Watanzania tuliadhimisha miaka 58 ya Uhuru jijini Mwanza, Disemba 9, 2019, na Januari 12, 2020, wiki iliyopita tuliadhimisha miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar mjini Unguja. 

Hivi sasa tunajiandaa tena kuadhimisha miaka 56 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ifikapo Aprili 26, 2020.

Uhuru, Mapinduzi na Muungano ni matukio muhimu kwa kila Mtanzania aliyezaliwa Tanganyika au Zanzibar. 

Mosi, ndipo ulipoanzia Uhuru wetu na kurudisha utu wetu. Pili, uliposimamia ukombozi wetu wa fikra, siasa na uchumi. Tatu, yalipoanzia maendeleo yetu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Ni wazi kunena kuwa tunapoadhimisha matukio haya tunaukumbuka utu wa wazee wetu (waasisi) na kuvijali vizazi vyao (sisi na vijavyo). Tunathamini kazi zao, uwezo wao na ushujaa wao katika harakati na mapambano dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na Kiarabu.

Katika utaratibu huu wa kuwaenzi waasisi wa Uhuru, Mapinduzi na Muungano, jamii imewapa majina watoto wao. Wapo wanaoitwa Uhuru, Mapinduzi na Muungano. Hakika Mtanzania na mwananchi huru hana sababu ya kutoadhimisha matukio haya.

Wakati wa maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika na miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, marais wa nchi hizi wametoa hotuba zilizoelezea mafanikio ya kijamii na kiuchumi na changamoto zinazojitokeza katika kuwaletea maendeleo wananchi, zikiwemo rushwa na demokrasia.

Watanzania wa Bara na Visiwani kila siku tunaona, tunasikia na tunashiriki katika miradi na shughuli mbalimbali za jamii katika kujiletea maendeleo yetu. Tunayo maendeleo ya watu na ya vitu. Maendeleo haya yanategemeana katika kumfikia Mtanzania yeyote.

Yanapoletwa maendeleo ya vitu, yaani miundombinu ya maji na nishati, yanapojengwa majengo bora ya shule na tiba, mitambo na viwanda, ni kupeleka huduma kwa wananchi. 

Zinapotengenezwa njia bora za usafirishaji na kununua vyombo bora vya kusafiria ni kuwarahisishia wananchi, wafanyabiashara, wataalamu mbalimbali na viongozi wa aina zote katika jamii kusafiri na kusafirisha bidhaa zao.

Watanzania wenye umri zaidi ya miaka 58, wanatambua na kukubali kuwa tangu tupate Uhuru na kufanya Mapinduzi, serikali zote mbili zimefanya kazi nzuri ya kuleta maendeleo ya jamii. Wachache wenye lao jambo wanajifanya Lila na Fila. Hawa si wema katika Muungano wetu. Jicho liwaangazie.

Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein katika hotuba zao wamezungumzia mafanikio yaliyopatikana ya maendeleo ya watu na ya vitu katika miaka hiyo 58 na 56. Nazipa kongole serikali zote hizi.

Jambo jingine lililozungumziwa ni usalama wa watu, mali na vitu. Nchi yetu lazima iwe katika hali salama na ya amani. Uhuru, Mapinduzi na Muungano wetu kila kimoja hakiwezi kuwa na maana iwapo Tanzania si salama. Usalama huu unategemea sana ukweli wa Watanzania.

Tanzania kuwa salama maana yake ni viongozi na wananchi wao kujirekebisha na kuacha tabia ya upeke peke na uchochezi wa kisiasa, kijamii na kiuchumi. 

Ipo tabia ya watu fulani kutamka hadharani kwamba, katika miaka 58 au 56 hakuna kilichofanyika katika maendeleo ya jamii.

Maneno kama haya kutoka kinywani mwa Mtanzania anayekula, anayelala na anayevuta pumzi kwa raha nchini Tanzania, ni mtu kiburi, mwenye dharau na mwenye ujinga usio kubali tiba.

Ipo haja ya kupiga mbizi kuitafuta Tanzania ilipo na kuiangalia haiba yake. Kweli hakuna kilichofanyika, au ni kauli za kina pangu pakavu tia mchuzi wakati bakuli la mchuzi limo mikononi mwa beberu?

497 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!