Ng’ombe 1,000 wanaliwa kila siku jiji Dar es Salaam. Takwimu hizo zimepatikana katika machinjio yote yaliyoko jijini. 

Hali hiyo imesababisha ongezeko la mapato kutoka Sh milioni 4 hadi Sh milioni 8 kwa siku katika Mnada wa Mifugo Pugu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

JAMHURI limefuatilia kwa ukaribu na kubaini kuwa usimamizi makini wa uongozi wa mnada na utaratibu mpya wa ukusanyaji malipo ya ushuru wa soko na yale ya kibali cha kusafirishia mifugo; ulioanzishwa mapema mwaka jana umesababisha kuongezeka kwa mapato ya takribani milioni 70 kwa mwezi mwaka 2016 ikilinganishwa na mapato ya mwaka 2015.

Nyaraka ambazo JAMHURI limeziona zinaonesha kuwa mapato yamepanda kutoka kati ya Sh milioni 100 na Sh milioni 130 (2015) hadi kati ya Sh milioni 200 hadi Sh milioni 230 (2016). Nyaraka hizo zinaonesha kuwa Januari 2015 zilikusanywa Sh milioni 115.7 wakati Januari 2016 zilikusanywa Sh milioni 203.5.

Julai  hadi Desemba 2015, makusanyo yalikuwa kama ifuatavyo: Julai 118,632,000/-, 116,986,000/-(Agosti), 123,289,000/- (Septemba), 112,720,000/-(Oktoba), 119,860,000/- (Novemba) na Desemba zilikusanywa 155,143,000/.

Julai hadi Desemba 2016 mapato yalikuwa kama  ifuatavyo: 250,185,500/- (Julai), 228,705,000/- (Agosti), 235,355,000/-(Septemba), 233,042,500/- (Oktoba), 221,534,500/- (Novemba) na Desemba  zilikusanywa 242,740,000/-.

Mbali na mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji mapato, uchunguzi umebaini pia uwepo wa sheria ndogo za soko zinazosimamiwa kwa uaminifu na uongozi mpya wa mnada, umechangia pakubwa ongezeko la mapato yanayokusanywa na mnada.

Mkuu wa Mnada, Kerambo Samweli, amesema kuwa yeye aliteuliwa kushika wadhifa huo Januari mwaka jana, ambapo alielezwa na mamlaka iliyomteua kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa wa kuiibia mapato Serikali yanayokusanywa mnadani hapo. Amesema usimamiaji na ushirikiano wa wafanyakazi wenzake ni sababu mojawapo iliyofanya mafanikio hayo.

Alipoulizwa ni mbinu gani uongozi huu mpya wa mnada unaoutumia kukusanya mapato mara mbili kwa yale ya awali, Samweli alisema kuwa ni usimamizi makini.

“Kuna watu wanasema kuwa mfumo wa kutumia benki ndiyo uliosababisha kuwapo kwa mabadiliko haya, si kweli ni usimamizi mzuri wa timu niliyonayo inayojumuisha askari, daktari na watu wa uhasibu. Benki imeanza kufanya kazi mwezi April mwaka jana katika tawi la Pugu ambalo limo humu mnadani. Benki ilikuwapo tangu awali, pesa zilikuwa zikipelekwa tawi la NMB Mzambarauni-Gongo la Mboto,” amesema Samweli.

Amesema kuwa uzalendo na uaminifu wa timu anayofanya nayo kazi ndiyo mzizi wa mafanikio hayo.

“Kama na sisi tungeendelea na utaratibu uleule wa kupiga dili basi kusingekuwapo na mafanikio haya. Watu wanaweza kusema najisifia lakini ukweli ni kwamba kama watu wasipofanya kazi kwa ushirikiano madili yataendelea kupigwa tu kwenye ofisi husika. Na pamoja na kutokana na kuwa wakali kwa kusimamia sheria, bado maneno ya chini chini yanayoenezwa kuwa sisi tunachukua fedha za mnada,” amesema Samweli.

Amesema kuwa wapo wafanyabiashara mnadani hapo ambao maslahi yao yameingiliwa, hivyo wanasambaza fitina ili mamlaka zisambaratishe uongozi wa mnada uliopo. Amesema tawi la Benki ya NMB Pugu lilisogezwa mnadani hapo kwa madhumuni ya kurahisisha utendaji na usalama wa fedha.

“Kabla ya 2016, Mhasibu ndiye aliyekuwa mambo yote. Pesa ilikuwa inatua kwake kama ilivyo kutoka kwa mfanyabiashara. Ila sasa hivi pesa haipiti kwake moja kwa moja yeye sasa anapokea risiti tu ya malipo yaliyofanywa na mfanyabiashara katika benki. Zamani mtoza ushuru alikuwa na uwezo wa kufanya ujanja kwa sababu ndiye aliyekuwa mtoza ushuru na mtoa risiti,” amesema Samweli.

Amesema kwamba utaratibu wa sasa wa malipo unawahusisha daktari wa mifugo, mhasibu, benki na mkuu wa mnada.

JAMHURI lilimtafuta aliyekuwa Mkuu wa Mnada huo, Habib Malamla, kutaka kujua kama ni kweli ubadhirifu ndiyo uliochangia kutokukusanywa mapato mengi lakini alikanusha.

“Hapana siyo kweli kwamba kulikuwa na ubadhirifu wa mapato ya mnada. Kilichochangia kuongezeka mapato ya mnada ni utaratibu mzuri uliopo sasa. Tulipokuwapo sisi hakukuwa na ‘support’ ya kutosha kudhibiti wafanyabiashara wakwepa kodi. Kuna wafanyabiashara wengi walikuwa wakiipeleka mifugo yao moja kwa moja kwenye machinjio wakikwepa malipo yanayotakiwa kufanyika mnadani,” amesema Malamla.

“Mbuzi na ng’ombe wengi walikuwa wakiuzwa juu kwa juu na kupitiliziwa machinjioni. Mfano, machinjio ya Kimara na Vingunguti yametumika sana kwa ukwepeshaji mifugo. Tulikuwa tukijitahidi kudhibiti hali hiyo lakini hatukupata uungwaji mkono kama wanaoupata wenzetu kutoka kwa Serikali. Hakuna mtu aliyekuwa anapiga dili. Ni usimamizi mzuri tu wa Serikali ya sasa ndiyo uliosababisha wafanyabiashara wote kuanzia Pugu. Hiyo ndiyo sababu ya kuongezeka mapato,” amesema Malamla.

Malamla amesema jambo lolote likisimamiwa kwa ushirikiano mkubwa wa viongozi, ni lazima tu litazaa matunda tofauti na pale ngazi fulani ya uongozi inapohitaji msaada wa kuboresha utekelezaji wa majukumu yake na isiupate ipasavyo.

JAMHURI lilizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa ng’ombe na mbuzi mnadani hapo ili kupata kujua tofauti ya hali ya mwenendo wa biashara ya mifugo kwa sasa ikilinganishwa na kabla ya Serikali Awamu ya Tano haijaingia madarakani, mmoja wa wafanyabiashara hao amesema:

“Hapa mnadani palikuwa ni shamba la bibi, kuna mama mmoja hapa alikuwa mtoza ushuru kwa muda mrefu, wamepiga sana hela…si mkuu wa mnada wala askari, wote walikuwa ni wapiga dili tu. Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kuleta heshima hapa mnadani….yaani kipindi cha nyuma mtu alikuwa haoni shida kumpangishia mwanamke chumba…hizi laki moja moja walikuwa wanahongwa sana wanawake,” amesema Mwita Bwire.

Bwire amesema yeye amekuwa mfanyabiashara ya ng’ombe kwa miaka 17 sasa. Amesema kuwa kuna wafanyabiashara ambao walikuwa wakiingiza mifugo mingi mnadani, ila kwenye kibali inaandikwa namba ya mifugo michache.

“Mfugaji alikuwa anatoka kijijini na ng’ombe labda 80 huku kibali chake alichokuja nacho kikionesha ana ng’ombe 60, akifika hapa wakihesabu wanakuta wamezidi ng’ombe ishirini, badala ya kumpiga faini mtu wa ushuru na wenzake wanaelewana kugawana hela ya wale ng’ombe waliozidi nusu kwa nusu, halafu ng’ombe hao hao 60 wanaandikwa kwenye kitabu kuwa ni 30, hela zote zinapigwa,” amesema Bwire.

Hata hivyo, mbali na kusifu hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Bwire amemshauri Rais Magufuli kupitia Wizara ya Mifugo kuendelea kuutizama kwa makini mwenendo wa mnada wa Pugu.

“Namshauri Rais Magufuli asiache kuuangalia huu mnada bado wapo watu wa kutumbuliwa. Hapa bado kuna majipu hususani  askari. Kuna askari hapa mimi nimeanza kuwaona tangu nimeanza kazi hii, hawahamishwi wakihamishwa wanakaa miezi mitatu tu kisha unawaona tena wamerudi,” amesema Bwire.

Alipoulizwa mkuu wa mnada kuhusu kuendelea kuwapo kwa rushwa miongoni mwa askari, daktari wa mifugo alikanusha na kusema hizo ni shutuma za wale ambao walizoea kuiibia Serikali kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu.

“Sasa hivi tumedhibiti suala la askari kuhongwa wala daktari. Hakuna tena kitu hicho, tunafanya kazi kama timu sasa baada ya kuona tumewabana wameanza kuzusha uongo ili tuonekane hatufanyi kazi,” amesema Samweli.

Uchunguzi wa JAMHURI  umebaini kuwapo ukata wa fedha miongoni mwa madalali wa mifugo inayoingizwa mnadani hapo kutoka mikoani. Sheria zilizopo ni pamoja na faini ya laki tatu ambayo atatozwa mfugaji atakayebainika kudanganya idadi ya mifugo. Ikibainika mfugaji amedanganya zaidi ya mifugo 20 anatozwa faini ya laki tatu na ikiwa chini yake faini inakadiriwa.

 

Changamoto

Mkuu wa Mnada Pugu, Samweli, amesema kuwa bado zipo changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi. Amesema kuna changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo. Amesema eneo kubwa la mnada limevamiwa hivyo kusababisha udogo wa eneo la malisho.

“Eneo lililovamiwa ni kubwa kuliko eneo lililopo kwa matumizi ya mnada na malisho. Tuna eneo la ukubwa wa jumla ya hekari 1900. Eneo lililovamiwa na watu waliofanya makazi ni nusu yake. Tatizo hili tumeshalifikisha Wizara ya Ardhi na Wizara ya Kilimo na Mifugo na hivyo tunasubiri mwafaka,” amesema Samweli.

Samweli amesema kuwa watumishi wa mnada wamekuwa wakiishi mbali na eneo la kazi, hivyo anaomba Serikali itenge bajeti ambayo itawezeshwa kujengwa kwa nyumba kwa ajili ya wafanyakazi wa mnada wa Pugu.

“Wafanyakazi wanaishi mbali, ingekuwa vyema zaidi kama tungepata makazi hapa jirani ili kuwa na ufanisi zaidi kwa sababu mifugo inaingia mnadani hata usiku wa manane kutoka mikoani. Vilevile suala la motisha litazamwe kwani sisi hatuna ‘weekend’ tunafanya kazi siku zote bila kujali kama ni sikukuu,” amesema Samweli.

2951 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!