Madhumuni ya Mamlaka:

 Dhana ya Mamlaka za Kimataifa (International Mandates) zilichagizwa na Rais Wilson na viongozi wengine wa mapinduzi ya Russia na ukomo wa vita katika Vita ya Kwanza ya Dunia isingehusisha mmego wowote (annexation), lakini ingekatika katika Kanuni Kuu ya Uhuru wa kujiamulia mambo ya watu.

Pendekezo mahususi la dhana ile lilitolewa na General Smuts kama sehemu ya mradi wa Muungano wa Mataifa (League of Nations) ambao uliochapishwa Desemba, 1918 katika kilele cha mkutano wa amani. Dhana ya malengo yake mahsusi kuainishwa katika kifungu cha 22 cha makubaliano (covenants) ya Muungano wa Mataifa na kuridhiwa 25 Aprili, 1919 kiliainisha mipaka ya kijiografia ambayo ilipaswa kuwa chini ya Mamlaka. 

 Mamlaka hizi zilikuwa kama ifuatavyo:- (i) maeneo yaliyokuwa yametengwa kutoka himaya ya Uturuki (ii) baadhi ya maeneo ya kijiografia katika Afrika ya Kati; na (iii) maeneo ya Kusini Magharibi mwa Afrika na baadhi ya maeneo ya visiwa vya kusini vya Pacific.

Mwenendo wa Mamlaka na nguvu za kimamlaka zingetofautiana kwa kila moja katika makundi haya matatu ya maeneo ya mipaka ya kijiografia. Palestina, ikiwa ni moja ya eneo la mpaka wa kijiografia lilitokana na himaya ya Uturuki, ilikuwa ni moja ya nchi ambayo uhuru wake ulikuwa ukitambuliwa kisheria. Aprili 25, 1920 pale San Remo, Baraza la Juu la Muungano wa Mataifa lilipoamua kugatua mamlaka kwa Palestina chini ya Uingereza, lakini masharti ya mamlaka ile hayakuwa yamewekwa bayana.

 Moja ya maudhui ya ziada ya Mamlaka ya Palestina ni kwamba masharti yake yaliundwa na chombo cha nje ambacho kilikuwa na maslahi ya kisiasa katika nchi husika kwenye makubaliano ya Februari 3, 1919 yaliyowasilishwa na Chama cha Kimataifa cha Wazayuni (The World Zionist Organization).

 Katika mkutano wa amani Paris, Ufaransa, chombo hiki kiliainisha matakwa na matamanio ya kimaslahi (desiderata) katika minajili ya hali ya baadaye ya Palestina. Ni muhimu kutanabahisha kwamba maoni mengi ya yale makubaliano, yalijikita katika rasimu ya Mamlaka kwa ajili ya Palestina ilisukwa na chama cha Wazayuni na kusambazwa mwishoni mwa mwezi Machi, 1919 na baada ya mapitio ya ziada ya chombo cha Mamlaka kwa Baraza la Muungano wa Mataifa inadaiwa kuwa mambo mengi katika ‘memorandum’ ile juu ya Palestina yalijadiliwa na Uingereza kwa mashauriano na uwakilishi wa Wazayuni.

Tofauti na ilivyotegemewa pande zilizokuwa muhimu kabisa – yaani Waarabu wa Palestina hawakushirikishwa. Julai 24, 1922, Mamlaka ya Palestina ilithibitishwa na Baraza la Muungano wa Mataifa, kwa kiwango kikubwa yakiwa ni mapendekezo ya organaizesheni (organization) za Wazayuni.

 Katika makubaliano haya, kutekelezwa kwa kifungu cha 22 cha makubaliano: Dokezo lake la mwanzo likiwa.

 “Kwamba Muungano wa Mataifa makubwa umekubaliana na utekelezaji wa kifungu cha 22 cha makubaliano ya Muungano wa Mataifa, kugatua mamlaka, yaliyotajwa kwa madhumuni ya kifungu hiki kwa Palestina kwa malengo ya utekelezaji wa kifungu cha 2 cha Mamlaka. Mamlaka itakuwa na wajibu wa kuendeleza taasisi zinazojitegemea.”

Lengo la pili lilikuwa ni utekelezaji wa Azimio la Balfour na kusimamia suala zima la uhamiaji wa Wayahudi.

 Wapalestina Waarabu waliikataa Mamlaka na wakaweka msimamo kwamba Mamlaka hiyo isingelinda haki zao kama wakazi wa asili wa Palestina. Kutokana na hali hii hawakuwahi kuondoka katika eneo lao la asili kwa kipindi chote cha ‘mandate’ ile. Hawakukubaliana na uhalali wake na wakaridhia sera za kutoshirikiana na mamlaka (non-cooperation with the mandatory).

 Kusema ukweli, historia ya Mamlaka ile ilikuwa ni harakati za Wapalestina dhidi ya Azimio la Balfour, uhamiaji wa Wayahudi na uanzishwaji wa makazi ya Wayahudi ndani ya Palestina, lakini mapambano yale yalikuwa ni sawa na vita kati ya sisimizi dhidi ya tembo!

 Ikitumia Mamlaka ile kama silaha, nguvu za himaya ya Uingereza na msaada wa majeshi ya Uzayuni, Serikali ya Uingereza ilitekeleza Azimio la Balfour ndani ya Palestina dhidi ya matakwa ya Wapalestina. Upinzani wao ulichukua taswira ya maandamano, vurugu na uasi wa mapambano.

Lakini maandamano ya Wapelestina  yalizimwa kwa nguvu za kijeshi na kutulizwa  kwa ahadi lukuki zilizokonga nyoyo zao.

Je, unajua nini kiliendelea? Usikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo.

 

>>ITAENDELEA.

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Anapatikana kwa:-

 (+255)784  142  137

(+255) 713 333141

Au  barua  pepe

[email protected]

[email protected]

By Jamhuri