Kampuni ya Taifa ya Uwekezaji (NICOL), imemsafisha mfanyabiashara maarufu nchini, ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi kuhusu tuhuma za kuidhoofisha kampuni hiyo.

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya NICOL, Gideon Kaunda na mmoja wa waanzilishi wa kampuni hiyo, Jaji msataafu Mark Bomani wamemsafisha Mengi katika Mkutano Mkuu wa wanahisa uliofanyika Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.


Awali kabla ya kusafishwa, Mengi alitishia kuondoka mkutanoni iwapo Mwenyekiti hangemweleza msimamo wa NICOL kuhusu tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake kwamba ameiua kampuni hiyo.


“Mengi yameelezwa mitaani kwamba Mengi kaua NICOL. Kama bado hayo yapo niombe mamlaka niondoke hapa [mkutanoni],” alisema Mengi na kuendelea:


“Yaliyoelezwa kuhusu mimi ni uongo. Wanasiasa wameingilia, Naibu Waziri mmoja ameshiriki kueneza habari hizo, sasa hali hiyo inanipa shida, nataka kujua hali ilivyo juu yangu ndani ya NICOL nione kama ninaendelea kukaa, au nitoke.”


Akijibu hoja hiyo, Kaunda alisema kitendo cha Mengi kuhudhuria mkutano huo (kama mwanahisa) kinadhihirisha kwamba yaliyosemwa juu yake ni ya uongo.


“…mimi sikubaliani na shutuma hizo, vyombo vya habari vina matatizo yao, sina tatizo na Mengi ni mwanahisa na mwanzilishi wa NICOL, hilo naomba tuliache na tutoke hapa tumelielewa vizuri,” amesema.


Naye Jaji Bomani katika kumtetea Mengi alisema: “Ninapenda kumsafisha Mengi, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji [ya NICOL]. Aliposikia tuhuma zinazomkabili aliandika barua ya kujiuzulu.”


Kwa upande mwingine, Kaunda ameuambia mkutano huo kwamba malumbano baina ya wanahisa wa NICOL yamesababishwa na uozo wa uongozi wa zamani wa kampuni hiyo.


Baada ya majadiliano, mkutano huo wa wanahisa wa NICOL umeazimia kwamba Mwenyekiti wa zamani wa kampuni hiyo, Felix Mosha alazimishwe kukabidhi ofisi viongozi wapya washike hatamu.


“Mosha akishindwa kuachia ngazi na kukabidhi ofisi kwa hiari tutamtoa kwa lazima kuiokoa NICOL,” amesisitiza Kaunda.


Inaelezwa Mosha ameongoza NICOL kwa kipindi cha miaka 10 huku kampuni hiyo ikikabiliwa na matatizo lukuki ikiwamo hasara ya Sh bilioni 9.874 kati ya mwaka 2007 na 2009.


5583 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!