Mwaka 2015 una mshindo mkubwa kwa Watanzania, mshindo unaotokana na matendo matatu muhimu yanayowaweka wananchi katika hekaheka na fukuto la moyo.

Tendo la kwanza ni kupitisha au kutopitisha Katiba mpya inayopendekezwa kwao na Bunge Maalum la Katiba baada ya kupitisha Rasimu ya Katiba hiyo Oktoba 2, mwaka jana. Pili, ni kujiandaa kujiandikisha na kupiga kura ya kupata viongozi safi na tendo la tatu ni kutafuta kiongozi mwenye sifa na uwezo wa kutambua na kuwatumikia Watanzania.

Kabla ya kuanza kuangalia kwa undani mshindo huo, napenda kurudi nyuma miaka 20 iliyopita yaani mwaka 1995, kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika mjini Dodoma, katika harakati za kupitisha jina la mgombea urais wa Tanzania wa mwaka ule.

Katika mkutano ule, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahutubia wajumbe wa mkutano mambo manne ya kuangalia na kuchukua hadhari kabla ya kumchagua mtu atakayekuwa rais wa Watanzania.

Alisema; Kwanza, Watanzania wamechoka na rushwa. Pili, nchi yetu bado maskini, CCM ni chama cha maskini, wakulima na wafanyakazi; hakijawa chama cha matajiri. Tatu, wameanza kuzungumzia udini na mwisho alisema Watanzania wanaulizana makabila. Tuache kuzungumzia udini, tuache lugha ya ukabila. Kiongozi safi hawezi kutoka nje ya CCM.

Mwalimu Nyerere alimalizia hotuba yake kwa kuweka msisitizo kwa wapigakura, “Mpeni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya wananchi. Ninyi wapigakura mnaweza kutupatia kiongozi safi wa kuongoza nchi yetu.”

Mwaka 1995 ulikuwa pia mwaka wenye mshindo. Kwa mara ya kwanza Watanzania walishiriki Uchaguzi Mkuu uliohusisha vyama vingi vya siasa. Vyama vipatavyo 17 vilishiriki uchaguzi huo chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Ni vyama vinne tu — CUF, NCCR-Mageuzi, UDP na CCM — ndivyo vilivyoweka wagombea udiwani, ubunge na urais.

Vilivyosalia viliweka wagombea wa udiwani na wabunge tu.  Mgombea urais wa CCM, Benjamin William Mkapa, ndiye aliyechaguliwa na wananchi baada ya kuwabwaga chali Augustino Lyatonga Mrema wa NCCR-Mageuzi, Ibrahim Haruna Lipumba wa CUF, na John Momose Cheyo wa UDP.

Mwalimu Nyerere  aliwaamini na kuwapenda sana Watanzania na hasa wana-CCM kwamba walikuwa na usiri, uwezo, ukweli na uono wa kuchagua kiongozi safi atakayeondoa rushwa, umaskini, udini na ukabila katika karne hii ya ishirini na moja.

Ni kweli baada ya uchaguzi ule, Watanzania walijaa matumaini ya kuondokana na matatizo hayo kwa kuchagua viongozi wa kuweza kuwaongoza wananchi. Huku wakiweka utii kwa viongozi hao kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu na kujipa imani ya kuondoa matatizo hayo na kujenga taifa.

Baada ya miaka minne kupita (1995-1999) Mwalimu Nyerere aliiacha dunia na hakuona tena kilichoendelea wala kujua rai yake kwa wapigakura imetekelezwa; na kwa viongozi imesimamiwa kwa asilimia ngapi. Leo wapigakura bado wanaweweseka nani anafaa kuchaguliwa kuwa kiongozi kutokana na rushwa kuwa ni tabia, umaskini kuwa ni mazoea, udini ni wimbo na ukabila ni sifa ya kupata ajira au madaraka na zaidi kutaka kujenga chuki.

Kiongozi safi anawekwa na wapigakura wanaotambua mtu safi mwenye kauli na vitendo, mwenye uwezo wa kukemea, si kuonea wala kupendelea na wala si mwenye kujaa nongwa. Wapigakura wasio watambuzi si wapigakura wazuri! Wao ni wachafuzi na si wajenga Taifa.

Wakati wapigakura wanajiandaa kupiga kura Oktoba mwaka huu kupata viongozi safi, tayari vigingi na vishimo vinawekwa katika miundombinu ya kupiga kura. Mashine za BVR hazitoshi, hazina uhimili wa joto wala kusoma vidole vyenye usugu wa ngozi, na waendesha mashine hizo hawana ujuzi na ufahamu wa kutosha!

Awali ya mwezi Oktoba wa kupiga kura ni Aprili 30, mwaka huu, wanapotakiwa wapigakura hao kupiga kura ya maoni kwanza ya kupitisha Katiba mpya wanapata vikwazo. Vipi watafaulu kupata kiongozi safi kwa mtindo huo? Je, ni sahihi kusema hizo ni dalili za kuvuruga taratibu za Uchaguzi Mkuu ujao?

Wapigakura wa mwaka huu hawana budi kuangalia rushwa, umaskini, udini na ukabila kama bado upo. Nini kimefanya mambo hayo yaendelee kuwapo ima kwa kuzidi au kupungua. Ikumbukwe, kiongozi safi atapatikana kutoka kwa mpigakura mkweli.

Miaka ishirini iliyopita (1995-2015) ni sawa na kusema tani ishirini za tope kichwani zikibebwa na mpigakura wa leo! Je, mpigakura huyo ataendelea kubeba mzigo huo? Ni vyema basi busara ikatumika kabla na wakati wa kumchagua mgombea nafasi ya uongozi.

Ndiyo maana hivi karibuni, Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM alipohutubia Watanzania na wana-CCM katika sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya chama chao mjini Songea mkoani Ruvuma, alikumbusha rai ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na kusisitiza wananchi wawatoe viongozi safi na wawapigie kura viongozi safi, jambo ambalo linawezekana.

Timizeni wajibu wenu.

1713 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!