Baada ya miaka 30 kupita Nigeria inaweza kutoa rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Kwa mara ya mwisho Joseph Nanven Garba ndiye aliyekuwa Rais wa UNGA mwaka 1989 kutoka Nigeria.

Profesa Tijjani Muhammad Bande ambaye kwa sasa ni mwakilishi wa kudumu wa Nigeria katika Umoja wa Mataifa, ndiye anatarajiwa kushika urais wa UNGA kutoka kwa rais wa sasa, Maria Fernanda Espinosa Garcè, raia wa Ecuador.

Akidokeza kuhusu matarajio hayo akiwa ziarani hivi karibuni nchini Nigeria, Maria amesema: “Natarajia kushuhudia mabadiliko ya uongozi kwa utulivu mkubwa kwa nafasi ya Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa, mwanadiplomasia raia wa Nigeria ambaye ni profesa aliyeliweka jina la Nigeria kileleni, nadhani ndiye atakayechukua mikoba.”

Garcès alitwaa wadhifa huo wa urais wa UNGA mwezi Septemba 2018.

UNGA imewahi kuongozwa na raia kutoka Afrika, Asia, Ulaya Mashariki, Latin America, Caribbean na Ulaya Magharibi.

Bande anatarajiwa kushika wadhifa huo akiwa raia; pili, kuushika kutoka Nigeria tangu kuanzishwa kwa baraza hilo mwaka 1946.

Katika kuzungumzia suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Geoffrey Onyeama, amesema matumaini yake ni kwamba rais anayeondoka atakabidhi mamlaka hayo kwa Profesa Bande.

Onyeama amesema: “Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa anatarajia kukabidhi wadhifa huo kwa raia wa Nigeria. Kwa hiyo, Mnigeria huyo atachukua madaraka hayo miezi michache ijayo.”

Bande, mkurugenzi mkuu wa zamani wa Taasisi ya Sera na Masomo ya Kimkakati (NIPSS) alizaliwa katika Jimbo la Kebbi nchini Nigeria mwaka 1957. Ni msomi wa shahada ya uzamivu katika Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Toronto, Canada alikohitimu mwaka 1987. Amekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Usman Danfodiyo, Sokoto, kati ya mwaka 2004 na 2009.

By Jamhuri