Desemba 31, 2012 Rais Jakaya Kikwete alitangaza matokeo ya sensa ya watu na makazi, iliyofanyika Agosti mwaka huo. Rais Kikwete alitangaza kwamba kwa mujibu wa matokeo ya sensa hiyo idadi ya Watanzania ni 44,929,002.

Kiongozi huo wa nchi alisema kwamba inakisiwa kuwa mwaka 2016 idadi ya Watanzania itakuwa imefikia milioni 51.


Akasema: “Sasa hii ni kazi kubwa kweli. Ndugu zangu ongezeko hili linatokana na watu kuzaliana na sasa tumefika wakati mwafaka wa kuangalia namna bora ya kuwa na uzazi wa mpango, ili kuwa na familia ambayo mtu ataweza kuilea na kuitimiza mahitaji yake.”


Ukitafakari kwa makini maneno hayo ya Rais Kikwete, utakubali kwamba alikuwa sahihi kabisa kusema hivyo.


Hata Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuzungumza umuhimu wa kufuata uzazi wa mpango kwa lengo hilo la kuwa na familia ambayo kila mtu ataweza kuilea na kuitimiza mahitaji yake.


Mwalimu Nyerere alisema: “Si kitu kama tunashindwa kupeleka roketi mwezini, lakini ole wetu kama tunashindwa kuwapeleka watoto wetu shuleni, au kuwalisha, au kuwavisha inayostahili.”


Katika kupanda gharama za maisha, familia isiyofuata uzazi wa mpango lazima itashindwa kuwapeleka watoto wote shuleni, kuwalisha na kuwavisha inavyostahili.


Cha ajabu ni kwamba baada ya Rais Kikwete kuwataka kwa haki kabisa Watanzania wafuate uzazi wa mpango, alijitokeza Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, ambaye amempinga Rais kwa kuwataka Watanzania wafuate uzazi wa mpango.


Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro, Arusha, Golugwa alimlaumu Rais Kikwete kwa kuwataka Watanzania wapunguze kasi ya kuzaana.

Golugwa anadai kuwa kitengo cha Rais Kikwete kuwataka Watanzania wafuate uzazi wa mpango, ni matokeo ya Rais kushindwa kuelewa namna ya kutumia idadi ya wingi wa watu kiuchumi.


Kauli hiyo ya katibu huyo wa Chadema ina mambo matatu; hapana shaka inawakilisha msimamo wa chama hicho kuhusu kasi ya ongezeko la watu, si kauli yake binafsi.


Kwanza, kwa nafasi yake kama katibu wa mkoa hapana shaka hawezi kuropoka. Anatoa msimamo wa chama chake. Pili, kauli hiyo ameitoa kwenye mkutano wa hadhara, hakuitoa kwenye mazungumzo ya kawaida. Kwa hivyo, pale alikwenda kueleza masimamo wa Chadema kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na hili la uzazi wa mpango.


Tatu, tangu  katibu huyo wa Chadema alipotoa kauli hiyo potofu, uongozi wa taifa wa chama hicho haukumpinga. Huo ni ushahidi mwingine unaothibitisha kwamba sera ya Chadema ni kuwahimiza Watanzania wazaane bila mpango. Sababu za chama hicho kuwataka Watanzania waendelee kuzaana kwa kasi zimetajwa.


Kwanza, Chadema inaelezwa vizuri sana namna ya kutumia idadi ya wingi wa watu kiuchumi, lakini wameshindwa kueleza namna ya kutumia idadi hiyo kubwa ya watu kiuchumi.


Pili, Chadema inaona kwamba kwa maneno ya Golugwa; “Hata kama tungezaliana tukafikia mabilioni ya watu hatuwezi kuijaza Tanzania.”


By Jamhuri