 waachiwa huru

 

Mahabusu 201 waliokuwa katika magereza ya wilaya za Musoma, Tarime na Serengeti mkoani Mara wamefutiwa kesi zilizowakabili.

Hatua hiyo imekuja baada ya ziara ya ukaguzi ndani ya magereza hayo iliyofanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju; na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, hivi karibuni.

Viongozi hao na timu ya wasaidizi wao walifanya ukaguzi magerezani na kuzungumza na wafungwa na mahabusu ili kujua changamoto za kisheria zinazowakabili na kuzitatua.

Baada ya kuzungumza na mahabusu na kupitia majalada yao, DPP Mganga aliwaagiza waendesha mashtaka Mkoa wa Mara kwenda mahakamani kuzifuta kesi zilizokuwa zikiwakabili. Hatua ya kuwaachia huru itafuata baada ya Mahakama kupokea nia ya DPP ya kufuta kesi hizo kwa mujibu wa sheria.

Mahabusu 29 wanatoka katika Gereza la Wilaya ya Musoma, mahabusu 106 ni wa Gereza la Tarime na wengine 66 wanatoka katika Gereza la Mugumu wilayani Serengeti.

Katika mahabusu hao, wanawake ni 11, watoto 39, wazee ni kenda. Wengi ni vijana ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi zilizoonekana zinaweza kumalizwa nje ya mahakama, kesi ambazo ushahidi wake ni hafifu, kesi ndogo ndogo kama kupigana, kutukanana, wizi wa simu na vitu vingine vidogo vidogo, kutishiana kwa maneno, waliokiri kunywa gongo na kuvuta bangi, na wengine ambao ni mashahidi wa mashtaka.

Akizungumza na wafungwa na mahabusu katika nyakati tofauti ndani ya magereza hayo, Naibu Katibu Mkuu Mpanju aliwataka watakaofutiwa mashtaka wabadili mienendo na kuwa raia wema.

“Ndugu zangu mmeona kazi kubwa tuliyoifanya leo hii humu ndani, ni wajibu wenu kuwa raia wema na kubadili mienendo ya maisha yenu, muache kuishi kwa mazoea, muangalie mnavyoishi na mkiachiliwa mkawaambie na wenzenu. Mkivunja sheria serikali haitawaacha, lazima hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Mpanju katika Gereza la Tarime.

Naye, DPP Mganga aliwataka wote wanaopeleleza kesi zinazowakabili mahabusu wakamilishe upelelezi kwa wakati.

Amesema kuchelewesha upelelezi kunawafanya watuhumiwa wa makossa ya jinai kukaa magerezani kwa muda mrefu bila kujua hatima zao, hivyo kufanya magereza kuwa na msongamano ambao unaweza kuepukwa.

“Wapelelezi mlioko hapa, nadhani mnaelewa ninachokisema hapa, fanyieni kazi haraka kesi za watuhumiwa hawa ili ziweze kumalizwa na wajue moja, kama wanafungwa au wanaachiwa huru, maana kwa kuendelea kuwa mahabusu hakuna tija kwa taifa.

“Hawa watu humu ndani wanatakiwa wafanye kazi za uzalishaji na hiyo inakuwa sehemu ya urekebishwaji na si kukaa bure na kujazana,” amesema.

Mahabusu hao walikabidhiwa kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mara ili kuhakikisha wanarudisha vitu walivyoiba, wanaomba msamaha na kuwa raia wema katika jamii.

Katika ziara hiyo, pamoja na Mpanju na DPP, walikuwapo pia wataalamu wa sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Dk. Edson Makallo; maofisa kutoka Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, waendesha mashtaka kutoka TANAPA na wadau wengine.

Aprili 26, mwaka huu Rais John Magufuli alitangaza msamaha kwa wafungwa 3,530. Waliofaidika na msamaha huo ni pamoja na wafungwa wagonjwa.

Msamaha huo wa Rais Magufuli umetolewa siku ya maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano wa Tanzania.

Katika idadi hiyo ya waliosamehewa, wafungwa 722 waliachiwa Aprili 26; na wengine 2,808 watabaki ili kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki kwa kuzingatia msamaha huo.

Pia Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa wote kwa kuwapunguzia robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza, Sura ya 58.

Takwimu za Magereza zinaonyesha kuwa hadi Aprili mosi, mwaka huu, idadi ya wafungwa katika magereza yote nchini ilikuwa ni 17,838; na mahabusu wa mahakama zote walikuwa 19,193. Jumla kuu kwa wafungwa na mahabusu wote nchini ni watu 38,668.

Uwezo wa magereza kuhimili wafungwa na mahabusu ni watu 29,902 pekee; hii ikiwa na maana kuwa magereza yamelemewa watu 8,766.

Hivi karibuni JAMHURI lilichapisha habari ya mahabusu wawili waliomwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, wakidai wanashtakiwa kwa kosa la kuua ilhali aliyefanya mauaji hayo na kukiri yuko huru uraiani.

Michael Laizer na Lucas Mmasi, wanashikiliwa katika Gereza Kuu Mkoa wa Arusha, Kisongo tangu mwaka 2015 wakikabiliwa na shtaka hilo, wanaodai kuwa ni la kubambikiwa.

Laizer na Mmasi wanadai kuwa wamebambikiwa kesi ya mauaji P.I Na. 17/2015 lakini kesi hiyo hiyo inamkabili mtuhumiwa mwingine ikiwa imepewa P.I Na. 14/2015.

Wanasema kinachothibitisha malalamiko yao ni kitendo cha kesi zote hizo mbili zinazohusu tukio moja kutajwa kwa hakimu mmoja katika mahakama iliyopo Arumeru mkoani Arusha. Jina la hakimu huyo tunalihifadhi.

Wanasema mtu wanayetuhumiwa kumuua, Julius Tarangei, aliuawa na mtu mwenye kifupisho cha jina F.M.

“Mtu huyo (F.M) aliripoti mwenyewe Kituo cha Polisi na baadaye alifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kuua bila kukusudia likiwa ni P.I Na. 14/2015 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arumeru. Katika kesi hiyo sisi tulikuwa mashahidi. Baadaye mtuhumiwa huyo alidhaminiwa na mpaka sasa [wakati wa kuandikwa barua] yuko nje kwa dhamana,” wanasema.

Laizer na Mmasi wanadai kuwa siku sita baada ya mtuhumiwa kuachiwa, waliitwa polisi na kuwekwa rumande; na siku iliyofuata wakapelekwa mahakamani na kusomewa shtaka la mauaji ya kukusudia. Kesi hiyo ni P.I Na. 17/2015.

“Ni jambo la kushangaza kwa polisi wakishirikiana na mawakili wa Serikali kufungua mashtaka mawili tofauti kwa mauaji ya mtu mmoja.

“Ni wazi kuwa baada ya kumfungulia [F.M] shtaka la kuua bila kukusudia sisi tungekuwa mashahidi katika kesi hiyo ila baada ya F.M kupewa dhamana na kutoroka, polisi wakaamua kutukamata sisi na kutufungulia mashtaka ya kuua kwa kukusudia…Hivyo, sasa kuna kesi mbili tofauti mahakamani zote zikiwa za kosa la kumuua mtu mmoja,” wanadai.

Mahabusu hao wanadai kuwa majalada yote mawili bado yanatajwa mahakamani yakimhusu marehemu mmoja, na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Wanadai kuwa wamelalamika kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini wamepewa majibu ya mdomo kuwa hawawezi kuachiwa hadi F.M akamatwe kwa kuwa hahudhurii mahakamani.

Machi 14, mwaka huu, DPP Mganga, akiwa mjini Dodoma, alizungumza na waandishi wa habari na kutangaza kumwachia huru mwananchi aliyebambikiwa kesi ya mauaji mkoani Tabora.

Alisema hatua hiyo ilitokana na uchunguzi uliofanywa kwa maagizo ya Rais John Magufuli, aliyesoma barua ya msomaji iliyochapishwa kwenye Gazeti la Majira la Machi 6, mwaka huu.

Baada ya kuisoma barua hiyo, rais aliiagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ifuatilie malalamiko ya mwananchi huyo kwa haraka ili kujua ukweli.

Kwenye barua hiyo, mlalamikaji, Musa Sadiki, alieleza jinsi askari wa Kituo cha Polisi Tabora Mjini walivyomkamata na kumnyang’anya Sh 788,000, simu ya mkononi na mali nyingine alizokuwa nazo kabla ya kumfungulia mashtaka ya mauaji katika Mahakama ya Tabora.

Please follow and like us:
Pin Share