Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yote anayotujaalia. Naamini kuwa ni kwa uwezo na mapenzi yake Mungu ndiyo maana tunayaweza yote tuyatendayo katika maisha yetu ya kila siku.
 Hivyo, ni wajibu na haki kumshukuru yeye aliye na uwezo na nguvu kuliko vyote. Hakuna ambaye yuko chini ya mbingu anayeweza kujidai kuwa mkuu kuliko Mungu tunayemwabudu na kumtumikia kupitia shughuli zetu za kila siku.
 Kwa utangulizi huo ni wazi kuwa hata rais tunayemtazamia baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu sifa yake ya kwanza ambayo mimi nathubutu kuisema kuwa iwe ndiyo sifa kuu kuliko zote: awe mcha Mungu na amtangulize Mwenyezi Mungu kila wakati, amhofu yeye na zaidi ampe sina na utukufu. Akifanya hivyo, nina hakika Tanzania itakuwa nchi iliyojaa ‘maziwa na asali’ na watu wake, yaani sisi Watanzania tutaneemeka kutokana na rasilimali tulizonazo ndani ya nchi yetu.
  Kinyume cha hivyo itakuwa laana na maangamizi kwa Taifa lenye maliasili nyingi; na watu wake wataendelea kuteseka kwa misingi kuwa mkono wa Mungu wenye nguvu utakuwa mbali nasi (The divine arm of the Almighty God will twist away from us).
  Gazeti moja lililochapishwa Ijumaa, Februari 20, mwaka huu liliainisha ajenda 10 kwa mrithi wa Jakaya Kikwete na kuongeza kuwa ni zile zilizotajwa na wananchi kutaka rais ajaye azisimamie ili kuiwezesha nchi isonge mbele.
  Hizo ajenda 10 zinaangaliwa kuwa ni kete za Uchaguzi Mkuu 2015. Ajenda zilizotajwa na wananchi na kuwekwa bayana ni ardhi, kodi, maji, ajira, miundombinu, elimu, mihadarati, rasilimali, kilimo na Mahakama ya Kadhi.
 
Mambo ya msingi ya kuzingatiwa
 
Nimetanguliza sifa ya kumtanguliza Mwenyezi Mungu wakati wote na katika utendaji kazi wake wa kila siku. Hii ninamaanisha kuwa rais ajaye akimweka Mungu mbele ataweza kusimamia mustakabali wa nchi yetu kwa kutenda haki, atakuwa muwazi na mkweli, atakuwa na upendo wa hali ya juu kwa watu wake na kuwahudumia ipasavyo bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile na kuhakikisha tunagawana mapato au urithi wa Taifa letu kwa upendo, amani, haki na usawa.
 Ataweza kusimamia maendeleo ya Taifa na watu wake bila woga na hofu ya mtu yeyote, maana yeye (rais) atakuwa ndiye kiongozi mkuu wa haki na amani ndani ya Taifa letu na masuala kama ufisadi, rushwa, kuwaua albino au polisi kunyanyasa raia bila sababu za msingi itakuwa ni historia. Atasimamia sheria na haki itatendeka na usalama vitakuwapo kwa kila raia na mali zake. Naamini atakuwa mkali kama simba kwa watendaji wasiofaa ambao kwa namna moja au nyingine hawatatenda haki au kutekeleza sheria ipasavyo.
 Rais atamhofu Mwenyezi Mungu tu na hatahofia binadamu ambao wanaweza kujitutumua kuudhuru mwili, lakini hawataweza kuiangamiza roho yake isipokuwa ni Mwenyezi Mungu tu aliye na dhamana ya kuiangamiza au kutoiangamiza roho yake. Rais wa aina hiyo ataweza kuzifanya kazi zake kifua mbele bila woga wowote na ataweza kufanya uamuzi sahihi na wa haki. Washauri wake wa karibu pia watakuwa makini mno katika kumpatia ushauri ambao yeye atauona unafaa kwa kuliletea Taifa letu maendeleo endelevu.
 
Ajenda kuu 10 zilizoainishwa na wananchi
 
Nirejee kwenye ajenda 10 ambazo wananchi wenzetu wameziainisha kama nilivyozitaja hapo juu. Kulingana na maelezo, wananchi wanataka rais ajaye azisimamie ajenda hizo ili kuiwezesha nchi isonge mbele.
 Nakubaliana nao kwa hoja ya kuzisimamia ili kuiletea maendeleo endelevu nchi yetu. Isipokuwa bado naziona kuwa ajenda hizo ni nyingi kusimamiwa kwa wakati mmoja. Vilevile, ni ajenda ipi itangulie na ajenda ipi ifuate, bado ni kitendawili.
 Watanzania tunahitaji kujadiliana kwa umakini kuweza kuainisha ajenda kuu za kitaifa kwa ajili ya kutuletea maendeleo endelevu. Yeye rais akiwa msimamizi mkuu na sisi tukachapa kazi ipasavyo nchi itasonga mbele. Ajenda 10 bado naziona kuwa ni nyingi mno kuweza kuzibeba kwa wakati mmoja ingawa nyingine ni matokeo na utekelezaji wa ajenda fulani kama nitakavyofafanua katika makala hii.
  Kusema kweli miaka 53 tangu tupate uhuru si muda mfupi na ndani ya miaka hiyo tumeshuhudia utawala au uongozi wa marais wanne wakitanguliwa na mwasisi wa Taifa letu: Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Yeye alisimamia ajenda kuu ya kuleta Uhuru na kuondoa dhuluma na uonevu ndani ya nchi yetu. Vilevile, akasimama kidete ukombozi wa Bara la Afrika kutoka mikononi mwa wakoloni na wakandamizaji.
  Pamoja na hayo, aliweza kusimama kidete katika kutuletea umoja wa kitaifa na kudumisha mshikamano kwa makabila zaidi ya 120 na watu wenye dini na imani mbalimbali. Alipotaifisha baadhi ya mali na huduma zilizokuwa zikiendeshwa au kumilikiwa na sekta binafsi, kwa mfano shule ambazo zilikuwa zinamilikiwa na vyombo au mashirika ya Kikristo, alilenga kuwezesha waumini wa dini nyingine kupata fursa ya kusomesha watoto na hivyo kujaribu kuleta usawa na umoja wa kitaifa.
  Kazi hizo hazikuwa lelemama. Zilihitaji ujasiri mkubwa na kuzitenda kwa moyo wa dhati kwa faida ya watu wote. Kwa maneno mengine, Mwalimu alituwekea msingi mzuri ambao umewawezesha marais waliofuata kuweza kuiongoza Tanzania kwa amani hadi kufika hapa tulipo.
 
Ajenda muhimu ni zipi?
 
Nathubutu kusema kuwa baada ya Mwalimu kung'atuka, kilichokosena hasa ni kutokuainisha vizuri na kwa usahihi wa hali ya juu vipaumbele muhimu ambavyo kila rais aliyetawala angehangaika navyo kwa ajili ya kutuletea maendeleo endelevu. Badala yake tumekuwa tukiendesha nchi yetu katika mfumo wa ‘kijumlajumla’ tu kiasi kwamba kuweza kuyaona matokeo halisi kwa miaka 50 iliyopita kidogo inakuwa vigumu.
  Ingelikuwa kwamba rais aliyefuata baada ya Mwalimu kung'atuka akawa na maono mazuri ya vipaumbele kama vitatu au vinne hivi ambavyo vingelipewa umuhimu wa kwanza na kutumia rasilimali za Taifa kwa kiwango cha asilimia 60 hivi na kuhakikisha utekelezaji wake unasimamiwa vizuri na kukamilika, hali ingekuwa tofauti na ilivyo sasa.
 Vivyo hivyo, kwa marais wote watatu wangelikuwa na utaratibu kama huo ninaousema ina maana tungelikuwa tunazungumzia ukamilishaji wa vipaumbele kati ya tisa na 12 kwa marais watatu baada ya Mwalmu; maendeleo ya Taifa letu yangekuwa mbali kuliko ilivyo sasa.
  Ninaposema vipaumbele vya kuanzia ninamaanisha ni mambo yapi ya msingi sana ambayo yakitekelezwa yangelichochea kukua kwa uchumi wa Taifa letu. Mimi si mtaalamu wa uchumi au masuala ya fedha, lakini waliobobea katika fani hizo wapo na wanaweza kutoa mawazo yao mazuri tu kuonesha kipi kifanyike kwanza ili kuwezesha masuala mengine kutoa matokeo makubwa na kwa faida ya nchi.
 Je, wataalamu kama hao wanapewa nafasi gani katika kuujenga uchumi imara wa nchi yetu?  Kama tunavyosikia kuwa kwa miaka 50 iliyopita nchi kama China, Brazil, India, Malaysia, Honk Kong na Korea Kusini, Afrika Kusini zimepiga hatua kiuchumi wakati miaka ya 1960 zilikuwa na hali isiyoridhisha kiuchumi. Lakini kutokana na uongozi imara na wenye dhamira thabiti na kwa kutumia wataalamu mahiri walionao na kuweka vipaumbele sahihi na kuwapo nidhamu ya hali ya juu katika kutekeleza mipango yao; nchi zao zimesonga mbele na kutuacha nyuma tunachechemea.
 Inawezeka kuna matatizo ya hapa na pale ndani ya mataifa hayo, lakini angalau maisha ya watu wao yanaboreshwa na maendeleo ndani ya miaka 50 yanaonekana. Hata sisi tunavutiwa kwenda kujifunza, kwa mfano Malaysia na China.
  Najiuliza nchi kama hizo zimetumia miujiza gani? Wao si binadamu kama sisi na wamezaliwa na kukua kama sisi, wakapata elimu kama tuliyoipata? Iweje sasa wasonge mbele sisi tuchechemee? Tutajitetea kuwa sisi ni maskini na rasilimali zetu zinahitaji utaalamu na mitaji mikubwa kama kuchimba madini?
Mimi naamini kuwa hatukujipanga vizuri na kuweza kuyaainisha mambo yetu kwa umakini na kuyasimamia ipasavyo.
 Kwa miaka mingi kumekosekana usimamizi na uongozi imara na wenye maadili mazuri. Siasa imetawala zaidi kuliko kitu kingine na ubinafsi na kutojali maslahi ya Taifa ni moja ya udhaifu wetu kwa miaka 50 iliyopita. Sasa wakati umewadia wa kusema basi (enough is enough) yatosha tubadilike kwa faida ya watu wote. Sisi si maskini kama inavyodhaniwa, bali kutojipanga vizuri na kuainisha vipaumbele vyetu kitaifa ndiyo hali inayotufanya tuonekane maskini.
  Wengine wanautumia mwanya huo kujinufaisha kirahisi. Wanakuja wanauchukua utajiri wetu sisi tukiangalia tu. Sasa rais ajaye aione hali hiyo na aifanyie kazi ipasavyo. Asimamie matumizi halali ya rasilimali za Taifa kwa kuwaletea maendeleo endelevu watu wake.
  Tunayo rasilimali ardhi; je, tunaitumia vipi kwa maendeleo yetu? Kusema kweli ardhi inatumiwa hovyo tu wakati ni rasilimali muhimu mno kwa maendeleo ya familia zetu na nchi kwa jumla. Tunayo rasilimali watu, je, kama Taifa rasilimali hii tunaitumia vipi kuliendeleza Taifa letu? Tunazungumzia ajira kwa Watanzania, maana yake nini? Serikali haitateremsha ajira kama mvua za vuli au masika. Ni lazima kuwepo mikakati mizuri ya kuwaendeleza Watanzania kielimu, kiafya na kimaadili.
  Fursa za ajira ni pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali ardhi vijijini na mijini. Kilimo kifanyike kibiashara (commercial farming). Vijana wawezeshwe na watalima kitaalamu na kibiashara. Vilevile, wajue kama ni kukopa watakopa wapi na kwa taratibu gani. Kilimo kuna fursa nyingi za ajira na kuweza kujitegemea kwa hali na mali. Vilevile, masoko ya mazao watakayolima na kupata matokeo mazuri, yako wapi na bei za mazao hayo zikoje? Zisiwe bei za kuwalalia wakulima au wafugaji na nani anahusika na masuala kama hayo.
  Tanzania Bara iangaliwe katika uhalisia wake kiikolojia na uwezo wa sehemu fulani kuzalisha mazao ya aina fulani (agro-ecological zones). Hii iwe ni msingi mkuu wa kupanga mipango muhimu ya kilimo na ufugaji na wakulima/wafugaji waelimishwe na kuwezeshwa kwa msingi wa kuzalisha mazao fulani muhimu katika sehemu husika au kufuga kibiashara katika maeneo fulani kuliko kuhangaika tu na kulima mfano mahindi wakati katika eneo husika mahindi hayafanyi vizuri; pengine zabibu au alizeti au mtama, au ufuta, au ulezi ndilo zao linalofaa.
  Watanzania wanataka waone mapinduzi halisi katika sekta ya kilimo na mifugo. Wataalamu wetu wote na kwa ngazi zote katika fani zote za kilimo na mifugo watimize wajibu wao kwa uadilifu mkubwa na kuwajibika ipasavyo. Kwa upandaji miti hali iwe hivyo hivyo. Watanzania wawezeshwe wapande miti kibiashara wakifahamu eneo fulani miti aina fulani inastawi vizuri na viwanda vya misitu vipewe kipaumbele ili wanaolima miti waweze kuwa na soko la uhakika.
  Karatasi nyingi zinaagizwa nje ya nchi pengine kutoka Afrika Kusini na kwingineko. Hakuna sababu ya kuendelea na hali hiyo. Viwanda vya aina hiyo viwepo hapa nchini na vifanye kazi kiuhalisia na kuleta maendeleo ndani ya Taifa letu.
  Wawekezaji wafanye hivyo kwa kuwekeza katika sekta ya misitu na nyuki na watapata faida tu maana soko kwa mazao ya misitu lipo la kutosha nchini na kwa nchi jirani. Sekta ya misitu na nyuki pia inao uwezo mkubwa wa kuwapatia Watanzania ajira za uhakika. Ni vizuri ikapewa kipaumbele na msukumo wa kutosha katika sera za nchi. Watanzania waone kuna fursa katika sekta ya misitu na nyuki. Wapande miti kama wanavyopanda mazao mengine ya biashara. Kwa mfano, wanavyopanda mazao kama kahawa, pamba, katani, tumbaku, chai, zabibu, alizeti, ufuta, korosho au mazao mengine.
  Vilevile, wananchi wapande miti ya matunda mbalimbali ambayo watapata matunda ya kutumia nyumbani na pia kuuza ili kujipatia kipato. Suala la kufuga nyuki lisisahauliwe maana watakaofuga nyuki watafaidika kutokana na uuzaji wa asali na nta na kuweza kuinua kipato chao haraka hivyo kuweza kuboresha maisha ya familia zao na jamii zetu kwa jumla.
 
Itaendelea

1497 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!