Upo usemi kuwa: “Wana macho lakini hawaoni, wana masikio lakini hawasikii.” Usemi huu haukuanza hapa Tanzania. Ni usemi wa zamani hata kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo. 

Katika Biblia, kwa mfano, neno ‘macho’ na neno ‘viziwi’ yametajwa kwenye vitabu vya Agano la Kale na Agano Jipya.

Katika Agano la Kale tunasoma Nabii Isaya aliomba hivi: “… walete vipofu walio na macho na viziwi walio na masikio…” (Isaya 43:8). Kumbe kwenye Agano Jipya tunasoma maneno “… Kwa kuwa wakitazama hawaoni na wakisikia hawasikii wala hawaelewi….” (Mathayo 13:13).

Kama ilivyokuwa zamani, hata hapa Tanzania bado tuna wananchi wenye macho lakini hawaoni maendeleo yoyote yanayotokea nchini.

Hawaoni licha ya kuwa na marais wanaoelezea kinagaubaga maendeleo yaliyopatikana nchini. Mtu mwenye akili timamu unabaki kushangaa, inakuwaje baadhi ya wananchi hawayaoni maendeleo yetu! Ni kweli wenzetu hawa hawaoni kwa macho yao au wanajifanya tu kuwa hawaoni?

Huko ni kujibaraguza! Inawezekanaje mtu usizione hizi barabara za lami zilizotapakaa nchi nzima, madaraja kama hili la Nyerere hapa Kigamboni, la Mkapa pale Rufiji, la Kikwete kule Malagarasi au la Magufuli pale Kilombero? 

Kwani hayapo kiuhalisia? Mtu unawezaje kubeza maendeleo kama hayo mpaka unadiriki kutamka eti hakuna lolote lililofanyika tangu tupate Uhuru?

Upo mradi wa umeme tunaita wa REA, umetapakaa vijijini kote. Kweli wenzetu wanaweza kuthubutu kusema hawaoni?

Nimesema tumebahatika kuwa na marais waliojitolea kuelezea maendeleo ya nchi hii kwa kutumia hata takwimu ili kuthibitisha yale tunayoyaita maendeleo endelevu.

Hapa ningependa nirudie maelezo ya marais hao katika sherehe tofauti na katika maeneo tofauti. Kauli ya hivi karibuni ilitolewa na Rais Dk. John Magufuli wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. 

Baada ya maelezo hayo nitarejea kwa yale yaliyotamkwa kwenye Uwanja wa Uhuru mwaka 1971, yaani miaka 10 baada ya Uhuru. Katika sherehe zote mbili hizo marais wametumia muda wao kuelezea maendeleo yaliyopatikana nchini.

Kwa kuwa Watanzania wengi ni vijana, watu waliozaliwa kati ya mwaka 1964 na kuendelea, na viongozi wetu karibu wote ni watu waliozaliwa miaka michache baada tu ya kuzaliwa kwa Chama cha TANU, ndiyo kusema wakati wa Uhuru walikuwa wadogo, na kwa vijana wetu wengi hawakuwepo kabisa wakati huo.

John Cheyo (maarufu kama Mzee Mapesa) alitamka pale Mwanza kuwa siku ya Uhuru alicheza usiku kucha; huku Profesa Lipumba alisema yeye ndiyo alikuwa shule ya msingi (nadhani darasa la nne). 

Kwa maana hiyo, ni vigumu kwa vijana wetu kufikiria ulinganisho wa kuyaona maendeleo kati ya namna alivyotamka Baba wa Taifa mwaka 1971 na namna alivyotamka Rais Magufuli mjini Mwanza mwaka 2019.

Vijana wengi katika nchi yetu hawana habari enzi za ukoloni hali ilikuwaje. Ndipo nimeona nielezee kidogo historia ya maendeleo kama ilivyotolewa na marais wetu wawili hawa na kama yupo yule asiyependa kuona, basi aendelee kujifanya kipofu.

Marais wametoa maelezo yao, sasa hapo mtu akimeza ni vema, la hataki kumeza, basi atapike. Ana hiari kabisa kufuata utashi wake. Halazimishwi!

Waingereza wana usemi: “You can take your horse to a river, but you cannot force her to drink water from the river.” Ukimaanisha unaweza kumpeleka farasi wako mtoni lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji.

Nia ya serikali kuelezea kuhusu maendeleo haya ni nzuri, lakini mtu kuyapokea au kuyakataa ni hiari yake, ila ukweli unabaki palepale. Maendeleo kwa maana ya mabadiliko katika nchi yetu yametokea na yanaendelea kutokea na yapo kiuhalisia.

Disemba 9, 2019 kumefanyika sherehe kabambe kule Mwanza. Haijapata kutokea! Umati wa washerehekeaji ulipita miaka yote tangu tuanze kufanya hiyo kumbukumbu ya Uhuru wa nchi yetu.

Katika jumla ya viongozi wetu wakuu wa vyama vya siasa walioshuhudia ni pamoja na wenyeviti wa Chadema, CUF, UDP na Chama cha Wakulima. Wasiobahatika kuhudhuria naona ni viongozi wa NCCR–Mageuzi, ACT-Wazalendo na CHAUMMA. Ilipendeza sana kuona hata wapinzani wameshiriki katika sherehe za mwaka jana za Uhuru pale Mwanza. Hatua hii inaleta faraja miongoni mwa wananchi.

Rais alisema wazi sababu za maadhimisho yale kutofanyika mwaka 2015 na 2018 na kwamba uamuzi wa kuyapeleka maadhimisho hayo mkoani Mwanza ni kubadili tu kufanya mambo kwa mazoea. 

Hii ya kutofanya tamasha lile kwa mazoea ya mapokeo ya Uhuru wetu Walatini walisema: “Varietas dilectat”, kwa Kiingereza ningesema: “Variety pleases” – yaani mabadiliko hupendeza na kweli sherehe zile za Uhuru zilifana sana.

Tena ziliwapa fursa na wakazi wa Kanda ya Ziwa kujionea miradi ya maendeleo ya kimkakati. Walioshiriki walitoka mikoa ya Shinyanga, Siminyu, Mara, Geita, Kagera na Mwanza yenyewe.

Jambo moja la muhimu ni kule kuanza kuonyesha moyo wa maridhiano kati ya vyama vyetu vya siasa. Wakati rais anamalizia hotuba yake ndipo aliona ulikuwa wakati muafaka kuwakaribisha viongozi wenzake kutoka vyama vya siasa angalau wausalimu umati ule pale Kirumba.

Hapo ndipo mimi ninaona ulipofunguliwa mlango kwa viongozi wengine kujionea yale yaliyotokea katika miaka minne ya utawala wa Mwenyekiti wa CCM. Sijui au sina uhakika kama mipango iliandaliwa ya kuwapa fursa wale viongozi wa vyama vingine kutembelea miradi ya pale Mwanza kama vile ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria, ukarabati wa zile meli kongwe, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza na kadhalika.

Kumekuwa na minong’ono kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa ‘eti tangu tupate Uhuru hakuna kilichofanyika!’ 

Maneno ya namna hiyo miongoni mwa viongozi katika nchi yetu ni upofu wa kujitakia. Hali ya kutokuyakubali yale macho yanaona ni upofu. Kwa lugha ya mitaani tunasema ni ‘kujibaraguza’ na ni kutokutaka kuona kile kilichopo.

Kama bado akili ya mtu inakataa kukubali uhalisia wa maendeleo katika nchi yetu kwa wale waliokwenda Mwanza, kama walitumia usafiri wa anga, je, hawakupanda ndege zetu hizi za ATCL? Kama walipanda, je, bado tu hawakubali kuwa yapo maendeleo katika huo usafiri wa anga?

Ingesaidia sana kama viongozi wetu wa vyama vya siasa nao wangepangiwa ziara mahususi kutembelea hii reli yetu ya kisasa (SGR) inayojengwa, wapelekwe na kule Rufiji kuona kinachofanyika katika mradi wa kufua umeme kutoka katika lile bwawa la Mto Rufiji – Nyerere Hydropower Dam.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

80 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!