Ni chongo au kengeza?

Kuna msemo wa Kiswahili usemao ‘akipenda chongo huita kengeza’. Nimetoa msemo huu kwa nia njema tu ya kutaka kuangalia matukio kadhaa ya vurugu au ghasia, yanayotokea mara kwa mara hapa nchini na kusababisha baadhi ya watu wanaokuwa maeneo ya matukio kuumia, kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha yao.

Matukio ni mengi tunayasikia au kushuhudia yanapotokea kwenye michezo, mikutano, mihadhara ya dini, maandamano na vikao mbalimbali vya siasa, utawala na sheria. Matukio yote hayo yanapotokea husababishwa na watu wakiwa na sababu zao za kukubali au kukataa jambo au neno fulani — iwe la ukweli, uonevu, dhuluma, ubabe, ubinafsi, sifa, mbwembwe au madaraka — kutendwa dhidi ya watu wengine.

 

Unapotokea mgongano huo wa mawazo kati ya wanaotaka kutenda na wasiotaka kutendewa, ndipo tafrani ya maneno makali, matusi, ugomvi, vurugu au ghasia hutokea na watu kuumizana bila kwanza kutafakari madhara ya kupenda chongo kuita kengeza. Ila tafakuri hiyo hujitokeza baada ya watu wamekwishavurugana na kuumizana.

 

Chongo ni hali ya kuwa na jicho moja. Kengeza ni jicho lenye mboni iliyokwenda upande (macho makengeza). Ukweli, kuna mtu ana jicho moja, lakini wewe kwa kumpenda huyo chongo, unasema hana chongo ana makengeza. Mtu anapenda jambo fulani au kundi fulani.

 

Ukweli, jambo au kundi hilo lina makosa, wewe bado utalipenda na kulitetea katika makosa yake japokuwa unatambua kuwa jambo au kundi hilo lina makosa. Kwa desturi watu hawapendi chongo wanapenda makengeza.

 

Tunashuhudia wakulima wanavyogombana na ndugu zao wafugaji kuhusu maeneo yapi ya kilimo na yapi ya ufugaji. Wakulima wanalia mazao yao shambani yanaliwa na kuharibiwa na mifugo inayochungwa katika mashamba yao. Wasuluhishi wa migogoro kama hiyo wanasema kuwa wafugaji wakachungie wapi, wakati hii ni nchi yao! Wote hao wanapokaidi kufuata taratibu wanaingia katika vurugu na ugomvi.

 

Wachimba madini wadogo nao wanalia na kusema kuwa wananyang’anywa maeneo yao waliyoyagundua yenye madini na kupewa wachimbaji madini wakubwa wenye mitaji mikubwa na vifaa bora vya kazi (wakiwamo wawekezaji kutoka nchi za nje). Wasuluhishi wanatoa maelezo kuwa maeneo hayo ni ya wachimbaji wakubwa, wamepewa tangu miaka kadhaa iliyopita. Wachimbaji madini wadogo wanapopinga tayari watu wanaingia kwenye vurugu.

 

Waumini wa dini wanapofanya maandamano kudai haki yao ya kikatiba ya kuabudu, kukataliwa na polisi wasifanye maandamano, kwa malengo kuwa wanaleta udini, uchochezi, hawana kibali cha maandamano au kuna sababu za kiintelejensia. Waumini wanapokaidi na  kupinga maelezo ya polisi na kufanya maandamano, wanakutana na nguvu ya polisi na kutiwa adabu.

 

Wanasiasa wanapokusudia kufanya mikutano ya hadhara kuelezea sera za vyama vyao, au kukerwa na tamko fulani la Serikali, wakati mwingine hunyimwa kibali cha kufanya hivyo, na polisi hutoa maelezo kuwa wanataka kuhatarisha amani na utulivu uliopo.

 

Wanasiasa wanapokaidi na kufanya mikutano kwa lazima, Serikali huwaona ni wafedhuli, polisi huwatawanya na kutembeza mkong’oto kwa wanasiasa hao na kuvunja mikutano. Ghasia zinatokea. Mifano kama hiyo ipo mingi kuanzia kwa wanafunzi wa vyuo, walimu, madaktari, wanaharakati na vyama vya wafanyakazi, wote hao wanaangukia pale pale penye kupenda chongo kuita kengeza.

 

Septemba 6, 2013, tumeona kupitia vyombo vya mawasiliano na umma kitimtim na pata shika hadi nguo kuchanika na watu kuumizana ndani ya Bunge la Tanzania, baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kutoa amri ya kutolewa ndani ya Bunge kwa Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe, ambaye ni Waziri Mkuu Kivuli, kutokana na kiongozi huyo kukaidi kukaa chini baada ya kuambiwa mara tatu na Naibu Spika.

 

Sina haja ya kurudia kuelezea chanzo cha mkasa huo wa Naibu Spika Ndugai na Mbowe kwa urefu, la msingi ni kuangalia nani kaanzisha vurugu bungeni. Baadhi ya wananchi wanasema Naibu Spika huyo hakutumia busara kumtoa Mbowe ndani ya Bunge, angemsikiliza.

 

Wananchi wengine wanasema Mbowe hakutumia busara. Kwamba kwanini hakutii amri ya Naibu Spika ya kumtaka akae chini? Mbowe kweli alikataa kukaa chini, lakini akionesha dalili ya kutekeleza amri ya kutoka ndani ya Bunge.

 

Vipi wabunge wengine kuacha viti vyao — Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, na Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulambai — kuwa mstari wa mbele kumzuia Mbowe asitoke na kuwazuia askari wa Bunge wasifanye kazi zao.

 

Wananchi bado wanazungumza na kutoa maelezo na maswali anuwai, kuhusu mwenendo wa viongozi wawili hao (Ndugai na Mbowe), wabunge wa vyama vya upinzani, wabunge wa CCM na wabunge wa Chadema.

 

Matukio kadhaa yakiambatana na vurugu, kauli za matusi na kejeli ndani na nje ya Bunge zilizopata kutokea, zinatoa taswira gani kwa wananchi na mustakabali wa uongozi wa Taifa letu la Tanzania.

 

Bunge ni muhimili mmoja kati ya mihimili mingine miwili, Serikali na Mahakama ya dola Tanzania. Bunge linatunga sheria na kufuatilia utendaji kazi wa Serikali kuona kama inatimiza wajibu wake ipasavyo kwa kufuata taratibu (kanuni) zilizowekwa kisheria. Vipi muhimili huo unajiletea wenyewe sokomoko?

 

Tunaweza kuangalia kanuni za Bunge la Tanzania na tamaduni za mabunge katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, kote huko bado tutaelekezwa kutii amri ya Spika wa Bunge na Kanuni za Bunge husika. Busara si kanuni wala sheria ni hekima, akili na falsafa.

 

Je, wabunge waliocheza kilinge kisicho chao hawakustahili kutii kanuni za Bunge, hawakupaswa kuwa na busara? Au ndiyo ukipenda chongo kuita kengeza? Tafakari kabla ya kusema!