Diwani wa Kata ya Nyugwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Donald Kabosolo, anafanya kazi ya ziada kuzima tuhuma dhidi yake juu ya uhusiano wa kingono na mwanafunzi wa sekondari ya kata hiyo iliyopo katika  Wilaya ya Nyang’hwale, mkoani Geita.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Diwani Kabosolo alifumaniwa na kukamatwa Januari 22, mwaka huu, saa 7 usiku kwenye nyumba ya kulala wageni inayojulikana kwa jina la Amani, iliyopo katika Kijiji cha Kharumwa. Nyumba hiyo ya kulala wageni ni kitegauchumi cha diwani huyo.

Inaelezwa kuwa Kabosolo ana uhusinao wa kimapenzi na mwanafunzi huyo (jina tunahifadhi), tangu akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kakora, kabla ya kuhamia Sekondari ya Nyugwa. Vyanzo vya habari kutoka Kijiji cha Kakora vimeiambia JAMHURI kuwa Kabosolo alikuwa akionekana mara kwa mara maeneo hayo akiwa na mwanafunzi huyo.

Kutoka na uhusiano huo kukolea, diwani huyo anadaiwa kumshawishi binti huyo kuwaomba wazazi wake wamchukulie uhamisho kwenda kusoma Shule ya Sekondari Nyugwa ambako yeye ndiye mheshimiwa wa kata hiyo kupitia CCM.

Taarifa zinasema kwamba binti huyo alifanikiwa kupata uhamisho mapema mwezi uliopita baada ya baba wa binti huyo, Joseph Balele, kufanikisha uhamisho huo kwa kushirikiana na Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Geita na wakuu wa shule za sekondari za Nyugwa na Kakora.

Barua hiyo ambayo JAMHURI imebahatika kupata nakala yake, inasema: “Tafadhari husika na kichwa cha habari hapo juu, mwanafunzi (jina tunalihifadhi) wa kidato cha pili naomba nimuhamishie hosteli ya Nyugwa kutoka Shule ya Sekondari Kakora. Natanguliza shukrani zangu za dhati kwako, kama ombi langu litakubalika.”

Baada ya ombi hilo kukubaliwa na mamlaka husika ngazi ya wilaya, mwanafunzi huyo alihamia Shule ya Sekondari Nyugwa kwa lengo la kwenda kuishi hosteli, lakini badala yake alikwenda kuishi kwenye nyumba ya kupanga katika Kijiji cha Mumbili, jirani na shule hiyo.

Taarifa zinasema kwamba alipohamia kijijini hapo Kabosolo alianza kumhudumia kila kitu alichokuwa anakitaka kama mke, kwa kumnunulia kitanda, viti, meza na alikuwa akipatiwa matunzo kama yuko kwenye ndoa japo ni mwanafunzi.

Baadhi ya watu wa karibu na diwani huyo  wanadai alikuwa akimchukua na kwenda naye kutanua sehemu mbalimbali za starehe kama Kharumwa, Kakora, Kahama, Geita, Sengerema pamoja na mji mdogo wa Katoro.

Kutokana na wananchi kuchoshwa na tabia ya diwani  huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Wilaya hiyo, waliweka mtego wa kumvizia akiingia kwenye gesti yake kana kwamba imehalalishwa watu kufanya mapenzi na wanafunzi.

 

Mtego

 

Shuhuda wa tukio hilo, Juliana Masolwa, aliieleza JAMHURI, “Sisi tulihisi tu ana uhusiano na huyu mwanafunzi, maana tumekuwa tukimuona naye mara kwa mara ila hatukuwa na uhakika kama huyo binti ni mwanafunzi, japo umri wake ulitutia shaka kutokana na mwanaume aliye naye kuwa mtu mzima mithili ya babu yake, tulipofuatilia tulibaini ukweli baada ya polisi kumkamata.”

Anasema siku ya tukio, mara baada ya diwani na mwanafunzi huyo kuingia katika nyumba hiyo ya kulala wageni, walitoa taarifa polisi waliokuwa doria usiku, walipofika eneo la tukio waligonga mlango kwenye chumba namba 10 walimokuwa.

Mlango ulipofunguliwa walimkuta diwani huyo akiwa kwenye taulo huku mwanafunzi huyo akiwa amelala kitandani.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa diwani huyo aliwahi kuwa Mkatekista wa Kanisa Katoliki, Kigango cha Mumbili, baada ya kufikishwa kituoni hapo, Januari 23, mwaka huu, alichukuliwa maelezo kisha lilifunguliwa Jalada Na. KH/IR/44/2015 kosa la kubaka kabla ya kuachiwa na mpaka gazeti hili linaibua taarifa hizi yuko uraiani akitanua kana kwamba hana kesi ya kujibu.

 

Kauli yake

JAMHURI ilipofunga safari hadi eneo la tukio kufuatilia sakata hilo, ilibahatika kumuibua mafichoni Kabosolo ambaye, hata hivyo, aligoma kuzungumzia kwa undani sakata hilo kwa madai kuwa akili yake imekwishavurugika na kumuomba mwandishi amwache ili atulize akili yake.

“Victor, naomba uniache kuhusu hili, akili yangu imevurugika sana maana kutwa nzima napokea simu kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu na kila mtu anataka nimwambie ilivyokuwa, sasa mimi nitakwambia nini! Niache tu akili yangu imevurugika sana na ninashindwa kuzima simu maana naweza kupigiwa na watu mhimu wakanikosa hewani,” anasema Kabosolo.

 

Maelezo ya daktari

 

Tabibu, Dk. Isaya Walwa, aliyemfanyia uchunguzi wa afya mwanafunzi huyo, anasema baada ya kufikishwa katika Kituo cha Afya Kharumwa, alipimwa mimba, magonjwa ya zinaa na vipimo vingine.

Majibu ya vipimo hivyo yalionesha hana ujauzito, hana mambukizi ya virusi vya Ukimwi wala magonjwa ya zinaa, isipokuwa manii na vivimbe sehemu za siri, na hivyo kuthibitika kwamba alikuwa amefanya mapenzi.

“Alifikishwa kituoni hapa saa 1:30 asubuhi akiwa na askari wa kike wawili, wakitokea Kituo cha Polisi Kharumwa baada ya kuwa wameeleza kwamba alikuwa gesti na mwanaume,” anasema Dk. Walwa.

Anasema baada ya kufanyika uchunguzi huo, aliijaza fomu Na. 3 (PF 3) na kuikabidhi kwa askari polisi ambao waliondoka na binti huyo kuelekea kituoni.

 

Ofisa Elimu Wilaya

 

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Dayness Samwel Mosha, anakiri mwanafunzi huyo kufumaniwa akiwa na diwani huyo, aliyemshangaa kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi mwenye umri mdogo, hasa ikizingatiwa kuwa diwani huyo ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kwenye halmashauri hiyo.

“Huyu diwani ni mzazi anayejua uchungu wa kusomesha na faida zake hapo baadaye na pia alipaswa awe kioo cha jamii lakini nashangaa kuamua kutaka kumharibia maisha mwanafunzi huyo, ambaye wazazi wake wanamsomesha ili awakomboe baadaye. Ningeomba sheria ichukue mkondo wake ili awe mfano kwa watu wengine wenye tabia kama yake,” anasema.

 

Ofisa Elimu Taaluma Wilaya

 

Mwalimu Christopher Makoye ambaye ni Ofisa Elimu Taaluma Wilaya ya Nyang’hwale, naye anakiri uwepo la tukio la diwani kufanya mapenzi na mwanafunzi wake.

”Hata sisi tulisikia kwamba mheshimiwa diwani Kata ya Nyugwa kakamatwa akiwa na mwanafunzi wa Sekondari ya Nyugwa, nikafuatilia ili kujua iwapo ni mwanafunzi na kumuomba mwalimu wake alete taarifa na kweli alikuwa mwanafunzi wa sekondari hiyo,” anasema.

Akizungumzia madhara anayoweza kuyapata mwanafunzi anayechanganya masomo na mapenzi, Makoye alidai ni pamoja na afya kudhoofu na kuwa hatarini kupata magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na kuambukizwa Ukimwi, kutokuwa na uwezo mzuri darasani na nidhamu mbovu.

 

Mkuu wa Shule

 

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyugwa, Henrick Jembe, anakiri mwanafunzi wake kukutwa akifanya mapenzi na mheshimiwa diwani wa kata yake.

Anasema Alhamisi asubuhi alipigiwa simu na Ofisa Tarafa ya Msalala akimtaarifu kwenda Kituo cha Polisi Kharumwa kuthibitisha kama kweli mwanafunzi huyo ni wake.

“Ni kweli nilimkuta mwanafunzi wangu. Nikamuuliza kulikoni yupo kituoni, akaniambia kwamba amekamatwa akiwa pamoja na diwani kwenye nyumba ya kulala wageni,” anasema mwalimu huyo.

Anasema mwanafunzi huyo ni miongoni mwa wanafunzi 66 wa kidato cha nne na miongoni mwa wasichana 21 ambao hawajaonekana shuleni hapo tangu Januari 19, mwaka huu.

Hata hivyo, anasema mwanafunzi huyo amekuwa akifanya vizuri darasani, tofauti na wanafunzi wengine wa kike baada ya kupata wastani wa 42 kwenye Mtihani wa Taifa wa kidato cha pili.

Kuhusu utoro shuleni hapo, Mwalimu Jembe anasema kwa wastani utoro ni asilimia 20, baada ya wanafunzi kuacha shule kwa kuozeshwa na kuchunga mifugo kwa wavulana.

“Hizi taarifa ni kweli, diwani wetu alikamatwa akiwa na mwanafunzi wangu saa 7 usiku wa kuamkia Alhamisi. Na asubuhi Ofisa Tarafa ya Msalala alinipigia simu akinitaka nifike kituo cha polisi kumthibitisha mwanafunzi huyo kama kweli anasoma kwenye shule yangu, ambayo inazo hosteli za wasichana na wavulana na nilipofika nikakuta ni mwanafunzi wangu,” anasema.

 

Baba mzazi

 

“Huyu mwanafunzi yeye haishi hosteli, amepanga nyumba ya kuishi katika Kijiji cha Mimbili Centre, umbali wa kama kilometa moja kutoka shuleni hadi kijijini hapo,” anasema Joseph Balele, baba mzazi wa binti.

Baba mzazi wa binti huyo anadai baada ya kupata taarifa za binti yake kukutwa akifanya mapenzi na diwani huyo, alifuatilia Kituo cha Polisi Kharumwa lakini hakupewa ushirikiano wowote na kuamua kurudi nyumbani.

Alipohojiwa sababu za kumpangishia mwanaye huyo uraiani ilhali sekondari hiyo ina hosteli, alikosa majibu ya kuridhisha kwa kudai kuwa mwanafunzi ndiye aliyelazimisha hivyo.

 

Mwenyekiti wa Halmashauri

 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Yavin Petro, anakiri diwani wake kukutwa na mwanafunzi huyo lakini hawezi kulizungumzia kwa undani suala hilo kwa vile lipo kwenye mikono ya sheria.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mbali na kulaani kitendo hicho, alidai pia kata hiyo haina maabara hata moja na kwamba zipo kwenye hatua isiyoridhisha (hatua ya msingi).

 

Polisi wathibitisha

 

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Peter Kakamba, anasema jalada la kesi hiyo lipo kwa Mwanasheria wa Serikali likisubiri hatua nyingine ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

“Ni kweli tukio hilo lipo na jalada la kesi hiyo ya kufanya mapenzi na mwanafunzi kinyume cha Sheria ya Elimu ya mwaka 2002 lipo kwa DPP kwa hatua zaidi,” anasema Kamanda Kakamba

 

Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita likidai kuwa jalada la kesi hilo lipo ofisi ya DPP, Februari 25, mwaka huu, saa 2:13 asubuhi gazeti hili lilipowasiliana na mwanasheria huyo mkoani hapa, Kiliani Kiliani, alikana kufikishiwa maelezo ya kesi hiyo.

”Sina brother (kaka),” anajibu mwanasheria huyo na alipofafanuliwa majibu ya polisi akasisitiza: “Nimekwambia sina.”

 

DC alaani

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Ibrahim Marwa, mbali ya kuthibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kudai tayari ameagiza Idara ya Elimu Sekondari kumhamishia hosteli mwanafunzi huyo, ameagiza pia vyombo vya dola kumfikisha mahakamani diwani huyo.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa wakati mwanafunzi huyo akisoma Shule ya Msingi Kakora, alikuwa na wastani wa 89 darasani ambapo darasa la tano wastani 117, sita wastani 89 na saba wastani 89 na alikuwa miongoini mwa wanafunzi 10 bora.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba hili ni tukio la pili linalofanana kutokea, kwani Novemba 8, 2014 saa 1:30 asubuhi, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Msalala, Garald Mshana, alikamatwa nyumbani kwake akifanya mapenzi na mwanafunzi wa kidato cha nne.

Hata hivyo, pamoja na watuhumiwa kukamatwa na polisi, hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya kufikishwa Kituo cha Polisi Kharumwa na kufunguliwa jalada Na. KH/IR/577/2014 kosa likiwa kufanya mapenzi na mwanafunzi.

By Jamhuri