NIDA inavyoliwa

*Yakwama kutoa Vitambulisho vya Taifa kwa wakati

*Mabilioni ya fedha za tozo yaachwa bila kukusanywa  

*Ukarabati wa magari, mitambo haujafanyika bila sababu

*Mkuu Kitengo cha Mawasiliano asema: ‘Hatuna majibu’

DAR ES SALAAM

NA DENNIS LUAMBANO

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatajwa kushindwa kutekeleza majukumu yake sawasawa na kugeuka kikwazo katika upatikanaji wa vitambulisho vya taifa, huku ikilisababishia taifa hasara ya mabilioni ya fedha.

Taarifa kutoka ndani ya NIDA zinaweka wazi kuwa iwapo hali hiyo itaachwa iendelee, Watanzania wasahau kufaidika na uwepo wa vitambulisho hivyo kutokana na kasi ndogo ya uchapaji wake.

“Tangu mashine za kuchapia vitambulisho zinunuliwe mwaka 2019, zimekuwa zikizalisha wastani wa vitambulisho 1,000 tu kwa saa kutokana na kasoro mbalimbali, badala ya vitambulisho 4,500 vilivyotarajiwa kuchapwa kwa saa,” anasema mtoa taarifa wetu ndani ya NIDA.

Uzembe mwingine unatajwa kuwapo katika ununuzi wa vifaa wezeshi au mashine ambazo hazijakamilika.

“Kwa mfano, unakuta mashine imenunuliwa lakini haina HSM (kifaa cha kuweka usiri wa taarifa za ndani ya kitambulisho) au ‘compressor’, unadhani kazi itafanyika hapo?” anasema na kuhoji mtoa taarifa wetu.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mbali na kasi ya uzalishaji wa vitambulisho kuwa ndogo na kusababisha ucheleweshaji, uongozi wa NIDA umesitisha utoaji wa vitambulisho vya awali (raw cards) kwa hoja kwamba teknolojia yake imepitwa na wakati.

Hata hivyo, kwa hali halisi vitambulisho hivyo vingeweza kutumika hata katika mitambo mipya.

“Si kweli kwamba enzi za ‘raw cards’ zimepitwa na wakati. Zinaweza kuendelea kutumika hata sasa. Hivi ninavyozungumza na wewe kuna rundo la ‘raw cards’ zaidi ya milioni 10 zenye thamani ya Sh bilioni 10!

“Hata mashine hizi mpya zinao uwezo wa kuzalisha vitambulisho kwa ‘raw cards’ za zamani. Kinachoonekana hapa ni ujanja tu wa watu fulani kutaka kununua ‘raw cards’ mpya kwa faida binafsi,” anasema ofisa mmoja ndani ya NIDA aliyezungumza na JAMHURI.

Uchunguzi huo umebaini pia kuwapo kwa ucheleweshaji wa vitambulisho vya wageni na kusababisha wasajiliwe kwa kupewa namba ya NIDA (NIN) pekee.

Baadhi ya wageni hawa ambao huishi nchini kwa muda tu, wamemaliza mikataba yao pamoja na vibali vya kazi pasipo kupata vitambulisho vya NIDA.

“Hali hii huwaletea usumbufu wakati wanapohitaji kuhuisha vitambulisho vyao. Shughuli hiyo hushindikana kwani huhitajika kuwapo kitambulisho (si namba) cha awali. Sasa kwa nini kuwaletea wawekezaji usumbufu usio na maana katika nyakati hizi tunapowahitaji sana?” anahoji.

Kwa upande mwingine, JAMHURI limeelezwa kwamba benki kadhaa za biashara zilizopo nchini zilizopewa mashine za kusoma kadi za NIDA (smart card readers) zaidi ya 100, hazijaanza kutozwa tozo maalumu lililokusudiwa kwa kuzitumia.

Mashine hizo zilinunuliwa na serikali kwa mabilioni ya fedha za walipa kodi.

Matengenezo ya mashine

Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa NIDA ilikuwa na mkataba wa awali na mkandarasi, IRIS Corporation Berhad, wa kuzifanyia matengenezo mashine za kuchapisha vitambulisho mali ya mamlaka hiyo, lakini hadi wakati huu mashine tatu kati ya tano hazijafanyiwa matengenezo, hivyo kuzorotesha kasi ya utoaji vitambulisho.

Lawama zaidi zinaelekezwa kwa maofisa wa juu wa NIDA kwa kushindwa kusimamia ipasavyo maduhuli na kuziacha kampuni nyingi kutumia taarifa za NIDA bila kuzilipia, hivyo kuipotezea serikali mapato.

“Huduma za utambuzi wa watu zikifanywa vizuri ni chanzo kikubwa cha mapato ya serikali, lakini NIDA haikusanyi fedha. Kwa mfano kuna kampuni zinatumia taarifa zilizomo katika mfumo wa utambuzi na usajili wa watu bila kulipia wakati Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu na Kanuni zake zinaelekeza kutoza Sh 500 kila unapotaka kupata taarifa za mtu.

“Mwaka 2019 wakati wa usajili wa laini za simu za mkononi kwa kutumia taarifa za NIDA, serikali ilipata hasara ya zaidi ya Sh bilioni 22 kwa kuwa iliruhusu taarifa hizo kutumiwa bila kuwapo mkataba kama utaratibu unavyoelekeza,” anasema mtoa taarifa wetu.

Wafanyakazi kadhaa wa NIDA wamelieleza JAMHURI kuhusu kuwapo uvunjifu wa taratibu za utumishi wa umma na unyanyasaji ndani ya mamlaka.

“Watumishi tunalipwa stahiki pungufu au kutolipwa kabisa kinyume cha taratibu. Kwa mfano, wakati wa usajili wa laini za simu za mkononi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alielekeza tufanye kazi kwa muda wa ziada kwa mwezi mmoja na kila mtumishi alipaswa kulipwa kati ya Sh 600,000 hadi Sh 900,000 kutokana na cheo chake. Hatukulipwa.

“Badala yake tulilipwa kama ‘honoraria’ ya kuanzia kati ya Sh 50,000 hadi Sh 300,000 kwa baadhi ya watumishi, viwango tofauti bila kuelezwa utaratibu gani ulitumika kupanga viwango. Kulikuwapo viashiria vya upendeleo,” anasema mfanyakazi mwingine aliyedumu NIDA kwa karibu miaka 10 sasa.

Vitendea kazi vingine

Kwa upande wa vitendea kazi kama magari, kuna taarifa kuwa kati ya magari 92 ya NIDA, ni magari 38 tu ndiyo yanayofanya kazi kwa sasa kwa nchi nzima kutokana na mengi kuwa mabovu, kwa kuwa hayafanyiwi matengenezo.

Hali hii inasababisha kuzorota kwa utendaji kazi wa mamlaka yenye ofisi katika kila wilaya.

“Mbali na magari, betri za ‘backup’ (za msaada nyakati za dharura) za mitambo ya Data Centre pale Kibaha zimeharibika zaidi ya mwaka mmoja sasa na hakuna mpango wa kununuliwa.

“Betri hizo zimekufa. Hali hii inaweza kusababisha upotevu wa data na kusababisha mfumo kushindwa kutumia taarifa za NIDA kwa wakati kama ikitokea hitilafu kubwa ya umeme; na kupoteza kanzidata au daftari la kumbukumbu ambalo ndilo lengo kuu la kuanzishwa kwa NIDA,” anasema ofisa mwingine wa kituo hicho cha Kibaha.

JAMHURI linafahamu kuwa tangu Mei mwaka huu NIDA imekuwa ikitumia umeme unaofuliwa na jenereta kwa ajili ya kuendeshea shughuli za kila siku, hali inayoiingizia hasara serikali.

Pia wino maalumu wa mashine mpya mbili za kutengenezea vitambulisho ambazo ndizo zinategemewa zaidi, umekwisha na uongozi haujakamilisha utaratibu wa kuagiza kutoka nje.

“Hata kama wataagiza leo, itachukua zaidi ya miezi sita (kuwasili nchini) kulingana na taratibu za ununuzi wa vifaa nje ya nchi. Maana yake uzalishaji wa vitambulisho utazidi kupungua,” anasema.

Vyanzo vya mapato vilivyotelekezwa

Mwandishi wa habari hii ameelezwa kwamba miongoni mwa njia ambazo kama zingetumika vema zingeiingizia serikali mapato makubwa ni tozo ya Sh 20,000 kwa anayepoteza kitambulisho au anayetaka kubadili taarifa.

Ada ya usajili wa wawekezaji ni dola za Marekani 100; dola za Marekani 50 kwa wafanyakazi wa kigeni na dola za Marekani 20 kwa wategemezi wao, wanafunzi, wamisionari na wakimbizi.

“Tayari kundi hili limesajiliwa lakini malipo hayajafanyika licha ya UNHCR (Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa) kuwa tayari kuwalipia,” anasema ofisa wa NIDA.

Mapato mengine yanayoweza kuifanya NIDA kujitegemea ni yanayotokana na miamala ya fedha kupitia simu za mkononi.

Tozo hilo ni la Sh 10 kwa muamala ili kusaidia utambuzi wa mtumaji na mpokeaji wa fedha, hasa yanapotokea makosa wakati wa kutumwa fedha kwa mlengwa. Kwa hali ilivyo sasa, makosa katika utumaji fedha husababisha upotevu wa fedha.

Waziri wa Mambo ya Ndani

Julai 19, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alionyesha kutoridhishwa na kasi ya uzalishwaji wa vitambulisho vya taifa.

Akiwa mkoani Iringa, Simbachawene amesema tangu alipoanza kupiga kelele kuhusu vitambulisho vya NIDA (mamlaka iliyo chini ya wizara yake), ni vitambulisho milioni mbili tu ndivyo vilikuwa vimetolewa.

“Mkurugenzi Mkuu wa NIDA (Dk. Arnold Kihaule) anapaswa kujitathmini na kama kazi imemshinda, amwambie Rais (Samia Suluhu Hassan) ili nafasi hiyo ichukuliwe na mtu mwingine,” anasema Simbachawene.

JAMHURI limemtafuta Dk. Kihaule kutaka kufahamu zaidi ni nini kinaikabili NIDA, na alipopigiwa simu yake ya mkononi Agosti 19, mwaka huu, alisema asingeweza kuzungumza kwa wakati huo kwa kuwa alikuwa na kikao na ‘Katibu Mkuu’.

Alipoendelea kutafutwa kwa siku zilizofuata, hakupokea simu.

Agosti 25, mwaka huu, JAMHURI lilifika Makao Makuu ya NIDA Dar es Salaam, ambako katibu muhtasi wa Dk. Kihaule alimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba: “Mkurugenzi Mkuu yuko safarini jijini Dodoma. Ukija kesho utampata.”

Hata hivyo, siku iliyofuata katibu muhtasi huyo aliliambia JAMHURI kuwa Dk. Kihaule asingeweza kukutana na mwandishi wa habari na kushauri aandikiwe maswali na kuwasilishwa Kitengo cha Mawasiliano cha NIDA kwa ajili ya ufafanuzi.

Maswali hayo yalipelekwa NIDA siku iliyofuata na wiki mbili baadaye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha NIDA, Geofrey Tengeneza, akasema mamlaka hiyo haina majibu ya maswali yote yaliyoulizwa.

“Maswali haya yalihitaji ufafanuzi kutoka katika vitengo mbalimbali. Hata Mkurugenzi Mkuu naye amepelekewa kwa sababu kuna mengine yanamhusu yeye binafsi. Lakini nikwambie tu kwamba, hatuna majibu ya maswali yenu yote mliyoyauliza,” anasema Tengeneza.