Yah: Na mimi nataka ukuu wa wilaya siku moja?

NA BARUA YA S.L.P.

Mzee Zuzu,

C/O Duka la Kijiji Kipatimo,

S.L.P. Private,

Maneromango.

Mtanzania Mwenzangu,

Yahoo.com/hotmail.com/excite.com/www.http,

Tanzania Yetu.

 

 

 

 

Kuna tetesi kwamba ukuu wa wilaya unagawiwa kama njugu na wanaosema hivyo labda wana taarifa kamili juu ya hilo. Mimi nipo Kipatimo sijui chochote juu ya hilo, lakini pia wamefika mbali hadi kuanza kuzungumza katika vyombo vya habari kama vile ni kweli.

Ukuu wa wilaya kwa lugha nyepesi ni uwakilishi wa rais katika eneo husika. Ni lazima awe na raghba (interest) ya rais aliyeko madarakani, ni lazima awe anaweza kumudu kasi na sera za kiongozi huyo mkuu wa nchi. Mkuu wa wilaya ni mtu muhimu katika nafasi yake ambapo kwa idadi ya wilaya hufanya Taifa ambalo litaenda sanjari na maendeleo ya Taifa.

Hii dhana imewafanya wanasiasa, vijana, na wananchi wengi kama mimi ambao siyo wanasiasa au viongozi kusikiliza maneno ya wasemaji juu ya hatima ya viongozi wetu hususani wakuu wa wilaya. Mimi bado sijavalishwa sawasawa njuga ili niweze kukubaliana na suala hili la ukuu wa wilaya kupewa hata wasio na uwezo.

Maendeleo ya taifa lolote lile duniani yanatokana na utendaji kazi wa wananchi wenyewe huku wakiona mifano ya viongozi wao. Maendeleo ya Taifa lolote hutegemea uwezo wa demokrasia kujadili hatima ya taifa lao katika kukabiliana na changamoto zilizopo na ndiyo maana leo tunajadili suala la ukuu wa wilaya wazi bila kuumauma maneno; wengi wao wakihoji dhima waliyonayo na uwezo wao katika kufikia malengo ya kiongozi mkuu wa nchi.

Leo mzee Zuzu nimejaribu kuoanisha mambo mengi ambayo yanazungumzwa na watu katika viunga mbalimbali vya nchi yetu. Huku ni kukosa taarifa nyeti kwa wakati na inawezekana pia usiri unaofanyika ndani ya Serikali yetu. Kwa ufupi, sifa za kuwa DC huenda wananchi hawazielewi na wanaona wanaochaguliwa labda hawatoshi.

Mimi sikubaliani na suala la kutosha ama kutotosha, isipokuwa vigezo vya uteuzi ndivyo vinavyotufanya wengi wetu tushawishike kuona labda yanayozungumzwa na wanasiasa wengine ni kweli. Hivyo basi, nilidhani ni wakati mwafaka kwa Serikali yetu kuweka bayana vigezo na masharti yanayozingatiwa ili tujue labda na mimi nataka ukuu wa wilaya siku moja.

Iwapo nitapata ukuu wa wilaya nitakuwa mwakilishi wa rais ndani ya wilaya nitakayopangiwa na kwa hakika nitafanya kazi za Serikali na siyo chama, na kazi hizo ni nyingi sana. Nitarejea sera za Ujamaa na Kujitegemea za wakati ule na kufanya kila linalowezekana kuwa mfano kwa wale wachache ambao namwakilisha kiongozi mkuu wa nchi. Sitaruhusu mambo ambayo nitahisi namwangusha kiongozi wangu.

Yapo mengi lakini kwa sera zile za Ujamaa na Kujitegemea nitaangalia kwa umakini uwepo wa mpasuko wa kisiasa ndani ya wilaya yangu kwa kuwa ndiye mwenyekiti wa kamati ya usalama, sitaangalia maslahi ya chama chochote kwa kuwa mimi ni mtumishi wa umma.

Nitaanza kazi na wote wanaoonekana na kuthibitika kuwa ni wabadhirifu wa mali za umma — mafisadi na mtandao mzima wa kujichukulia mali za umma bila utaratibu — kwa wadhifa wangu nitawafikisha mahakamani na hata ikibidi kuwa shahidi nitafanya hivyo kama kiongozi mwakilishi wa rais ambaye ninataka kumthibitishia aliyeniteua kuwa mimi ndiye DC wa kweli.

Nitainua kiwango cha uelewa kwa wananchi wangu wa wilaya ikiwamo elimu ya msingi na elimu ya wananchi wote juu ya uraia na haki zao. Hapa nitawawezesha kujua mambo mengi kama kutotoa rushwa, kulipa kodi na kadhalika. Ni muhimu wananchi wakajua kuanzia katika ngazi ya wilaya ambako DC ndiye mwakilishi wa kiongozi.

Nitahamasisha suala la uzalendo, elimu ya kupiga kura, kujitegemea, kuwawezesha wanawilaya yangu kuwa wajasiriamali, kuamini katika nguvu zao kujikomboa kiuchumi. Sitakuwa mwanasiasa wa chama chochote hapa nchini, nitatenga muda wa siasa kwa wananchi na kutoruhusu siasa kuwa jukwaa katika wilaya yangu.

Mwisho nitaangalia machukizo ambayo wananchi wanayo dhidi ya Serikali yao, huenda ni masuala ya kijamii, kiuchumi au kisiasa na nitafanyia kazi japokuwa wapo watakaoumia katika urais wangu wa wilaya. Hayo nitayafanya kwa dhati ya moyo wangu kwa kuwa siku ya mwisho nitakuwa shujaa wa kweli daima uongo na unafiki kwangu siyo sera ya Ujamaa na Kujitegemea.

Mungu wabariki marais wa wilaya zetu.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.