MtotoNA VICTOR BARIETY, GEITA
Mtoto mwenye umri wa miaka 13 amelazimika kutoroka nyumbani na kwenda kuishi kwa wasamaria wema, baada ya kulemewa na kichapo kutoka kwa mwanaume mwenye kifua na misuli mipana (baunsa).
 Mtoto huyo, mwanafunzi wa Darasa la Saba B, katika Shule ya Msingi Kalangalala, iliyoko wilayani hapa alikula kichapo na baunsa huyo aliyelipwa ujira Sh. 5,000 na mama mzazi wa mtoto huyo.
  Siri hiyo imetolewa na mtoto huyo wa kike, Grace Samwel, akiwa mafichoni baada ya kukataa kurejea nyumbani kwa Mama yake, Hellen Edwin Katambi (32).
 Taarifa ambazo zimethibitishwa na binti huyo zinasema kwamba Hellen alikodi baunsa wa kumpa mkong'oto wa nguvu kila atokapo shule kila binti huyo anaposhindwa kufanya kazi nyingi zinazozidi uwezo wake.
  Anasema wakati baunsa huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja anapotekeleza unyama huo, humfunga kamba mikononi na miguuni ili asifurukute kisha kuanza kumpa kichapo sehemu mbalimbali za mwili wake.
  Mateso hayo yamemfanya binti huyo kuanza kujitegemea baada ya mama yake kumpatia jiko lake kwa ajili ya kujipikia huku mahitaji mengine kwa ajili ya chakula akitakiwa kutafuta kwa njia anazojua yeye.
  Mbali ya jiko, mama yake humhudumia unga pekee ilhali mboga anajitegemea sambamba na kuchanja kuni tangu Desemba 5, mwaka jana baada ya mama yake kumwambia kwamba wakifunga shule asirudi nyumbani na atafute pa kuishi.
 
Maelezo ya mtoto

“Nimeamua kutoka nyumbani kwa maana mama yangu ananitesa sana, ninapigwa pasipo sababu na mama amenitafutia mwanaume (baunsa) kwa ajili ya kunichapa na anamlipa Sh. 5,000 kila anapomaliza kunichapa sehemu mbalimbali za mwili kasoro kichwani na tumboni,” anasema.
  Anasema, “Wakati ninaishi nyumbani nilikuwa najitegemea, maana nilipewa mahindi ili nisage, masufuria mawili yaliyotoboka ndiyo niwe napikia chakula changu, mwiko mmoja na beseni, moto naazima kwa jirani maana nyumbani mama alinizuia kuchukua.”
  Huku akionesha majeraha mwilini, binti huyo anasema, “Sipati huduma, mafuta ya kupaka natumia ya kula (kupikia) na si yale ya kupaka mwilini, nguo hanunui na kama unavyoniona sikio limeathirika, limejaa vidonda kwa ndani, kiuno kinauma, miguu imejaa majeraha pamoja na mikono.”
  Binti huyo ambaye alikuwa akijitahidi kuzungumza huku machozi yakimwagika, anasema awali kabla ya kuchukuliwa na wasamaria wema, mama yake alikuwa amemwambia wakifunga shule Desemba 5, 2014, “Tafuta pa kuishi.”
 
Baba anajua hili?
Samwel Peter (36), baba wa kambo wa binti huyo, anasema; “Nimeona mwanangu ana majeraha kama wiki mbili zilizopita.”
 Anasema kwamba alipohoji, binti huyo akajibu haraka, “Nimepigwa na mama na mwanaume aliyemkodi ili awe ananichapa.”
  Anasema alipotaka kujua sababu za kupigwa, mwanaye huyo hakuweza kuitaja kwa kuwa mama yake alikuwa eneo hilo na anadhani alihofia kupigwa tena iwapo angeeleza zaidi. Alipomhoji mkewe sababu za kumpiga alidai ni kugoma kuosha vyombo.
  Hata hivyo, hakuchoka kwani baada ya mkewe kutoka eneo hilo alimhoji tena binti yake ambaye alikiri kugoma kuosha vyombo na hata alipomuomba msamaha mama yake hakuweza kumsamehe.
  “Baadaye nilimwambia mke wangu asirudie kumpiga mtoto huyo lakini jibu alilonipa ni kasheshe.”
  Kwa mujibu wa mama huyo aliyekuwa akimjibu mume wake Samwel, ni kwamba binti ana kiburi licha ya kwamba ni wa kuzaliwa kwa mama huyo. Anaishi na Samwel kama baba wake wa kambo.
  “Mimi nakaa hapa na mtoto wako ambaye si wa kumzaa mimi, nimemfundisha kuoga na kuosha vyombo hadi ameelewa. Kwanini wewe hutaki wangu nimfundishe, je, mna ajenda gani ya siri?”
  “Akaniambia niache amfundishe mwenyewe na yanayohusu mwanangu niachie nimfundishe mimi mwenyewe,” amenukuliwa mama huyo na Samwel.
  Anasema pamoja na majibu ya hovyo ya mkewe, hakunyamaza na alikwenda kumweleza shemeji yake, kaka wa mkewe aitwaye Dotto Katambi.
  “Kaka yake mke wangu alishauri mtoto akifunga shule nimpeleke kwake jijini Mwanza akaishi huko kwani mateso aliyokuwa akiyapata ni makubwa,” anasema.
 “Huyu mwanamke nimezaa naye mtoto mmoja Janeth Samwel ambaye ana umri wa miaka tisa sasa na huyu anayenyanyasika nilimuoa akiwa naye, hivyo nilimkuta naye,” anasema.
  “Nilikuwa kwenye shughuli zangu nikapata taarifa kwamba familia yako haipo na mke wangu anatafutwa na polisi. Nikaenda kwa balozi kutoa taarifa na baadaye nikafika shuleni kujua kulikoni,” anasimulia Samwel.
  “Alipokulia mtoto huyu, kakulia kwa bibi yake mzaa baba na  alikuwa akiishi wilayani Misungwi, na baada ya kufariki bibi yake akahamishiwa kwa shangazi yake Mwanza. Nami nimeanza kuishi naye mwaka 2013 mpaka sasa,” anasema.
 
Mwalimu anasemaje?
“Nilipigiwa simu Alhamisi Desemba  4, 2014 saa 4 asubuhi na jirani wa mtoto ambaye hakutaka kutaja jina lake, akasema kwamba samahani kuna binti (akamtaja jina) wa Darasa la Sita B Kalangalala anaishi na mama yake mzazi, lakini anamfanyia sana ukatili,” anaanza kusimulia Mwalimu Veronica Samo.
  “Akaomba nimtafute mtoto anipe maelezo baadaye nikamfuatilia mtoto na kumchukua maelezo na ile naanza kumchukua maelezo tu akaanza kulia akidai anaogopa kuuawa na mama yake iwapo atagundua amenieleza, nikamsihi sana ndipo akaanza kunisimulia.
  “Kwanza anasema anapewa kazi nyingi pale nyumbani na anaposhindwa kuzimaliza anapigwa sana na mpaka anakodiwa mtu (baunsa) wa kumpiga, anamfunga kamba mikono na miguu na kuanza kumpiga.
 “Kwa vile ni mtoto wa kike, alinionesha maeneo yote aliyopigwa na kujeruhiwa, niliwashirikisha walimu wenzangu na kila mmoja akatoa maoni yake.
 “Tulimwandikia mama wa mtoto barua aje shule siku ya kufunga shule, ile Desemba 5, 2014 asubuhi ili kuzungumza naye. Hii ni kwa sababu mtoto alithibitisha kwamba alipewa jiko lake kujipikia na unga, lakini mboga anajitegemea.
  “Baada ya hapo Mwalimu Regina, Mkuu wa Shule ya Kalangalala akamwandikia barua mama mzazi afike shuleni kwa ajili ya kutafuta suluhu ya tatizo hilo, yule mama hakufika na wala hakudiriki kusoma barua ya wito aliopelekewa na binti yake huyo,” anasema.
  Anasema baada ya kuona mama huyo kasusa, wakampeleka Ofisi ya Ustawi wa Jamii, Halmashauri ya Mji wa Geita, na kusikilizwa na Valeria Makonda ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii.
 Anasema maelezo hayo tu yaliwafanya wagundue kuwa kuna kosa la jinai, hivyo wakapewa msaada hadi Kituo cha Polisi Wilaya ya Geita na kutoa maelezo kwa PC Rebecca wa Dawati la Jinsia aliyefungua jalada na kupewa hati ya matibabu PF3.
 
Idara ya Maendeleo ya Jamii Geita
Nsia Mananda, Ofisa Maendeleo ya Jamii Kitengo cha Wanawake na Watoto, ndani ya Idara ya Maendeleo, Ustawi wa Jamii Geita, Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii imekwishaanza mkakati wa kukomesha matukio ya ukatili wanayofanyiwa watoto.
  Anasema hali hiyo inachangiwa na upungufu wa wataalamu katika maeneo ya mtaa na kata, kwani wananchi wanashindwa kujua athari za ukatili kwa watoto.
  Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Margareth Nakainga, tayari wamekwishaomba watumishi wa kada hiyo ili kupunguza tatizo hilo.
  Kadhalika, Valeria Makonda anakiri kuwapo kwa matukio ya ukatili kwa watoto na kueleza kuwa sababu hasa ni pamoja na  migogoro ya kifamilia, malezi duni kwenye familia wanazotoka, muingiliano wa watu, mimba za utotoni, mmomonyoko wa maadili na utandawazi.
 
Nini kifanyike?
Anasema mkakati uliopo ni kutoa elimu kwa njia ya semina kwa wazazi ili kuachana na ukatili, akidai kwamba wameanzisha mkakati wa kuwakumbusha wazazi majukumu yao ya malezi na tayari halmashauri kwa mwaka ujao wa fedha, wametenga fungu kwa ajili ya kutoa elimu ya malezi bora kwa wazazi ili kuwakumbusha majukumu yao.
  Pia kuwawajibisha wazazi watakaokaidi na tayari matangazo yamekwishaanza kubandikwa kwenye mbao za matangazo mijini na vijijini kuanzia ngazi ya mtaa, kata na wilaya.
  “Lakini pia kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwafanyia ukatili na kuwatumia watoto kwa maslahi yao binafisi,” anasema Valeria na kuongeza:
  “Tunafanya utafiti kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa ili kujua idadi ya watoto ambao hawako majumbani kwao, pamoja na kukutana na wadau wanaohusika na jamii kila mwezi kukumbushana namna ya kuondoa tatizo la ukatili kwa watoto ikiwamo kuwatumikisha.”
 
Taarifa ya RPC Konyo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, anasema kuwa mama wa mtoto huyo alikwishatoroka na sasa jeshi hilo linamsaka kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi mtoto wake.
  Kamanda Konyo anasema mwanamke huyo alifanya makosa hayo Novemba, mwaka jana, na kutoroka baada ya kugundua kuwa anatafutwa na polisi na taarifa za kiintelejensia zinasema kwa sasa anaishi mkoani Shinyanga.
  Kamanda Konyo ameomba polisi wenzao wa Shinyanga kuanza kumsaka mtuhumiwa huyo kwa kuwa ameshafunguliwa shitaka la shambulio la kudhuru mwili.
  “Hilo suala tunalifuatilia na tumeshagundua mama huyo baada ya kutenda kosa alikimbilia mkoani Shinyanga, hivyo anatafutwa,” anasema Konyo, aliyewataka wananchi kusaidia kutoa taarifa za sehemu alipo mama huyo ili akamatwe.
  Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa binti huyo baada ya kujisalimisha kwa msamaria mwema, baba yake wa kambo alimfuata huko na kuamua kuishi naye na kuendelea kumtunza, taarifa ambazo pia zimethibitishwa na Koplo Butono Kasusura wa Jeshi la Polisi upande wa Dawati la Jinsia.

By Jamhuri